Tunachojua kuhusu shambulio dhidi ya Wahouthi na mkakati nyuma yake

    • Author, Jonathan Beale
    • Nafasi, Mwandishi wa habari za ulinzi
    • Author, Jacqueline Howard
    • Nafasi, BBC News

Marekani na Uingereza zimefanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo ya Wahouthi nchini Yemen kwa lengo la kuzuia mashambulizi dhidi ya meli zinazopitia Bahari ya Shamu.

Mashambulizi hayo pia yaliungwa mkono na baadhi ya washirika wa Marekani na Uingereza.

Makombora yalirushwa usiku kucha hadi Ijumaa, na kugonga makumi kadhaa ya maeneo yaliyolengwa - huku baadhi ya majeruhi wakiripotiwa.

Waasi wa Houthi wanasema hawajakatishwa tamaa na mashambulizi hayo, lakini Marekani inasema kwamba mashambulizi hayo yameharibu uwezo wa kijeshi wa kundi hilo la waasi.

Lakini kundi hilo limeweza kunusurika na mashambulizi mabaya zaidi - ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya miaka kutoka kwa Jeshi la Wanahewa la Saudia.

Haya ndiyo tunayojua kuhusu mashambulizi ya Marekani na Uingereza kufikia sasa.

Ni maeneo gani yalipigwa?

Marekani inasema "ilifanya mashambulizi kwenye shabaha zaidi ya 60 katika maeneo 16 ya wanamgambo wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran".

Pentagon ilielezea maeno yaliyolengwa kama vile kama mifumo ya rada, maeneo ya kuhifadhi na kurusha ndege zisizo na rubani, hifadhi na vifaa vya kurusha makombora na zana za kudhibiti mashambulizi za Wahouthi.

Mashambulio yaliripotiwa katika mji mkuu wa Yemen Sanaa - ambao unadhibitiwa na waasi - pamoja na bandari ya Houthi Red Sea ya Hodeidah, Dhamar na ngome ya kaskazini-magharibi ya kundi hilo ya Saada.

Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Uingereza (MoD), mashambulizi ya Uingereza yalifanyika Bani, kaskazini-magharibi – eneo ambalo wizara ya ulinzi ilisema lilikuwa eneo la operesheni ya ndege zisizo na rubani - na uwanja wa ndege wa Abbs, ambao ujasusi wa Uingereza ulisema ni mahali pa kurushia makombora na droni.

Kulikuwa na mashambulizi 72 kwa jumla, kulingana na msemaji wa jeshi la Wahouthi.

Je, kulikuwa na majeruhi?

Msemaji huyo wa Houthi pia alisema wanachama wake watano wameuawa na wengine sita kujeruhiwa.

Pentagon ilisema mashambulizi hayo yalikuwa ni dhidi ya jeshi na hayakuwalenga raia na walitumia "silaha za usahihi".

Kuna mkakati gani hapa?

Rais wa Marekani Joe Biden amesema hatasita kuchukua hatua zaidi za kijeshi ikibidi.

Lakini Marekani pia imeweka wazi kuwa haitaki kuona mzozo unaopanuka zaidi katika Mashariki ya Kati.

Hilo linanaashiria kwamba hatua zozote za kijeshi zinazoongozwa na Marekani siku zijazo, ikiwa ni lazima, zitakuwa na kikomo tena.

Mashambulizi ya anga na makombora ya masafa marefu ni hatari na ya gharama kubwa kwa Bw Biden katika mwaka wa uchaguzi.

Kumbuka Marekani pia imekuwa ilifanya mashambulizi machache ya anga kulenga makundi mengine yanayoungwa mkono na Iran nchini Iraq na Syria katika miezi ya hivi karibuni.

Huenda mashambulio ya jana usiku pia yalishusha hadhi na kuharibu baadhi ya uwezo wa Houthi wa kufanya mashambulizi dhidi ya meli katika Bahari Nyekundu.

Lakini hadharani, angalau, wanabaki kuwa waasi. Bado wana uwezo wa kuanzisha mashambulizi zaidi.

Chaguo pekee lililosalia kwa Marekani na Uingereza ni - kulenga shabaha kutoka mbali.

Marekani ina uzoefu wa hivi majuzi wa hatua za kijeshi za moja kwa moja katika eneo hilo - kama vile kuwaweka wanajeshi wake ardhini.

Marekani na Uingereza walitumia silaha gani?

Sehemu kubwa ya milipuko hiyo ilitoka kwa ndege za Marekani.

Marekani ina chombo cha kubeba ndege katika Bahari Nyekundu, pamoja na vituo vya anga katika eneo hilo.

Meli za kivita za Jeshi la Wanamaji la Marekani zilirusha makombora ya baharini ya Tomahawk, ambayo yanaongozwa na GPS na yanaweza kuratibiwa kuruka kwa kukwepa, jeshi la Marekani linasema.

Ingawa hakuna takwimu maalum zilizotolewa kuhusu ni makombora mangapi yalirushwa, Marekani inasema zaidi ya silaha 100 zilizoongozwa kwa usahihi "za aina mbalimbali" zilitumika.

Wakati huo huo, Uingereza ilisema ilituma ndge nne za kivita aina ya RAF kutoka Cyprus, zikiwa zimebeba mabomu ya kuongozwa vilipiga lakini haijasema ni idadi ngapi ya makombora iliyofyatuliwa.

Ingawa Jeshi la Wanamaji la Ugingereza lina meli mbili za kivita katika Bahari Nyekundu, haziwezi kurusha makombora ya kushambulia nchi kavu na hivyo halingehusika moja kwa moja katika mashambulizi hayo.

Je, Wahouthi wanajibu vipi?

Akijibu kuhusu mashambulizi ya Ijumaa, kiongozi wa kundi hilo Mohammed al-Bukhaiti alisema Marekani na Uingereza "zitatambua hivi karibuni" hatua hiyo ni "ujinga mkubwa zaidi katika historia yao".

"Marekani na Uingereza zilifanya makosa kuanzisha vita dhidi ya Yemen kwa sababu hazikufaidika kutokana na uzoefu wao wa hapo awali," aliandika kwenye mtandao wa kijamii na kuongeza "kila mtu katika ulimwengu huu anakabiliwa na chaguzi mbili - ama kusimama na waathiriwa wa mauaji ya halaiki au kusimama na wahusika wake."

Msemaji mwingine wa kundi hilo alisema Marekani na Uingereza zilikosea kufikiria kuwa zinaweza kuzuia uungaji mkono wa Yemen kwa Wapalestina.

Iran, ambayo inawaunga mkono Wahouthi, imelaani mashambulio dhidi ya Yemen kama "ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya Yemen na uadilifu wa ardhi" na ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Msimamo wa Wahouthi kuhusu mashambulizi ya Bahari Nyekundu ni kwamba wanazuia meli zenye uhusiano na Israel kuvuka njia - kutokana na matukio ya Gaza.

Hapo awali walisema kwamba meli yoyote inayopelekwa Israeli au yenye vifaa vya Israeli ni "lengo halali". Hata hivyo, meli nyingi za kibiashara ambazo zimelengwa zinaonekana kutokuwa na uhusiano huo.

Je, Biden na Sunak wanahalalisha vipi mashambulio?

Bw Biden alisema mashambulio hayo ni "jibu la moja kwa moja" kwa mashambulizi ya Wahouthi katika Bahari ya Shamu.

"Mashambulizi haya yamehatarisha maisha ya wafanyakazi wa Marekani, mabaharia wa kiraia, na washirika wetu, yamehatarisha biashara, na kutishia uhuru wa usafirishaji bidhaa kupitia njia hiyo," alisema.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak aliongeza kuwa hatua hiyo ni "lazima na sawia" ili kulinda usafiri wa meli duniani.

"Licha ya maonyo ya mara kwa mara kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, Wahouthi wameendelea kufanya mashambulizi katika Bahari ya Shamu, ikiwa ni pamoja na dhidi ya meli za kivita za Uingereza na Marekani wiki hii tu," alisema. "Hii haiwezi kukoma."

Mashambulizi hayo ya Marekani na Uingereza yaliungwa mkono na washirika wap Australia, Bahrain, Canada, Denmark, Ujerumani, Uholanzi, New Zealand na Korea Kusini.

Katika taarifa, washirika hao walisema mashambulizi ya kutoka pande nyingi yalitekelezwaa "kulingana na haki ya asili ya mtu binafsi na ya pamoja ya kujilinda".

"mahsambulizi haya yalikusudia kuvuruga na kudhibiti uwezo ambao Wahouthi hutumia kutishia biashara ya kimataifa na maisha ya wanamaji wa kimataifa katika mojawapo ya njia muhimu zaidi za maji duniani," ilisoma taarifa hiyo.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi