Mzaha mzaha tu Mandonga anauheshimisha mchezo wa ngumi Afrika Mashariki
Na Yusuph Mazimu
BBC Swahili

Chanzo cha picha, Mandonga FB
Miaka miwili iliyopita ungemwambia Karim Mandonga ‘Mtu kazi’ bondia mwenye maneno na mbwembwe nyingi wa Tanzania kwamba, angekuwa kwenye ulingo katika nchi ya ughaibuni anapigana, asingekukubalia.
Sidhani kwamba pia angekukubalia kwamba leo hii angekuwa bondia anayetajwa zaidi Afrika Mashariki kuliko mabondia wengine wote.
Angekujibu kimzaa tu ‘ acha utani’, lakini ndoto hiyo isiyootwa leo anaiishi, tena anaiishi kwa viwango vya umaarufu mkubwa.
Sina shaka na kila mtu atakubaliana na mie, ukitaja bondia maarufu na mwenye mvuto kwa sasa Tanzania ni Mandonga. Na sasa amevuka mipaka amepeleka umaarufu wake nje ya mipaka. Mwishoni mwa wiki hii huko Kenya, alimchapa bingwa wa zamani wa taji la Afica Boxing Union (ABU), Daniel Wanyonyi kwa TKO (Technical Knock Out).
Pambano hilo lililofanyika katika ukumbi wa KICC Nairobi, lilikuwa la raundi 10, lilimalizika katika raundi ya 5, ambapo ilipoingia raundi ya 6 Wanyonyi hakurejea na muamuzi akaashiria ushindi kwa Mandonga.
Ushindi wake huo nje ya ardhi ya Tanzania sio tu umezidi kumpaisha na kumpa sifa zaidi Mandonga, bali umemjengea heshima yeye. Lakini muhimu zaidi ameanza kuwashitua watu na kujenga msingi wa heshima ya mchezo wa ngumi Afrika Mashariki.
Mandonga na ngumi ya ‘masoko’

Chanzo cha picha, MandongA fb
Mandonga ni zaidi ya bondia, anapigana ulingoni na anapigana ‘kimasoko’. Mdomo wake umekuwa sehemu kubwa ya silaha yake na umaarufu wake. Na ndivyo inavyopaswa kuwa kwenye ndondi.
Muhammad Ali, bondia bora wa wakati wote, alikuwa wa aina ya mandonga. Lakini yeye alikuwa anakupiga ulingoni na anakupiga kwa maneno. Mandonga angalau sasa anaanza kupiga kwa maneno na anakupiga ulingoni.
Huko nyuma alikuwa anaonekana mtu wa kuchapwa zaidi….na alichukuliwa hivyo kama mtu wa kupigwa
Haijalishi matokeo, ila mbwembwe zake tu, madoido, muonekano na maneno ni zaidi ya matangazo…. Hicho ndicho kinachofanya Mandonga kujitofautisha na mabondia wengine wa eneo hili la Afrika Mashafriki
Aliitwa Kenya kushiriki kwenye pambano la utangulizi kusapoti pambano kuu la siku hiyo kati ya Mkenya Rayton ‘Boom Boom’ Okwiri na Ally Shabani Ndaro pia wa Tanzania. Hata hivyo Mandonga alibadili upepo.

Chanzo cha picha, Mandonga FB
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alionekana mkubwa kuliko pambano lenyewe la Okwiri na Ndaro. Kabla hajafika Kenya, kila mtu Kenya alijua kuna mtu anaitwa Mandonga, alijua kuna pambano la ngumi linafanyika Nairobi.
Hata watu wasiofuatilia kabisa ngumi, walijua. Alikusanya kijiji, alijaza ukumbi wa KICC. Pengine hata wasanii wakubwa tunaowajua Afrika Mashariki wasingeweza kufanya hata nusu ya alichofanya Mandonga. Si kujaza ukumbi tu, wengine hata kujulikana tu kwamba wapo mahali fulani ni ngumu. Lakini Mandonga amefanikiwa.
Haishangazi sasa anatoka kuwa bondia wa mapambano ya utangulizi na kupewa nafasi ya kuwa bondia wa pambano kubwa la siku.
Wewe utaisikia akisema nmekuja na 'ngumi mpya Sugunyo kutoka Ukraine' au ngumi ya Peresu peresu' ama ndoige' . Lakini kwa jicho la masoko, hiyo ni ‘ngumi ya masoko’ ya Mandonga. Anajitangaza na anautangaza mchezo wa masumbwi.
Rais wa Kamisheni ya ngumi za kulipwa Kenya (KPBC), Reuben Ndolo amenukuliwa akisema ' tutamleta tena Mandonga Kenya, ni mtu mzuri wa kutangaza (masoko)'.
Alianza kwa mzaha mzaha tu leo Mandonga ni mtu mwingine
Ukitaja mabondia wakali na wenye rekodi za kufurahisha duniani, Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’ hawezi kuwemo hata kwa dawa. Ukitaja mabondia wakali wa kiwango cha kufikirisha Afrika Mashariki Mandonga hayumo. Na hata ukitaja mabondia wakali watano wa Tanzania kwa sasa, sina uhakika kama Mandonga atakuwa miongoni mwao.
Ni dhahiri Mandonga ni bondia wa kawaida, ukilinganisha na mabondia waliowahi kutamba ndani na nje ya Afrika Mashariki. Alianza tu kufahamika miaka miwili mitatu iliyopita lakini zaidi mwaka jana. Na umaarufu wake ulikuja kwa kupigwa katika moja ya mapambano yake baada ya kutamba sana kwa maneno.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 1
Ni mzaha mzaha tu, hata watanzania wengi hawafikirii Mandonga ni mtu wa kushinda mapambano zaidi ya kumuona ni mtu wa kuburudisha tu. Mtu wa maneno
Muhammad Ally alifanya hivyo, alitumia maneno lakini alikuchapa kweli kweli ulingoni. Tyson Fury, ambaye ni bondia namba moja kwa sasa wa uzito wa juu duniani anafanya hivyo, na hata Mike Tyson wakati huo alikuwa bondia ‘mtata’ aliufanya mchezo wa ngumi duniani kuwa wenye mvuto wakati wake kutokana na utata wake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini kupigwa ama kushinda hiyo siyo hoja, hoja ni namna anavyoyapa hadhi ya kufuatiliwa mapambano yake. Uwepo wake, maneno yake hayo hayo yanamtofautisha na mabondia wengi wakubwa wa Afrika Mashariki, waliokuwepo.
Hakuna asiyemjua Rashid Matumla wakati wake, akizichapa ndani na nje ya Tanzania. Michezo ya Olimpiki ya Atlanta ya mwaka 1996 ilimjenga sana akipoteza kwa ‘mbinde’ dhidi ya Phillip Boudreault, aliyeshinda kwa alama 16-12.
Karama Nyilawila (Captain), bingwa wa zamani wa mkanda wa dunia wa WBF, wadau wa ngumi wanamtaja kama moja ya mabondia bora kuwahi kutokea Tanzania, ambaye ni miongoni mwa mabingwa wachache kutwaa mikanda hiyo nje ya nchi.
Hassan Mwakinyo, bondia bora Afrika akiiwakilisha vyema Tanzania, Dullah Mbabe na Twaha Kassim Rubaha ni mabondia wakubwa zaidi ya Mandonga ni mabondia wazuri wa Tanzania.
Francis Cheka, Mbwana Matumla na Mada Maugo (King) walikuwa mabondia wakubwa wa Tanzania kama ilivyo kwa Nick Okoth, George Owano, Joshua Wasike na Elly Ajowi wanaoendela kutajwa kwenye ndondi za Kenya.
Usisahau Kenya pia alikuwepo bondia anayetajwa kuwa bora zaidi kwa uzito wake (welterweight ) Robert Napunyi Wangila aliyeshinda medali ya dhahabu katika mashindano ya olimpiki ya mwaka 1988.
Nchini Uganda walikuwepo kina Ayub Kalule, John Mugabi na Kassim Ouma na hata miaka ya hivi sasa kina Sharif Bogere, Brayan Mayanja na wengineo.
Lakini wote hawakuufanya mchezo wa ngumu kwa wakati wao na kwa muda mfupi kupata umaarufu Afrika Mashariki kwa kiwango cha sasa anachofanya Mandonga. Kinachombeba Mandonga ni mdomo wake.
‘ngumi ni ubabe, ngumi ni vitisho, maneno ya mandonga yameufanya mchezo kufuatiliwa sana’, alisema Kassim Janja, mmoja wa wadau wa masumbwi Tanzania.
‘Wanahitajika Mandonga 5 tu’

Chanzo cha picha, Kbc
Mandonga umri umemtupa. Umri wake wa zaidi ya miaka 40 kwa ndondi ni miaka ya lala salama. Jua limezama, lakini kwa muda mfupi huu ameutendea haki mchezo wa masumbwi hasa kwenye eneo la kuutangaza.
‘Tunahitaji Mandonga watano tu, kuufanya mchezo wa masumbwi kuwa mkubwa, kuwe na Mandonga wa Tanzania, Mandonga wa Kenya, Uganda sijui Rwanda, hii italeta hamasa na msisimko mkubwa ya mchezo huo‘.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 2
Hamasa ni hatua muhimu na ya kwanza katika mchezo wowote. Mandonga ameanza kujenga misingi, kinachofuata sasa ni kuongezeka Mandonga wengine na kuupa hadhi mchezo huo.
Hata muziki wa bongo flava ulianza kwa kujengewa misingi yake na wasanii kama Profesa Jay, Juma Nature, Inspector Haruni na wengine, lakini sasa kina Diamond Platnumz, Ally Kiba, Harmonize na wengine wanafurahia maisha.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 3
Tunamuona akitangaza matangazo mengi, akipigana karibu kila mwezi kwa burudani, hakuna mwenye uhakika kama umaarufu wake unaendana na kipato chake. Ukweli huenda Mandonga asinufaike sana kwa sasa, lakini mchezo wa masumbwi unaweza kunufaika zaidi na yeye na baadaye zaidi kunufaisha vizazi vijavyo.
Majukumu ya wadau wa masumbwi Afrika Mashariki kwa sasa wana kazi moja tu kubwa; Kutengeneza kina Mandonga wengine. Kama ni jambo rahisi kutokea, hakuna anayefahamu, lakini hilo ni muhimu kwa msingi wa ndondi za maana huko siku za usoni












