Fahamu kwanini madaktari wa kike wa Pakistan wanahofia usalama wao

Mauaji ya daktari mmoja nchini India yameibua maswali kuhusu usalama wa wataalamu wa afya wa kike katika nchi nyingine ikiwemo Pakistan

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mauaji ya daktari mmoja nchini India yameibua maswali kuhusu usalama wa wataalamu wa afya wa kike katika nchi nyingine ikiwemo Pakistan
    • Author, Farhat Javed
    • Nafasi, BBC Urdu
    • Akiripoti kutoka, Pakistan
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Wanawake wanaofanya kazi katika hospitali nchini Pakistan wanasema mara kwa mara wanakabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia na matusi kutoka kwa wenzao wa kiume, wagonjwa na familia zao.

Kufuatia tukio la daktari mwanafunzi mwenye umri wa miaka 31 kubakwa na kuuawa akiwa kazini katika hospitali ya India, zaidi ya makumi ya madaktari wa kike nchini Pakistani waliiambia BBC kuwa wanahofia kuhusu usalama wao wenyewe.

Lakini huu ni mzozo unaoendelea kisiri, kwani wengi wanaogopa kujitokeza kuripoti uhalifu huo - wakati wale wanaodhulumiwa mara nyingi huambiwa hakuna mtu atakayeamini madai yao.

Wanawake wengi ambao BBC ilizungumza nao waliombamajina yao yasitajwe kwa hofu ya kupoteza kazi zao.

Miezi michache iliyopita, daktari mdogo alimjia Dk Nusrat (si jina lake halisi) huku akilia. Daktari wa kiume alimpiga picha mwanamke huyo akiwa chooni na kuanza kuitumia video hiyo kumlaghai.

"Nilipendekeza kuwasilisha malalamiko kwa FIA [Shirika la Upelelezi, ambalo linashughulikia uhalifu wa mtandaoni], lakini alikataa. Alisema hataki ivujishwe na ifikie familia yake au wakwe zake,” Dk Nusrat alieleza, akiongeza kuwa anajua visa kadhaa vya madaktari wa kike kurekodiwa kisiri wakiwa katika mazingira ya kutatanisha.

Dk Nusrat alitokea kumfahamu mtu mmoja mkubwa katika idara ya polisi ambaye alizungumza na msaliti huyo, na kuonya kwamba anaweza kukamatwa kwa kile alichokifanya. Afisa wa polisi alihakikisha kuwa video hiyo imefutwa.

"Kwa bahati mbaya, hatukuweza kuchukua hatua zaidi, lakini tulifunikiwa kukomesha uovu huo na hakuna mtu anayeweza kuifanya tena," anasema Dk Nusrat.

Wanawake wengine wasimulia jinsiwalivyonyanyaswa kingono, akiwemo Dk Aamna (si jina lake halisi), ambaye alikuwa afisa wa matibabu katika hospitali ya serikali miaka mitano iliyopita alipolengwa na daktari wake mkuu, mtu mwenye ushawishi mkubwa.

Wanawake wanaogopa kuzungumzia hadharani unyanyasaji dhidi yao kwa kuhofia hatua hiyo itaathiri taaluma na maisha yao ya kibinafsi.
Maelezo ya picha, Wanawake wanaogopa kuzungumzia hadharani unyanyasaji dhidi yao kwa kuhofia hatua hiyo itaathiri taaluma na maisha yao ya kibinafsi.

“Aliponiona nikiwa na faili mkononi, alijaribu kuegemea juu yake, akitumia lugha isiyofaa, na kujaribu kunigusa,” alisema.

Aliwasilisha malalamiko kwa uongozi wa hospitali, lakini anasema suala hilo lilipuuzwa. “Niliambiwa nimehudumu hapo kwa muda mfupi, na kuulizwa nina uthibitisho gani wa unyanyasaji huo. Walisema, 'Hatujafanikiwa kumrekebisha mtu huyo kwa miaka saba - hakuna kitakachobadilika, na hakuna mtu atakayekuamini'.

Dk Aamna anasema anawafahamu wanawake wengine ambao wamerekodi video za unyanyasaji, "lakini hakuna hatua inayochukuliwa - mnyanyasaji anahamishiwa kwenye kata nyingine kwa miezi michache, kisha anarudi tena".

IAlilazimika aendelee kufanya kazi katika mazingira hayo ili ahitimu kuwa daktari, lakini aliondoka mara tu ilipokamilisha mpango huo.

Ushuhuda uliokusanywa na BBC unaonyesha kuwa hadithi yake ni jambo la kawaida.

Dk Summaya Tariq Syed
Maelezo ya picha, Dk Summaya Tariq Syed, anataka watu wanaotuhumiwa kwa unyanyasaji wachukuliwe hatua
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tatizo hili linatokana na ukosefu wa uaminifu na uwajibikaji, kulingana na Dk Summaya Tariq Syed, daktari mkuu wa upasuaji wa polisi huko Karachi na mkuu wa kituo cha kwanza cha mgogoro wa ubakaji nchini Pakistan.

Anaelezea kuwa katika miaka yake 25 ya utumishi amekabiliana na visa vya mara kwa mara vya unyanyasaji, na kuongeza kwamba amekatishwa tamaa na jinsi masuala hayo yanavyoshughulikiwa.

Anasimulia jinsi, miaka michache iliyopita alipokuwa katika jukumu tofauti, alifungiwa chumbani na wenzake waliomtaka abadilishe kile alichoandika kwenye ripoti ya uchunguzi wa maiti kuhusu mtu aliyeuawa.

“Walisema, ‘Weka saini la sivyo hujui tutakufanyia nini',” lakini alikataa. Kutokana na cheo cha juu cha mmoja wa watu waliohusika, anasema, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao.

Daktari mwingine wa kike katika hospitali ya serikali huko Punjab anaeleza kuwa ni vigumu kwa wanawake kuripoti visa vya unyanyasaji.

“Kamati za usimamizi [za hospitali] mara nyingi hujumuisha madaktari wale wale wanaotunyanyasa, au wandani wao. Kwa hivyo kuna haja gani ya kuwasilisha malalamiko yatakayofanya maisha yako kuwa magumu zaidi?”

Hakuna takwimu rasmi kuhusu mashambulio dhidi ya wafanyikazi wa afya wa kike nchini Pakistan. Lakini, ripoti ya Taasisi za Kitaifa za Afya za Marekani mnamo 2022 ilitoa picha ya kutatanisha.

Inaonyesha kuwa hadi 95% ya wauguzi nchini Pakistan wamekabiliwa na unyanyasaji katika mazingira ya kazi walau mara moja wakitekeleza majukumu yao. Hii ni pamoja na kushambuliwa, kutishiwa, kutukanwa na kunyanyaswa kisaikolojia, na wafanyakazi wenzako, wagonjwa na wageni wa hospitali.

Takwimu hiyo inalingana na ripoti ya Jarida la matibabu la Pakistan, ambayo inanukuu utafiti wa 2016 wa hospitali za sekta ya umma mjini Lahore ambayo ilipendekeza 27% ya wauguzi walikumbwa na unyanyasaji wa kijinsia.

Pia inanukuu utafiti kutoka mkoa wa kaskazini-magharibi wa Khyber Pakhtunkha nchini Pakistan ambao ulionyesha kuwa 69% ya wauguzi na 52% ya madaktari wa kike walikabiliwa na fulani ya unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa wafanyikazi wengine.

Soma pia:
Kando na unyanyasaji, madaktari wa kike walizungumzia ukosefu wa vifaa vya msingi, kama vile vyoo katika kila mtaa na mahali pa kupumzika wakiwa zamu.
Maelezo ya picha, Kando na unyanyasaji, madaktari wa kike walizungumzia ukosefu wa vifaa vya msingi, kama vile vyoo katika kila mtaa na mahali pa kupumzika wakiwa zamu.

Dk Syed anasimulia shambulio la kutatanisha lililotokea Karachi mwaka wa 2010: "Daktari katika hospitali ya serikali alimvuta muuguzi kwenye chumba chake, ambapo kulikuwa na madaktari wengine wawili."

Muuguzi huyo alibakwa na kufadhaika sana hivi kwamba aliruka kutoka kwenye paa ambapo alianguka na kupoteza fahamu kwa muda wa wiki moja. "Hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi ya wanyanyasaji wake ingawa aliamua kutoendelea na kesi hiyo.”

Dk Syed anaamini kwamba jamii mara nyingi huwalaumu waathiriwa na kama muuguzi angeripoti hilo "lawama ingemwangukia".

Pia kuna unyanyasaji na vitisho kutoka kwa wagonjwa, marafiki na familia, anasema, akielezea jinsi wananchi walivyoshambulia maafisa wake walipokuwa wakishughulikia miili katika chumba cha kuhifadhia maiti mwaka jana.

Wafanyakazi wa afya wanawake wanataka usalama kuimarisha katika majengo ya hospitali
Maelezo ya picha, Wafanyakazi wa afya wanawake wanataka usalama kuimarisha katika majengo ya hospitali

Muuguzi Elizabeth Thomas (sio jina lake halisi) anasema matukio ambapo wagonjwa walevi hujaribu kuwagusa ni ya kawaida. "Tunaogopa, hatuna uhakika kama tutamhudumia mwanamume huyo au kujilinda. Tunajihisi wanyonge kabisa. Na hakuna wafanyakazi wa usalama wa kutusaidia.”

Dk Saadia anasema hata hawajui "kama mtu anayefagia au kuzungukaka hospitalini akidai kuwa mfanyakazi ni mfanyakazi halisi".

Kulingana na Utafiti wa Uchumi wa Pakistani 2023, kuna hospitali za serikali 1,284 nchini. Madaktari wanasema hatua za usalama haijaimarishwa.

Wahudumu wa afya wanasema vituo vya afya havina kamera za CCTV au vile vilivyo navyo ni chache sana na zile zilizopo pia hazifanyi kazi ipasavyo. Wanasema maelfu ya wagonjwa na familia zao hutembelea hospitali hizi kila siku, na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa matibabu yamekuwa ya kawaida.

Dk Saadia anasimulia jinsi alilazimika kujificha baada ya jamaa wa mgonjwa kumshambulia kwa kusubiri majibu ya vipimo yafike kabla ya kumchoma sindano.

“Alianza kunifokea. Nilibanwa mlangoni. Alinitishia, akisema, ‘Nichome sindano haraka, la sivyo nitakuua’.

Baadhi ya wauguzi wa Pakistan wanatoka kwa jamii ndogo zisizo za Kiislamu, hali ambayo inaweza kuwafanya kuwa hatarini wakati mwingine, anasema Elizabeth Thomas.

"Ninajua wauguzi wengi wanaonyanyaswa, na ikiwa hawatatii, wanatishiwa kwa tuhuma za kufuru. Ikiwa muuguzi anavutia, mara nyingi huambiwa abadili dini yao.

"Siku zote tunajiuliza jinsi ya kujibu kwa sababu tusipofanya wanachotaka, tunaweza kutushtaki kwa kufuru. Wauguzi kadhaa wamejipata katika hali hiyo."

Kutokana na unyanyasaji huo, madaktari wa kike wanafanya kazi katika mazingira ya hofu.

Wanafunzi wa matibabu, madaktari na wananchi wamefanya maandamano, wakitaka haki itendeke kwa daktari mwanafunzi aliyeuawa nchini India mwezi Agosti.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wanafunzi wa matibabu, madaktari na wananchi wamefanya maandamano, wakitaka haki itendeke kwa daktari mwanafunzi aliyeuawa nchini India mwezi Agosti.

Juhudi za BBC za kupata kauli ya mawaziri wa afya wa eneo hilo katika majimbo manne ambayo wanawake hao wamefanya kazi, pamoja na mratibu wa afya wa kitaifa huko Islamabad hazikufanikiwa.

Tangu kubakwa na kuuawa kwa daktari anayefunzwa nchini India, mijadala imezidi kati ya madaktari wa kike nchini Pakistani kuhusu jinsi ya kuhakikisha usalama wao wenyewe.

Dk Saadia anasema imemuathiri sana na amebadilisha utaratibu wake: “Sitembei tena gizani au bila watu. Nilikuwa nikipanda ngazi, lakini sasa ninahisi salama kutumia lifti.”

Na Elizabeth Thomas anasema imemtikisa pia. “Nina binti mwenye umri wa miaka saba, na mara nyingi anasema anataka kuwa daktari. Lakini huwa najiuliza, je daktari yuko salama katika nchi hii?”

Pia uanaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah