Simulizi isiyojulikana na wengi ya mamluki wa Uskoti aliyeajiriwa kumuua Pablo Escobar

Mnamo mwaka wa 1989, timu ya mamluki wa Uingereza, ikiongozwa na Mskoti Peter McAleese, walisafiri hadi katikati ya himaya ya uhalifu ya mtu hatari zaidi duniani kwa lengo la kumuua.

Pablo Escobar alikuwa kiongozi wa genge la ulanguzi wa mihadarati Medellín nchini Colombia na mmoja wa wahalifu matajiri zaidi katika historia.

Genge lake liIlikuwa mtengenezaji na msambazaji mkubwa zaidi wa kokeini ulimwenguni, wakati huo ilithibiti hadi 80% ya biashara ya kimataifa ya dawa hiyo.

McAleese,ajenti wa zamani wa SAS - kikundi cha kikosi maalum cha Jeshi la Uingereza - aliajiriwa na kundi pinzani la dawa za kulevya ili kumuua Escobar.

Katika filamu ya Killing Escobar , iliyoonyeshwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2021, hadithi ya misheni hiyo - ambayo iliishia kutofaulu - na mtu aliyehusika inasimuliwa.

Msanii wa filamu David Whitney alisema McAleese, ambaye alizaliwa Glasgow mwaka wa 1942, alikuwa "mtu mgumu" ambaye alikuwa na "kutotulia kwa ndani".

Alilelewa katika kitongoji cha Riddrie katika Gereza la Barlinnie, ambapo baba yake - "mtu mgumu sana na mwenye jeuri" - alihudumu.

Katika filamu hiyo, McAleese alisema: "Nilifunzwa kuua na Jeshi lakini silika ya mapigano ilitoka Glasgow."

McAleese anadai aliondoka mjini na kujiunga na Jeshi akiwa na umri wa miaka 17 ili kutafuta njia ya kukabiliana na uchokozi wake.

Alijiandikisha katika kikosi cha Miavuli na baadaye akawa mwanachama wa kikosi cha 22 cha SAS.

Alihudumu huko Borneo na SAS, akishiriki katika vita vikali vilivyopiganwa msituni, kabla ya kustaafu kutoka kwa Jeshi la Uingereza mnamo 1969, uamuzi aliouelezea kuwa jambo baya zaidi kuwahi kufanya .

McAleese alihama kutoka kazi hadi nyingine" Alisema kwamba alijihisi mpweke na kwamba uchokozi wake ulizidi kuwa mbaya.

Mwanamume huyo alizidi kuwa mkali hadi akafungwa jela kwa kumshambulia mpenzi wake.

Alipopata tena uhuru wake, McAleese alitaka kuunda upya "msisimko" wa kazi yake ya Jeshi kwa kutafuta kazi kama "mlinzi" katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Angola na baadaye huko Rhodesia (Zimbabwe ya sasa), na pia katika Afrika Kusini.

Alikutana na Dave Tomkins huko Angola mwaka wa 1976. Tomkins hakuwa askari wa kawaida, alijua jinsi ya kufanya mikataba ya kuuza silaha.

Wawili hao wakawa marafiki wakubwa na Tomkims ndiye aliyemwendea McAleese ili kujitolea kushiriki katika misheni ya kumuua Escobar.

Jorge Salcedo, ambaye alikuwa sehemu ya kundi la Cali - kundi pinzani la ulanguzi wa dawa za kulevya nchini Colombia - alikuwa akiratibu shambulio hilo na alitaka Tomkins kuajiri timu kutekeleza hilo.

Mafunzo

McAleese alikuwa mtu wa kwanza alijaribu kumuajiri.

"Hawakuulizi kumuua Pablo Escobar isipokuwa kama una uzoefu unaohitajika," McAleese alisema.

"Sikuwa na tatizo la kimaadili kuhusu kumuua. Sijawahi kuchukulia kama mauaji. Nimeona kama mlengwa," alisema.

Kundi la wapiganaji wa Cali lilikuwa na imani kwamba Escobar angeweza kuuawa atakapoenda kwenye eneo lao la kifahari la Hacienda Nápoles .

Mali hiyo kubwa ilijumuisha bustani nzima ya wanyama iliyojaa wanyama wa kigeni, mkusanyiko wa magari ya kifahari na ya zamani, uwanja wa ndege wa kibinafsi, na mchezo wa fahali.

McAleese asafiri kwa ndege hadi ranchi hiyo ili kufahamu mahali hapo na akakubali kwamba inaweza kufanywa . Misheni hiyo ilikuwa ya kuvutia kwake.

Tomkins aliajiri timu ya mamluki 12. Kulikuwa na watu ambao walifanya kazi naye hapo awali na watu ambao walikuwa wamependekezwa kwake.

Jorge Salcedo aliwasaidia kuvuka mpaka na shirika la Cali lilifadhili kukaa kwao.

Kila mmoja wa wanaume hao angepokea dola za Marekani 5,000 kwa mwezi pamoja na gharamaza matumizi lakini Tomkins alipata dola za Marekani 1,000 kwa siku.

Filamu hiyo ilipata video zilizorekodiwa na Tomkins ambazo ni pamoja na matukio ambayo wanaume hao walionekana wakicheza na vibunda vikubwa vya pesa.

Mwanzoni walikaa katika jiji la Cali lakini huko waliingia kwenye hatari ya kuonekana na watu wengi sana, kwa hiyo wakahamia katika katika eneo la mashambani ambako walipewa silaha nyingi.

"Ilikuwa kama Krismasi. Kila kitu tulichohitaji kama silaha kilikuwa pale," McAleese alisema.

Mamluki walifanya mazoezi kwa bidii kwa ajili ya misheni yao lakini Tomkins na McAleese pekee ndio walijua lengo lao lilikuwa nani.

Kabla hawajafahamishwa, mwanakikundi mmoja aliamua kuondoka na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Aliuza habari zake kwa magazeti lakini hakufichua majina wala kutoa maelezo ya operesheni hiyo.

Wakati wa shambulio hilo ulipokaribia, watu hao walihamishia mafunzo yao msituni, ambapo waliweza kufanya mazoezi wakiwa na bunduki na mabomu bila kusikika

Mpango wa mashambulizi

Mpango wa shambulio hilo ulihusisha kutumia helikopta mbili kuwasafirisha hadi kwenye jumba la Hacienda Nápoles, ambapo mamluki wangelazimika kufyatua risasi kupambana na walinzi wa Escobar, kumuua na kurudisha kichwa chake kama taji.

Walipojulishwa na mtoa habari kwamba Escobar alikuwa kwenye shamba lake, walianza kuelekea lengo lao. Lakini shambulio hilo halikutokea kamwe.

Helikopta iliyokuwa imewabeba McAleese na Tomkins ilianguka ilipokuwa ikiruka chini kwenye mawingu juu ya Andes. Rubani aliuawa.

Wengine walinusurika lakini McAleese alijeruhiwa vibaya sana kuondoka eneo la tukio.

Akiwa na maumivu makali, alilala mlimani kwa siku tatu hadi alipookolewa.

Escobar alisikia kuhusu mpango wa mashambulizi na akatuma watu wake milimani kuwatafuta.

"Ikiwa Pablo angenikamata, ningekumbw ana kifo chenye uchungu sana, cha kusikitisha," McAleese alisema.

Badala yake, alitoroka na kujaribu kutimiza ahadi alizotoa kwa Mungu akiwa amelala kando ya mlima.

McAleese alikiri kwamba alikuwa "mtu mchafu, asiye na aibu; na kwamba alitambua kwamba alipaswa kubadilika.

Lakini alisema kwamba anachojutia si matendo yake katika maeneo ya vita, bali kushindwa kwake kama mume na baba.

"Nina majuto ya kutisha na hakuna hata moja linalohusiana nakazi yangu kama mwanajeshi katika maisha yangu," alisema akiwa na umri wa miaka 78, kama sehemu ya filamu hiyo.

Wakati huo alisema amepata "amani."

Baadaye, Pablo Escobar aliuawa kwa kupigwa risasi huko Medellín mwaka wa 1993 alipokuwa akijaribu kutoroka msako wa mamlaka

*Maelezo haya yalichapishwa mnamo Machi 12, 2021 na yalisasishwa kufuatia kifo cha Peter McAleese.

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah