Madai ya mauaji kuhusu mahari yaliopelekea kulipa kisasi na kusababisha msiba mkubwa

Chanzo cha picha, Ankit Srinivas
Mkasa mbaya ambao umezikumba familia mbili, umeacha watu watatu wakiwa wamefariki huku wengine saba wakipelekwa jela .
Tukio la usiku wa tarehe 18 Machi katika mji wa kaskazini mwa India wa Prayagraj (zamani Allahabad) pia limezua mshtuko mkubwa miiongoni mwa wakazi wa vitongoji viwili vya watu wa tabaka la kati.
Onyo: Taarifa hii ina maelezo ambayo wengine wanaweza kuyaona ya kuhuzunisha.
"Ilikuwa takriban saa 11 jioni wakati watu 60-70 walifika nyumbani kwetu. Walianza kutupiga bila huruma," anasema Shivani Kesarwani.
Wavamizi hao, anasema, ni pamoja na wanafamilia na jamaa wa Anshika, mke wa kaka yake Anshu, ambaye alipatikana akining'inia nyumbani kwa Kesarwani saa moja kabla.
Shivani na polisi wanasema Anshika alikufa kwa kujitoa uhai - lakini familia yake na majirani wanadai kuwa aliuawa kwa ajili ya mahari.
Akina Kesarwani walikuwa na biashara ya familia ya kuuza mbao na waliishi katika familia ya pamoja.
Nyumba ya chini ilichukuliwa na duka na ghala na familia iliishi juu yake.
Kila ghorofa ilikuwa na chumba kimoja cha kulala - Anshu aliishi kwenye ghorofa ya juu na mkewe tangu ndoa yao mwaka mmoja uliopoita, wazazi wake waliishi kwenye ghorofa ya kwanza na dada yake Shivani alikuwa na ghorofa ya pili.
"Anshika alishuka kwa kawaida saa nane mchana kwa chakula cha jioni lakini siku hiyo, hakufika na tulifikiri lazima alikuwa amelala," Shivani aliambia BBC.
Wakati kaka yake alipotoka dukani saa 10 jioni, alisema, alienda kumwita mkewe.
"Wakati hodi na simu zake ziliposhindwa kujibiwa alivunja kioo kilichokuwa juu ya mlango ili kutoa kufuli. Alimkuta Anshika akiwa amekufa. Alipiga mayowe na sote tukaelekea huko."

Chanzo cha picha, Ankit Srinivas
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Anshu na mjomba wake waliripoti kifo hicho katika kituo cha polisi, chini ya nusu kilomita kutoka nyumbani kwao, na wazazi wa Anshika walijulishwa.
Chini ya saa moja baadaye, polisi wanasema, familia ya Anshika iliwasili pamoja na makumi ya jamaa na dakika chache baadaye, ghasia zinasemekana kuzuka kati ya familia hizo.
Katika simu yake ya mkononi, Shivani anatuonyesha video za wanaume wakipiga kelele, wakisambuiliana kwa fimbo. Polisi anasimama katikati, akijaribu - na kushindwa - kuleta utulivu.
Mara baada ya mwili wa Anshika kutolewa nje ya nyumba, polisi wanasema jamaa zake walichoma moto nyumba hiyo.
Mbao, zilizohifadhiwa katika ghorofa ya chini zilichomeka, na kumnasa Shivani, wazazi wake na shangazi ndani ya nyumba.
Shivani na shangazi yake walivunja dirisha la ghorofa ya pili na kutambaa hadi kutoka salama katika nyumba iliyopakana ambayo ni ya mjombake. Hatahivyo wazazi wake hawakubahatika.
Wakati wazima moto, ambao walichukua zaidi ya saa tatu kuzima moto huo, walipoingia ndani ya nyumba mwendo wa saa tatu asubuhi, walipata miili ya wanandoa hao wazee ikiwa imeteketea.
"Mama yangu alikutwa amekaa kwenye ngazi. Alibebwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwenye gunia," Shivani anasema, huku akifuta machozi yake.

Chanzo cha picha, Ankit Srinivas
Malalamiko ya Shivani kwa polisi yanawataja watu 12 wa familia ya Anshika na "watu 60-70 wasiojulikana".
Afisa wa polisi aliambia BBC kuwa watu saba, akiwemo babake Anshika , mjomba wake na wana wao wa kiume, wamekamatwa na wanaendelea kuzuiliwa jela.
Wanasema baba yake Anshika amewasilisha malalamiko yake akimtuhumu "Anshu, wazazi na dada zake" kwa kumnyanyasa bintiye kwasababu ya mahari na kumuua.
Shivani anakanusha shutuma dhidi ya familia yake, ingawa anakiri kuwa walipokea zawadi, likiwemo gari, kutoka kwa familia ya Anshika kwenye harusi hiyo. "Walimpa binti yao chochote walichotaka. Hatukuomba chochote," anasema.
Anshu hajarudi nyumbani tangu mke wake afariki. "Amejificha kwa sababu anaofia maisha yake iwapo jamaa wengi wa Anshika watatoka jela, ," anaongeza.
Kutoa na kukubali mahari - ni kinyume na sheria nchini India tangu 1961, lakini 90% ya ndoa za Wahindi bado zinahusisha mpango huo, kulingana na utafiti wa hivi karibuni.
Polisi hupokea maelfu ya malalamishi ya unyanyasaji kutoka kwa wake kila mwaka na data ya uhalifu inaonyesha maharusi 35,493 waliuawa nchini India kati ya 2017 na 2022 kwa kukosa kuleta mahari ya kutosha.
Lakini aina hii ya kisasi kinachodhaniwa kuwa cha kutisha katika kesi ya madai ya kifo cha mahari haijasikika.
Shivani, ambaye sasa anaishi na familia ya mjomba wake jirani, anatupeleka kwa matembezi katika eneo ambalo - hadi hivi majuzi - lilikuwa nyumbani kwake.
Mabaki ya mkasa huo wa usiku yametapakaa kila mahali. Kuta zimeingia masizi na sakafu imefunikwa na jivu nene, huku vitu vilivyochomeka vikitapakaa kila mahali
"Nataka haki, maisha yangu yameharibika, nyumba yangu na familia zimepotea. Nataka uchunguzi huru na wa haki na kila atakayepatikana na hatia aadhibiwe," anasema na kuongeza, "Kwa nini walichoma nyumba? Je! tutapata vipi ushahidi sasa?"

Chanzo cha picha, Ankit Srinivas
Pia ana hasira na polisi. "Kulikuwa na angalau polisi dazeni mbili nje ya nyumba yetu lakini hakuna aliyeingia kuwaokoa wazazi wangu. Walisimama tu na kutazama," anadai.
Polisi hatahivyo wanapinga vikali shtaka hilo. "Ilikuwa ni suala nyeti na hisia zilizidi kupanda. Tulilenga kuutoa mwili kutoka eneo la tukio na kuupeleka hospitali kwa uchunguzi. Lengo letu lilikuwa kupunguza umati wa watu na kutuliza hali," afisa mkuu wa polisi ambaye hakutaka kutajwa jina aliambia BBC.
"Hakuna mtu aliyetarajia nyumba ingechomwa moto. Haikutarajiwa kabisa," aliongeza. "Tuliita huduma ya zima moto mara moja. Pia tulisaidia kuokoa watu watano."
Msiba huo pia umeitia kovu familia ya Anshika. Ili kusikia upande wao , tunatembelea nyumba ya wazazi wake ambapo Anshika aliishi hadi harusi yake mwaka mmoja nyuma. Imefungwa kwa kufuli kubwa ya chuma kwenye lango kuu.
Umbali wa kilomita 2 tu kutoka nyumbani kwa Anshika ni nyumba ya mjomba wake. Yeye na wanawe ni miongoni mwa waliokamatwa. Familia hiyo hadi sasa imekataa kuzungumza na vyombo vya habari.
Tunapobisha hodi mlangoni anatoka Jawahar Lal Kesarwani, babu ya Anshika . Mmoja wa wajukuu zake analeta kiti cha plastiki na anakaa chini, akipumua kwa taabu.
"Nikuambie nini? Familia yangu yote iko jela, wanangu, wajukuu zangu," anasema baada ya dakika chache.
"Walimuua Anshika na kumnyonga ili ionekane kama mtu aliyejiua," anaongeza.
Harusi ya Anshika, Bw Kesarwani ananiambia, ilikuwa ndoa ya kifahari. "Tulitumia rupia milioni 5 ($60,000; £48,000). Tulimpa kila kitu ambacho nyumba yake inahitaji, na gari ambalo liligharimu rupia milioni 1.6."
Anaongeza kuwa Anshika alipowatembelea mwezi Februari mwaka jana, "alituambia kuwa ananyanyaswa. Tulimwambia aendelee, ajirekebishe, tukamwambia mambo yatakuwa vizuri", anasema huku akionyesha majuto kwa sauti yake.

Chanzo cha picha, Ankit Srinivas
Familia ya Kesarwani ni familia inayojulikana katika eneo lao, ambayo inaelezewa tofauti kuwa wanyenyekevu, wenye urafiki na wenye kusaidia, na maelezo ya msiba huo yamewaacha majirani zao katika mshtuko.
"Wao ni watu wazuri sana. Hatuwezi hata kuanza kufikiria jinsi hii inaweza kutokea. Sio watu wanaojiingiza katika ugomvi," alisema mwanamume anayeishi milango michache chini ya barabara yao.
"Hatujui ni nani aliyewasha moto huo, lakini mtu yeyote angekasirika kuona mwili wa binti yake," anaongeza.
Mwanamke katika mtaa huo anasema Anshika "alikuwa na tabia nzuri sana... msichana mrembo" na anaelezea familia yake kama "ya kawaida.. isiyoweza kutekeleza uhalifu wa kutisha wanaotuhumiwa kutekeleza".
"Inasikitisha kwamba wakwe zake walikufa kwa moto," anasema.
"Lakini kinachonisikitisha sana ni kwamba sasa hakuna anayezungumza kuhusu kilichompata Anshika. Alikufa vipi?"












