Tunachojua kuhusu milipuko ya simu za upepo za Hezbollah

Chanzo cha picha, Getty Images
Takribani watu 26 wakiwemo watoto wawili waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa, wengi wao wakiwa vibaya, baada ya vifaa vya mawasiliano, vingine vinavyotumiwa na kundi lenye silaha la Hezbollah, kulipuka kwa kiasi kikubwa kote nchini Lebanon siku ya Jumanne na Jumatano.
Katika tukio la milipuko, iliwaua watu 14 na kujeruhi takribani watu 450, kulingana na wizara ya afya ya Lebanon.
Milipuko hiyo ilitokea karibu na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya mazishi ya wahanga wanne wa milipuko hiyo ya Jumanne.
Timu za BBC katika jiji hilo ziliripoti matukio ya fujo ambapo ambulensi zilitatizika kuwafikia waliojeruhiwa, na wenyeji walitilia shaka mtu yeyote anayetumia simu.
Milipuko hiyo ilizidisha hali ya wasiwasi katika jamii ya Lebanon, ikitokea siku moja baada ya shambulio kama hilo, na la hali ya juu sana likilenga paja zinazotumiwa na wanachama wa Hezbollah.
Kundi hilo la wapiganaji lilimlaumu adui yake Israel. Maafisa wa Israel hadi sasa wamekataa kutoa maoni yao.
Makampuni mawili yaliyoko Taiwan na Hungary yanayoshutumiwa katika ripoti za vyombo vya habari kwa kutengeneza vifaa hivyo na nchi zote hizo zimekana kuhusika.
Hapa ndio tunayojua hadi sasa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Duru ya kwanza ya milipuko ilianza katika mji mkuu wa Lebanon Beirut na maeneo mengine kadhaa ya nchi mnamo 15:45 saa za ndani (13:45 BST) siku ya Jumanne.
Mashuhuda waliripoti kuona moshi ukitoka kwenye mifuko ya watu, kabla ya kuona milipuko midogo iliyosikika kama fataki na milio ya risasi.
Likinukuu maofisa wa Marekani, gazeti la New York Times lilisema kwamba vifaa hivyo vilipokea ujumbe ambao ulionekana kuwa unatoka kwa uongozi wa Hezbollah kabla ya kulipua. Ujumbe huo badala yake ulionekana kuwasha vifaa, chombo kiliripoti.
Milipuko iliendelea kwa takribani saa moja baada ya milipuko ya awali, shirika la habari la Reuters liliripoti.
Muda mfupi baadaye, watu wengi walianza kuwasili katika hospitali kote Lebanon, na mashuhuda wakiripoti mkanganyiko mkubwa katika idara za dharura.
Matukio kama haya yalijitokeza kote nchini katika awamu nyingine ya milipuko Jumatano, karibu 17:00 saa za ndani (15:00 BST).
Ripoti zinaonesha kuwa ni simu za upepo ambazo zililipuliwa, vifaa ambavyo vilinunuliwa na Hezbollah miezi mitano iliyopita, kwa mujibu wa chanzo cha usalama kikizungumza na Reuters.
Takribani mlipuko mmoja ulikuwa karibu na mazishi yaliyokuwa yakifanywa huko Beirut kwa baadhi ya waathiriwa wa shambulio la Jumanne, na kusababisha hofu miongoni mwa wale waliokuwa karibu na maandamano.
Watu tisa wameuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa, kulingana na wizara ya afya ya Lebanon.
Tunajua nini kuhusu vifaa hivyo vya mawasiliano?
Maelezo kuhusu simu za upepo zilizolipuka Jumatano bado yanatolewa.
Picha zilizopigwa baadaye zilionesha vifaa vilivyoharibiwa vilivyo na chapa ya Icom, kampuni ya Kijapani. BBC iliwasiliana na Icom Japan kupitia fomu ya mawasiliano kwenye tovuti yao lakini haijapata jibu.
Vifaa vilivyolipuka siku ya Jumanne vilikuwa chapa mpya ambayo kundi hilo halikuwa limetumia hapo awali, mhudumu mmoja wa Hezbollah aliliambia shirika la habari la AP.
Afisa mmoja wa usalama wa Lebanon aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba takribani vifaa 5,000 vilipelekwa nchini humo takribani miezi mitano iliyopita.
Lebo zinazoonekana kwenye vipande vya kurasa zilizolipuka huelekeza kwenye muundo wa paja unaoitwa Rugged Pager AR-924.
Lakini mtengenezaji wake wa Taiwan Gold Apollo amekanusha kuhusika na milipuko hiyo. Wakati BBC ilipotembelea Gold Apollo siku ya Jumatano polisi wa eneo hilo walikuwa wakivamia ofisi za kampuni hiyo, wakikagua nyaraka na kuwahoji wafanyakazi.
Mwanzilishi huyo, Hsu Ching-Kuang, alisema kampuni yake ilitia saini makubaliano na kampuni yenye makao yake makuu nchini Hungary - BAC - kutengeneza vifaa hivyo na kutumia jina la kampuni yake. Aliongeza kuwa uhamishaji wa pesa kutoka kwao umekuwa "ajabu sana", bila kufafanua.
BBC Verify imefikia rekodi za kampuni za BAC, ambazo zinaonesha kuwa ilijumuishwa kwa mara ya kwanza mnamo 2022.
Mkurugenzi Mtendaji wake Cristiana Bársony-Arcidiacono aliiambia NBC kwamba hajui lolote kuhusu milipuko hiyo. "Sitengenezi vifaa hivyo. Mimi ni wa kati tu. Nadhani ulikosea," alisema.
Serikali ya Hungaria ilisema kuwa kampuni hiyo "haina eneo la utengenezaji wala kazi" nchini humo.
Ni nini kilichochochea shambulio la vifaa vya mawasiliano?
Maafisa wa Marekani na Israel ambao hawakutajwa majina waliiambia Axios kwamba kulipua vifaa hivyo kulipangwa kama hatua ya ufunguzi katika mashambulizi dhidi ya Hezbollah. Lakini katika siku za hivi karibuni Israel iliingiwa na wasiwasi kwamba Hezbollah walikuwa wamefahamu mpango huo, hivyo tukio hilo lilifanyika mapema.
Maafisa wa Israel hawajazungumzia madai hayo, lakini wachambuzi wengi wanakubali kwamba inaonekana kuna uwezekano kuwa ndio waliohusika na shambulio hilo.
Prof Simon Mabon, mwenyekiti wa Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Lancaster, aliiambia BBC: "Tunafahamu kuwa Israel ina historia ya kutumia teknolojia kufuatilia malengo yake", lakini alisema ukubwa wa shambulio hili "haujawahi kutokea".
Lina Khatib, kutoka Chatham House yenye makao yake nchini Uingereza, alisema shambulio hilo liliashiria kuwa Israel "imejipenyeza" kwenye "mtandao wa mawasiliano" wa Hezbollah.
Katika taarifa yake inayoishutumu Israel kwa kuhusika na mashambulizi hayo, Hezbollah ilisema nchi hiyo "inawajibika kwa uvamizi huu wa uhalifu ambao pia ulilenga raia".
Kwa nini Hezbollah inatumia vifaa hivi?
Hezbollah inategemea sana vifaa hivi kama njia ya teknolojia ya chini ya mawasiliano ili kujaribu kukwepa kufuatiliwa na Israel. Vifaa hivi vya mawasiliano ya simu ni vifaa visivyotumia waya ambavyo hupokea na kuonesha ujumbe wa alphanumeric au sauti.
Ni ngumu zaidi kuzifuatilia kuliko simu za mkononi, ambazo zimeonekana kwa muda mrefu kama hatari sana, kama mauaji ya Israel dhidi ya mtengenezaji wa bomu Hamas Yahya Ayyash yalidhihirisha muda mrefu uliopita kama 1996, wakati simu yake ilipolipuka mkononi mwake.
Mwezi Februari, Hassan Nasrallah aliwaagiza wapiganaji wa Hezbollah kuondoa simu zao, akisema walikuwa wameingiliwa na ujasusi wa Israel. Aliwaambia wanajeshi wake kuvunja, kuzika au kufunga simu zao kwenye sanduku la chuma.
Wataalamu sasa wanasema agizo hilo, lililotolewa wakati wa hotuba ya moja kwa moja ya televisheni, huenda liliwaonya maafisa wa ujasusi wa Israel kwamba kundi hilo lingetafuta njia mpya ya mawasiliano ambayo inaweza kuwa ya chini zaidi.
Kinachofahamika kuhusu waathiriwa wa shambulio la Jumanne
Chanzo kilicho karibu na Hezbollah kiliiambia AFP kwamba wawili kati ya waliouawa katika shambulizi la Jumanne walikuwa wana wa wabunge wawili wa Hezbollah. Pia walisema binti wa mwanachama wa Hezbollah aliuawa.
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni balozi wa Iran nchini Lebanon, Mojtaba Amani. Ripoti katika vyombo vya habari vya Iran zilisema majeraha yake yalikuwa madogo.
Mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah hakujeruhiwa katika milipuko hiyo, shirika la habari la Reuters liliripoti likinukuu chanzo.
Waziri wa Afya ya Umma wa Lebanon Firass Abiad alisema uharibifu wa mikono na uso ndio unaochangia majeruhi wengi.
Waathiriwa waliowfikishwa kwenye vyumba vya dharura walikuwa wa umri tofauti, kutoka kwa wazee hadi vijana sana, wengine wakiwa wamevaa nguo za kiraia, alikiambia kipindi cha Newshour cha BBC.
Nje ya Lebanon, watu 14 walijeruhiwa katika milipuko kama hiyo katika nchi jirani ya Syria, kulingana na wanaharakati wa haki za binadamu chenye makao yake nchini Uingereza cha Syrian Observatory for Human Rights.
Je, mzozo wa Hezbollah na Israel utaongezeka?
Hezbollah inashirikiana na adui mkubwa wa Israel katika eneo hilo, Iran. Kundi hilo ni sehemu ya Mhimili wa Upinzani wa Tehran na limekuwa likipigana chini chini na Israel kwa miezi kadhaa, mara kwa mara wakijibizana na maroketi na makombora katika mpaka wa kaskazini wa Israel. Jamii nzima imehamishwa kutoka pande zote mbili.
Milipuko hiyo imekuja saa chache baada ya baraza la mawaziri la usalama la Israel kuwarejesha salama wakazi kaskazini mwa nchi hiyo kuwa lengo rasmi la vita.
Wakati akitembelea kambi ya jeshi la anga ya Israel siku ya Jumatano, Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant alisema nchi hiyo "inafungua awamu mpya katika vita.
Licha ya mvutano huo unaoendelea, wachunguzi wa mambo wanasema hadi sasa pande zote mbili zimelenga kuzuia uhasama bila kuvuka mipaka na kuingia katika vita kamili. Lakini kuna hofu kwamba hali inaweza kushindwa kudhibitiwa.
End of Unaweza pia kusoma
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Yusuf Jumah












