Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zawadi za mashada ya maua ya pesa taslim zinazungumziwaje?
Kwa muda mrefu wakazi wengi wa jiji la Nairobi wamekuwa wakichangamkia zawadi za rangi nyekundu kila tarehe 14 Februari.
Siku ya Wapendanao, watu huvaa nguo nyekundu, rangi inayoashiria mapenzi, au maua ya waridi.
Wafanyabiashara hujipatia pesa haraka, wakiuza maua ambayo ndio tu yametoka mashambani, hasa ukizingatia kuwa Kenya ni mojawapo ya wazalishaji wakuu wa maua duniani.
Katika siku za hivi karibuni badala ya mapetali ya rangi nyekundu laini, baadhi ya watu wamekuwa wakitengeneza mapetali ya noti mbali mbali zilizokunjwa au kufungwa pamoja katika shada la maua.
Mtindo huu umeenea katika nchi zingine za Afrika lakini umeshuhudiwa sana kiasi kwamba umetia wasiwasi benki kuu nchini Kenya, Uganda, Rwanda, Botswana na Namibia.
Nchi zote hizo zimetoa onyo kwa umma dhidi ya kuharibu noti wanapotengeneza mashada yam aua ya pesa taslimu.
Benki Kuu ya Kenya (CBK) inasema kwamba katika visa vingi, noti "hubandikwa, hugusishwa kwenye utepe, pini, sindano na kila aina ya ubunifu".
Noti zilizoharibika zinaweza kukataliwa na mashine za kutoa pesa kiotomatiki (ATM) na vifaa vya kuhesabu pesa, ikimaanisha kuwa lazima ziondolewe kwenye mzunguko, kwa gharama kwa mlipakodi.
Katika notisi yake, CBK ilisema haipingi matumizi ya zawadi za pesa taslimu - isipokuwa vitendo vinavyoharibu noti - kosa ambalo linaweza kusababisha watengenezaji wa mashada ya pesa kufungwa jela hadi miaka saba.
Maua ya pesa taslimu yamependwa na watu mashuhuri na wenye ushawishi mtandaoni, ambao mara nyingi hushirikisha video zao wakitoa zawadi kama hizo.
Sherehe hizo haziishii tu Siku ya Wapendanao - zinaenea hadi siku za kuzaliwa na zingine maalum, ikimaanisha kuwa shada la pesa linahitajika mwaka mzima.
Mashada ya maua huja katika miundo mbalimbali, huku wabunifu wakipanga noti ili ziendane na bajeti ya kila mteja.
Pesa taslimu zinazotumika katika mashada kama hayo hutofautiana sana – kwa jumla, zinaweza kuwa shilingi 1,000 ($8; £6) au hadi shilingi milioni moja, anasema Angela Muthoni, mfanyabiashara wa maua katika duka la Gift and Flowers katikati mwa Nairobi.
Ingawa mashada mengi yametengenezwa kwa miundo ya maua, au mchanganyiko wa maua na pesa pamoja na vitu vingine vya kifahari, zinaweza pia kuwa sehemu ya miundo ya keki au kutolewa kama zawadi.
Muthoni anasema mashada ya pesa yamekuwa maarufu katika miaka miwili iliyopita. Katika kuelekea Siku ya Wapendanao, amekuwa akipokea oda za kati ya mashada 15 na 20 kila siku, licha ya onyo la CBK.
"Kila mtu anapenda pesa," anaambia BBC, akiongeza kuwa kuwapa watu zawadi ya pesa taslimu huondoa msongo wa mawazo wa kuchagua zawadi.
Hata hivyo, baadhi ya Wakenya wanasema kwamba tabia hii inaonyesha jinsi watu wanavyozidi kupenda vya dunia wakitafuta kununua mapenzi kwa mabadilishano ya pesa, badala ya mapenzi ya kweli.
"Ni aina fulani ya shinikizo," Haskell Austin mwenye umri wa miaka 24 anaiambia BBC.
Anapendelea zawadi ya maua, akielezea wazo la kutoa zawadi ya pesa kama "kukosa uhalisia".
Lakini ikiwa ni lazima pesa taslimu itolewe, anapendelea kupewa pesa moja kwa moja badala ya mtindo wa kuikunja au kuipamba katika shada la maua.
Mwanamke anayejitambulisha kama Lynn pekee amekatishwa tamaa wakati CBK ilipotoa tahadhari kuhusu mashada ya maua ya pesa taslimu, iliyotolewa kabla ya Siku ya Wapendanao, kwani alikuwa akitarajia kupokea moja.
"Watu bado wanafurahishwa na mtindo huu," anaambia BBC katika Mtaa wa Koinange, eneo maarufu la kununua maua ya mashada ya pesa Taslim jijini Nairobi.
"Ningependelea pesa taslimu," Nicole Rono anaiambia BBC. "Nani asiyependa pesa? Maua yako sawa, ndiyo, lakini sasa kwa kile ambacho CBK imesema, bado unaweza kutoa pesa taslimu bila kuziharibu," anasema.
Kwa mwanafunzi wa chuo kikuu Benjamin Nambwaya, ukweli kwamba wanawake kwa kawaida ndio wapokeaji unatokana na matarajio ya kijamii.
Anaiambia BBC kwamba utamaduni wa kutoa mashada ya pesa ni "jambo baya" na unaweza kuishia "kuharibu mahusiano", hasa inaposababisha matarajio hata wakati mtu hawezi kumudu kutoa pesa.
Angependelea zawadi ya maua.
"Maua ni mazuri, kwa sababu hii ni sherehe ndogo au kitu cha kuonyesha jinsi unavyompenda mtu wako," anasema.
Mtaalamu wa uchumi Odhiambo Ramogi anasema yote yanahusu "mbinu yetu ya kibepari katika maisha".
"Jamii za kibepari zinazoendeshwa na matangazo na siku maalum kama za wapendanao ni fursa nzuri sana."
Kwa Muthoni, muuza maua, inategemea jinsi mtu anavyotaka kuonyesha upendo wake.
"Wapende watu jinsi wanavyotaka kupendwa," anasema, ingawa anakubali kwamba hatimaye pesa ndio kiini cha yote.
"Unaweza kununua vitu vingi kwa pesa. Huenda usijue mtu anapenda nini, lakini pesa ndiyo suluhisho."
Majadiliano kuhusu mashada ya pesa yamekuwa yakienea kwenye mitandao ya kijamii tangu onyo la CBK, na kusababisha mijadala.
Imeibua ucheshi pia, kama vile vibonzo vya mashada ya maua vilivyotengenezwa kwa chapati zilizokunjwa.
Akizungumzia kuhusu mtindo huo kwenye TikTok, Mkenya Scott Ian Obaro alisema huenda pia ulichochea utamaduni wa "kujionyesha".
Ramogi anasema kwamba wazo la kutoa maua kwa kiasi kikubwa ni dhana ya kigeni barani Afrika, ambayo anasema husaidia kuelezea ni kwa nini utamaduni wa kutoa zawadi za pesa unakumbatiwa kwa urahisi zaidi.
"Mwafrika alikuwa akitoa maua kwa shida sana," anasema, akiongeza kwamba desturi hiyo ni utamaduni wa Magharibi na kwamba Wakenya wengi wangependelea pesa "kutatua hitaji" lako badala ya ua linalotolewa kwa sababu za hisia tu.
"Lakini sasa imehusishwa na ukweli kwamba tunazidi watu wa kupenda vya uwongo. Ua la asili limebadilishwa na ua la sarafu," anasema.
Kuingilia kati kwa mdhibiti wa Kenya, pamoja na wale walio katika nchi zingine, kunaweza kupunguza utamaduni wa kutoa ma ya maua.
Muthoni anahofia hatua hiyo inaweza kusababisha hasara ya mapato kwa watu ambao wanapata riziki kwa kutengeneza shada la maua, ingawa anaamini kuna kuna fursa ya uvumbuzi.
Anasema amebuni shada zenye mifuko inayoweza kuhifadhi pesa bila kuharibika na anafikiria mawazo mengine kama vile shada za kidijitali.
Baadhi wamebadili na kutumia dola za Marekani, jambo ambalo halingeathiriwa na onyo kutoka benki kuu ya Kenya.
Hivyo basi, utamaduni wa maua ya pesa hautaondolewa hivi karibuni.
Imefasiriwa na Asha Juma