Hunter Biden: Mapambano ya kashfa za mtoto wa rais wa Marekani

Hunter Biden, mtoto wa pili wa Rais Joe Biden, ameingia tena katika vichwa vya habari.

Julai, Hunter Biden (53) alisuluhisha mashtaka ya kodi na bunduki na kuepuka kifungo cha jela katika makubaliano na waendesha mashtaka. Lakini mpango huo umesambaratika, timu maalumu inaongoza uchunguzi dhidi yake, na kesi inakaribia Kwenda mahakamani.

Wabunge wa Republican pia wanachunguza madai ya ushawishi haswa katika biashara yake ya kigeni wakati wa baba yake akiwa makamu wa rais.

Wakati huo huo, mapambano yake binafsi - ya uraibu wa pombe na dawa za kulevya, na ugomvi katika mahusiano – hayo yote yameingia pia katika siasa.

Tunajua nini kuhusu Hunter Biden?

Utoto ulianza na msiba

Alizaliwa Wilmington, Delaware, 1970 na Joe Biden na mkewe wa kwanza Neilia. Alipata ajali akiwa na umri wa miaka miwili Disemba 1972, ikiwa ni chini ya wiki sita tu tangu baba yake kushinda kiti cha useneti.

Lori liligonga gari ya familia. Ajali hiyo iligharimu maisha ya mama yake na dada yake mdogo Naomi, huku ikimuacha akiwa amevunjika fuvu la kichwa na kaka yake Beau akivunjika mguu. Biden - ambaye hakuwa ndani ya gari - alikula kiapo chake kando ya kitanda chao hospitalini.

Baadaye Hunter alihudhuria Shule Georgetown University na Yale Law School na kuhitimu mwaka 1996. Kisha alijiunga na Kikosi cha Kujitolea cha Jesuit, kikundi cha Kikatoliki kinachohudumia jamii zilizotengwa.

Huko alikutana na mke wake wa kwanza, Kathleen Buhle, ambaye ni mwanasheria, na wakafunga ndoa mwaka wa 1993. Wana watoto watatu - Naomi, Finnegan na Maisy - lakini wana ndoa hao walitengana mwaka 2017.

Uraibu

Hunter alianza kunywa pombe akiwa kijana na anakiri kuwa alitumia kokeini akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Amekuwa akiingia na kutoka kwenye matibabu ya kuacha.

2013, alijiandikisha katika Jeshi la Wanamaji la Marekani na aliapishwa mbele ya babake - wakati huo makamu wa rais - katika hafla iliyofanyika Ikulu.

Lakini siku yake ya kwanza kabisa katika kituo cha jeshi la majini, alipimwa na kukutwa anatumia kokaini na akaondoshwa jeshini, jambo ambalo baadaye alisema lilimfedhehesha.

Kulingana na gazeti la New Yorker, alikunywa pombe kupita kiasi baada ya kifo cha kaka yake mkubwa, Beau, kutokana na saratani ya ubongo 2015.

Wakati wa talaka yao, mke wake alimtuhumu Hunter kwa, "kutumia kupita kiasi kwa masilahi yake binafsi (dawa za kulevya, pombe, makahaba, vilabu vya ngono, na zawadi kwa wanawake ambao ana uhusiano wa kimapenzi) huku akiiacha familia bila pesa za kulipa bili. ".

Akivunja ukimya mwaka jana kuhusu ndoa yake ya miaka 24 ilivyovurugika, aliiambia Good Morning America: "mapambano dhidi ya uraibu mkubwa wa dawa za kulevya, yalikuwa yakiniumiza na sikuwa nikiumizwa na mwanamke niliyekuwa nimemuoa."

Katika kitabu chake cha Beautiful Things - 2021, Hunter anakubali kwamba usaliti wake lilikuwa jambo la mwisho kuvunja ndoa yao.

Uchunguzi wa DNA 2019 uligundua kuwa ni baba halali wa mtoto aliyezaliwa na Lunden Alexis Roberts, mnenguaji kutoka Arkansas. Hunter alidai kuwa hakumbuki kukutana naye, lakini alikubali kupima DNA na hulipa karo ya mtoto.

Familia ya Biden haijakutana na Navy Roberts, ambaye sasa ana umri wa miaka minne. Lakini shinikizo la vyombo vya habari, lilimlazimisha Rais Biden hivi karibuni kumtambua mjukuu wake wa saba.

Hata kabla ya kutengana Bi Buhle kukamilishwa, Hunter aliingia katika uhusiano na mjane wa kaka yake, Hallie Biden. Ripoti za kutengana ziliibuka 2019, wiki moja baada ya babake kuzindua kampeni ya urais.

Wiki chache baadaye, Hunter alifunga ndoa na mtengenezaji filamu wa Afrika Kusini, Melissa Cohen. Wana mtoto mmoja wa kiume.

Akizungumza mwaka 2019 kuhusu mapambano yake dhidi ya uraibu, alisema: "Huwezi kuiondoa. Unajifunza jinsi ya kuishi nayo."

Katika kitabu chake, anaamini kuokoka kwake ni kutokana na upendo wa familia yake, akisimulia kisa cha baba yake kumkumbatia na kusema: "Sijui nifanye nini kingine. Ninaogopa sana. Niambie la kufanya."

Miaka ya hivi karibuni Hunter amegeukia uchoraji kama aina ya tiba, akiambia New York Times kwamba "huniweka mbali na watu na mahali ambapo sistahili kuwepo."

Rais Biden amemtetea mwanawe mara kadhaa, haswa wakati wa mjadala wa urais 2020. "Mwanangu - kama watu wengi - alikuwa na tatizo la dawa za kulevya. Amelirekebisha na kulifanyia kazi, na ninajivunia mwanangu."

Kuchanganya familia na biashara

Baada ya kuhitimu Yale, Hunter alifanya kazi MBNA America, kampuni ya benki yenye makao yake makuu Delaware na baadaye kununuliwa na Benki ya Amerika.

Uhusiano wa karibu wa Joe Biden na benki hiyo - mchangiaji mkuu katika kampeni zake za kisiasa - ulimletea sifa mbaya. Hunter alipopandishwa cheo hadi cheo cha makamu wa rais mtendaji, Joe alishawishi sheria ya mageuzi ya ufilisi iliyopendelea MBNA kupitia Seneti.

2006, wakati Seneta Biden alipopanga kuchukua tena uenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Seneti, Hunter na mwana ndugu mwingine walifanya ununuzi wa hasara wa kampuni ya hedge fund.

Mfuko huo uliunganishwa na wadanganyifu kadhaa, ikiwa ni pamoja na mfadhili wa Texas aliyepatikana na hatia ya kuendesha mojawapo ya miradi mikubwa ya Ponzi katika historia ya Marekani.

Familia ya Biden imekanusha makosa yoyote na hawakabiliwi na mashtaka yoyote.

China na Ukraine

Mengi yamefanywa katika miaka ya hivi karibuni kuhusu masilahi ya biashara ya Hunter wakati baba yake akiwa makamu wa rais. 2013, aliingia katika bodi ya kampuni ya BHR, kampuni binafsi ya Uchina – na baadaye kumiliki hisa 10% katika hazina hiyo.

Kampuni hiyo ilisajiliwa Shanghai chini ya wiki mbili baada ya Hunter kusafiri na baba yake katika safari rasmi ya makamu wa rais hadi Uchina na kukutana na mtendaji mkuu wa BHR.

Baada ya baba yake kuondoka ofisini mwaka 2017, Hunter alishirikiana na tajiri mkubwa wa mafuta wa China, Ye Jianming kwenye mradi wa gesi asilia huko Louisiana. Makubaliano hayo yaliporomoka baada ya Ye kuzuiliwa na mamlaka ya Uchina kwa tuhuma za ufisadi.

Mahusiano ya Hunter nchini Ukraine yamezua utata zaidi, ikizingatiwa kwamba babake alikuwa mtu wa serikali ya Obama. 2014, alijiunga na bodi ya kampuni ya nishati ya Ukraine, Burisma Holdings, ambapo alilipwa dola za Marekani 1.2 kwa mwaka.

Kama sehemu ya harakati ya kupambana na ufisadi, Makamu wa Rais Biden wakati huo alikuwa akiandamana kutaka mwendesha mashtaka mkuu wa nchi hiyo Viktor Shokin afutwe.

Shokin aliondolewa na bunge mwaka wa 2016, lakini wakosoaji wanasema kwamba mwendesha mashtaka alipoteza kazi yake kwa sababu alikuwa akimchunguza Burisma.

Warepublican wamedai Joe na Hunter Biden walipokea malipo ya milioni 5 dola za kimarekani kutoka kwa watendaji wa Burisma badala ya kufutwa kwa Shokin.

Kompyuta ndogo iliyoachwa na Hunter kwenye duka huko Delaware. Uchambuzi wa yaliyomo umetoa uthibitisho wa mapato makubwa ya Hunter kutokana na kazi yake nchini Uchina na Ukraine.

Rais Biden anapotaka kuchaguliwa tena, wanamkakati wake watakuwa na matumaini kwamba mchezo wa kisheria wa mwanawe hautoleta usumbufu kwake.