Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini kuhariri picha ili kubadilisha mwonekano wa uso kunasababisha sonona?
- Author, Yaye Awa Niang
- Nafasi, BBC Africa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Katika dunia ya mitandao ya kijamii, watu wengi wanapendeleaa kujipiga picha isiyo na dosari, jambo ambalo limekuwa uraibu mkubwa kwa mamilioni ya watu duniani.
Majukwaa haya, ambayo awali yalikusudiwa kuwa njia ya kuungana na wengine, sasa yamekuwa maeneo ambapo mwonekano na picha zinakuwa muhimu zaidi kuliko ukweli.
Wakati mwingine, picha za kujipiga uso, video, na picha zilizohaririwa zinabeba shinikizo la kutii viwango visivyo halisi vya urembo, jambo linaloathiri mtazamo wetu kuhusu sisi wenyewe.
Kundi linalohariri picha kwa kutumia vikorombezo vya mitandao ni kama zile zinazolainisha ngozi, kunenepesha kope, na kufanya sura ionekane nyembamba.
Hii ni changamoto kubwa, kwani ni vigumu kutofautisha ukweli na kile kinachoonyeshwa kwenye mitandao.
Katika muktadha huu, Faynaraa, msichana mwenye umri wa miaka 23 kutoka Senegal, anasema wazi kuhusu madhara ya mitandao ya kijamii, huku akihimiza watu kujiuliza kuhusu uhusiano wao na picha binafsi wanazozichapisha mitandaoni.
Ushawishi wa kuhariri picha kubadilisha muonekano wa mtu
Idadi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii inazidi kuongezeka.
Baada ya mwaka 2024, takribani watu bilioni 5 duniani, sawa na asilimia 62.3% ya idadi ya watu duniani, watakuwa wanatumia mitandao ya kijamii.
Jukwaa kama Facebook, Instagram, TikTok, na YouTube vimekuwa sehemu ambapo watu wanashiriki maisha yao, mara nyingi wakitumia vikorombezo na uhariri wa picha ili kuboresha mwonekano wao.
Faynaraa ni mmoja wa watu maarufu kwenye mitandao ya kijamii.
Alianza kutengeneza maudhui akiwa na umri wa miaka 18 na alijizolea umaarufu mkubwa, hasa TikTok, ambapo alikusanya zaidi ya wafuasi milioni moja kwa muda wa miezi sita.
Hata hivyo, nyuma ya tabasamu lake na video za ngoma, Faynaraa anaangalia kwa makini athari za ulimwengu huu wa kidijitali.
Mnamo mwaka 2023, aliamua kuvaa hijabu kama ishara ya kujitolea kwa uhalisia na kutaka kuwa na picha ya kweli ya maisha yake binafsi.
Anasema alijiona kana kwamba anabadilisha mtindo wa maisha yake kwa sababu ya shinikizo la jamii, lakini alijua kuwa hiyo siyo nafsi yake ya kweli. Alijua kuwa anahitaji kuwa na picha ya kweli, bila shinikizo la mitandao.Anasema Faynaara.
Kuwa wazi ukifanyiwa upasuaji wa maumbile: Wito wa kuwa mkweli
Katika dunia hii ya picha zinazohaririwa na vikorombezo za mitandaoni, Faynaraa anaamini kuwa ni muhimu kurudisha uwazi kuhusu mwonekano.
Anasema kuwa kila mtu anapaswa kuwa wazi kuhusu matumizi ya bidhaa au wamefanya upasuaji wanapobandika picha za mwili wao.
"Kama umefanyiwa upasuaji, ni muhimu kuelezea jamii yako," anasisitiza. Hii inamaanisha kuwa watu wanapaswa kusema ukweli kuhusu mwili wao badala ya kudanganya kwa kutumia picha za kuhaririwa au wakifanya upasuaji wa kutengeza umbile waeleze kuwa sio umbile waliozaliwa nalo.''anaendelea kuelezea
Faynaraa anasisitiza kuwa uhalisia ndio ufunguo wa uzuri wa kweli. Anataka kila mtu aelewe kwamba uzuri hautokani na picha za mitandao pekee, bali na jinsi unavyojiamini na kukubaliana na kasoro zako.
"Huwezi kuwa mkamilifu, na ni kasoro zako zinazounda uzuri wako," anasema.
Katika jamii ya sasa, mitandao ya kijamii imetengeneza shinikizo kubwa kwa vijana, ambao mara nyingi wanakutana na picha za urembo ambazo siyo za kweli.
Vikorombezo vya mitandao vinavyotumika kubadilisha sura na mwili vimekuwa vichocheo vya kutaka kufanana na kile kinachoonyeshwa kwenye mitandao, jambo ambalo linaweza kuathiri hali ya kiakili na kujithamini kwa mtu.
Utumizi wa kuhariri picha kubadilisha maumbile : unageuza uhalisia
Kuhariri picha imekuwa kigezo muhimu vya kupiga picha za mitandaoni.
Mchakato huu ambao unakumbatiwa na wengi una madhara chungu nzima.
Mountaga Cissé, mchanganuzi wa masuala ya kijamii anasema: ''Kuhariri picha kubadilisha muonekano huleta picha tofauti na kutokuwa na uhalisia.Inakulazimu kujiweka au kuonekana kama mtu tofauti na uhalisia wako''
Pengo hili kati ya picha na ukweli wa mambo huleta shinikizo hasa miongoni mwa vijana ambao wanajipata wakishurutika kuwa na urembo kama huo japokuwa sio uhalisia.
Unapoingia mtandaoni hasa Tiktok utakutana na baadhi ya watu wanaouza bidhaa wakiaminisha zinabadilisha maumbile yawe ya kuvutia na baadhi ya vijana wanapojiangalia wanahisi hawana mvuto.
Unaanza kutokujiamini na kuanza kutafuta suluhu ya kubadilisha muonekano wako,''anasema Mame Fatou Samba mwanamke mwenye umri wa miaka 25.
Lakini Khady Dioup, mwenye umri wa miaka 26 anaonyesha ukakamavu alionao haswa kujiamini akisema sio rahisi kushawishika nakujibadilisha nilivyo.''
Na kinachozidisha tabia hii ya kuhariri picha ni ukosoaji unaolimbikiziwa watengeneza maudhui .
''Vijana wengi wanakumbana na picha zilizohaririwa ambazo hazina uhalisia ''anasema Ibraheem, kijana mwenye umri wa miaka 26 ambaye ni muigizaji nchini Senegal.Majibu yasioridhisha ,kubeza na kubagua huathiri utu wa mtu.
''Iwapo unajua kujiamini kwako kutatingishwa , usijiweke mitandaoni,'' anasahauri François Ndiaye, mtumiaji wa mtandao ambaye anaonya madhara ya kisaikolojia unayoyapata ukiwa mitandaoni.
Ari ya kuwa maarufu mitandaoni: Chambo hatari!
Mitandao ya kijamii pia imechochea kuibuka kwa umaarufu wa kidijitali.
Vijana, hasa,wanatamani kutambuliwa kwenye ulimwengu huu wa mtandao, wakitafuta wafuasi mitandaoni.
Inawalazimu wengi kuhariri picha ili wabadilishe mwonekano wao wakiamini wafuasi wao watavutiwa zaidi.
Uzuri wa Uhalisia: Wito wa kujiamini
Ari hii ya kuwa maarufu mitandaoni husababisha madhara ya afya ya akili anaonya mchanganuzi wa masuala ya umma Djiby Diakhate.
''Kuna wakati ukifika mtengezaji maudhui anachoka kujieleza kama mtu fulani na kurejea kwa uhalisia wake'' anasema mtalaam.
Hali hi huleta siutafahamu miongoni mwa wafuasi wake na kutoaminiana pindi mtengezaji maudhui anarejelea uhalisia wake .Wengi wanakosa kujitambua wao ni nani na inakuwa vigumu kutofautisha maisha yao halisi na maisha wanayoyatangaza mitandaoni.
Faynaraa anawashauri watumizi wa mitandao ya kijamii kukubaliana na nafsi zao na kuepuka kuishi kulingana na viwango visivyoweza kufikiwa vinavyowekwa na mitandao. Kwa kumalizia, anatoa wito kwa watu kuwa wa kweli na kukubali udhaifu wao kama sehemu ya uzuri wao wa kipekee.
Mitandao ya kijamii: Ushawishi wa kimataifa, lakini kwa gharama gani?
Mitandao ya kijamii ina athari kubwa kwenye jamii, na inazidi kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.
Hata hivyo, ni muhimu kutafakari athari za matumizi ya mitandao hii, hasa kuhusu picha, afya ya akili, na uhusiano wa kijamii.
Teknolojia hiyo inaweza kuhatarisha mahusiano ya watu na kusababisha sonona.
Harakati ya kutafuta ukamilifu kupitia picha za mitandao ni changamoto kubwa, lakini kwa uaminifu na kukubaliana na nafsi zetu, tunaweza kupata uhuru wa kweli.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid