HFO: Mafuta hatari yanayoyeyusha barafu kwa kasi duniani

ds

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Meli nyingi za mafuta na gesi katika bahari ya Arctic hutumia mafuta ya HFO.
    • Author, Matt McGrath
    • Nafasi, BBC

Marufuku ya matumizi mafuta yanayoathiri mabadiliko ya tabia nchi, imeanza kutekelezwa katika bahari ya Aktiki. Mafuta haya hutumika na meli zinazopita katika maji haya.

Mafuta haya, yanayoitwa HFO, yanafanana na lami nzito. Ni nafuu sana ikilinganishwa na mafuta ya kawaida. Mafuta haya hutumiwa sana na vyombo vya usafiri ulimwenguni kote, haswa na meli za kubeba mafuta.

HFO inasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, haswa katika eneo la Aktiki. Theluji inayeyuka kwa kasi kutokana na kaboni nyeusi inayotolewa wakati mafuta haya yanapoendesha vyombo.

Marufuku hiyo imekaribishwa na wanaharakati wa mazingira, lakini wanasema kuanza kwake kutekelezwa hakutakuwa na athari chanya ya haraka.

Kwa sababu ya mianya katika utekelezaji wake, na idadi kubwa ya meli zinaweza kutumia mafuta haya hadi 2029.

Pia unaweza kusoma

Kwanini ni hatari?

DSX

Chanzo cha picha, Getty Images

HFO, yanazalishwa kutokana na mabaki ya mafuta katika viwanda vya kusafisha mafuta, yanaleta tishio kubwa kwa bahari, hasa eneo la Aktiki.

Mafuta haya mazito, yenye kuteleza, ni vigumu kuyasafisha ikiwa yataingia kwenye maji baridi.

Hayachangayiki yanapoingia kwenye maji baridi. Wataalamu wanasema huzama ndani ya maji kama yalivyo kwa pamoja na kuwa masimbi, na ni tishio kwa mazingira.

Wataalamu wanasema mafuta ya HFO ni hatari zaidi kwa angahewa. HFO yanapoungua, hutoa kiasi kikubwa cha gesi inayoleta joto duniani, gesi ya kaboni nyeusi.

"Kaboni nyeusi husababisha joto katika eneo la Aktiki. Hutoa joto kwenye angahewa na kisha hutua kwenye barafu, na kusababisha kuyeyuka haraka," anasema Dk Sian Prior, kutoka kikundi cha wanaharakati wa mazingira cha Clean Arctic Alliance.

Marufuku Yenyewe

DFC

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka 2011, matumizi na mafuta haya kwa usafirishaji yalipigwa marufuku katika bahari ya Antarctic.

Wanamazingira wamekuwa wakifanya kampeni kwa miaka, ili kupanua marufuku ya matumizi ya mafuta haya kwa bagari ya kaskazini.

Hatimaye, mwaka 2021, waliomba nchi wanachama wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Bahari (IMO), kutekeleza marufuku hiyo.

Kulingana na sheria zinazohusiana na marufuku hiyo, meli zilizo na matangi ya mafuta yaliyo na vibali maalumu, haziingii kwenye marufu. Maanake, mafuta hayo yanaweza kutumika katika meli hizo.

Pia marufuku hiyo haifanyi kazi kwa nchi zinazopakana na bahari ya Aktiki – yaani katika eneo lao la maji.

Urusi, moja ya nchi katika eneo hilo, inaendesha meli zaidi ya 800 katika maji ya kaskazini. Nchi hizo zitaendelea kutumia mafuta hayo hadi 2029.

Baraza la Kimataifa la Usafiri Safi, linakadiria karibu asilimia 74 ya meli zinazotumia HFO zitaweza kutumia mafuta haya hadi 2029.

Wachunguzi wengine wanasema, kuongezeka kwa safari za kuchimba mafuta huko Arctic hakutapunguza kiwango cha matumizi ya HFO katika bahari, lakini inaweza hata kuongeza.

"HFO yanatumika kwa kiwango kikubwa katika meli za mafuta na gesi. Hii ina maana kwamba kadiri matumizi ya meli za mafuta yanavyoongezeka, ndivyo matumizi ya HFO yanavyoongezeka," anasema Dk Elena Tracey wa WWF.

Wanaharakati wa mazingira wanasema nchi zenye kupakana na bahari ya Arctic na zinazotumia mafuta hayo, zinapaswa kuichukua marufuku hiyo kwa uzito.

Wanasema Norway inapaswa kuchukuliwa kama mfano kwa hili. Serikali ya Norway imetekeleza marufuku ya matumizi ya HFO karibu na visiwa vya Svalbard.

Hivi karibuni, meli ya Ireland iliyonaswa ikitumia HFO katika eneo hilo ilitozwa faini ya dola za kimarekani 93,000.

Wanaharakati wa mazingira wanataka hatua kama hiyo itekelezwe katika eneo la Aktiki pia.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla