Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siku ya kondomu na siku ya wapendanao: Je, upewe kondomu au maua?
Februari 13 ya kila mwaka ni siku ya kondomu duniani, huadhimishwa siku moja kabla ya siku ya wapendanao maarufu kama Valentines Day. Uamuzi wa kuiweka karibu na Februari 14, siku ya wapendanao si wa bahati mbaya, bali ni ujumbe kwamba mapenzi na uwajibikaji wa afya vinapaswa kwenda pamoja.
Lengo la siku hii ni kuhamasisha matumizi sahihi ya kondomu kama njia ya kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukwimi (VVU), magonjwa mengine ya zinaa pamoja na mimba zisizotarajiwa. Ni siku inayokumbusha kwamba kinga ni sehemu ya heshima kwa mwenzi wako na kwa afya yako mwenyewe.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS), watu wanaokadiriwa kufikia milioni 40 wanaishi na VVU duniani kufikia mwaka 2024. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa janga la VVU bado lipo na halijaisha.
Katika mazingira haya, kondomu imeendelea kuwa moja ya nyenzo muhimu zaidi za afya ya umma duniani. Ni chombo rahisi, chenye gharama nafuu na kinachopatikana kwa urahisi, lakini matumizi yake bado yanakabiliwa na changamoto za kijamii, kiutamaduni na kielimu.
Ngozi, vitambaa, hadi mipira, safari ya kipekee ya kondomu
Kondomu ziliibuka kama njia ya kinga kama mapambano dhidi ya magonjwa ya zinaa na mimba zisizotarajiwa kwa karne nyingi. Awali hasa karivu miaka 3,000 huko nyuma watu walijikinga kwa kutumia ngozi za wanyama au mifuko ya vitambaa, Mtindo unaotajwa na wanahistoria kuanzia Misri na China.
Kwa wale wa karne hizo, vifaa hivi vilionekana kuwa sahihi na salama, lakini ufanisi wake ulikuwa mdogo na hatari ya maambukizi iliendelea kuonekana. Katika karne ya 18, kondomu ilikuwa bidhaa ya gharama kubwa, na kuzikosa wengi kutokana na gharama.
Mapinduzi makubwa yalikuja karne ya 20 pale mipira (latex) ilipoanza kutumika kutengeneza kondomu. zilitengenezwa kondomu nyepesi, rahisi kutumia na yenye ufanisi mkubwa wa kinga. Kondomu za mipira zinazoendelea kutumika mpaka sasa ziilibadilisha kabisa mfumo wa kinga na kuifanya kondomu kuwa chombo cha afya ya umma.
Katika safari ya kuhahamisha matumizi yake, huwezi kuacha kumtaja Mechai Viravaidya, mwanaarakati wa afya nchini Thailand. Huyu anayejulikana duniani kama "Mr. Condom" kwa kazi yake ya kuhamasisha matumizi ya kondomu Thailand na ulimwenguni. Yeye aanaeleza jinsi uvumbuzi huu ulivyobadilisha maisha ya mamilioni ya watu kwa kupunguza idadi ya watoto na kupunguza maambukizi ya magonjwa ya zinaa. "Tulijifunza kuwa elimu na upatikanaji wa kondomu ni ufunguo wa afya ya jamii," anasema.
Ingawa kuna changamoto za kijamii na kitamaduni, historia inaonyesha kwamba teknolojia na elimu vinapounganishwa, zinapata mafanikio makubwa katika kubadilisha tabia za afya ya uzazi.
Maswali kuhusu ufanisi na takwimu za maambukizi
Pamoja na uwepo wa kondomu za kisasa ambazo uwezo wake umethibitishwa na Shirika la afya duniani (WHO) kwa asilimia zaidi ya 98%, bado wapo wasiotumia, wanaotumia isivyo salama, na wanaoamini katika matumizi ya mbadala mwingine kama mifuko ya plastiki.
Na hawa wanatajwa kuchangia ongezeko la maambukizi ya virusi vya ukimwi, mimba zisizoza lazima au ambazo hazikupangwa na magonjwa mengine. Ukiacha watu zaidi ya milioni 40 kuishi na maambukizi ya Ukimwi duniani, WHO inasema kila mwaka ulimwenguni watu milioni zaidi ya 300 huambukizwa magonjwa ya zinaa wengi wakiwa ni wa umri wakati ya miaka 15-49. Huku upande wa UKWIMWI maambukizi mapya milioni 1.7 yanatokea kila mwaka.
Hata kwa nchi za Afrika Mashariki, hali tete kuhusu kondomu na maambukizi ya Ukimwi. Nchini Tanzania, kwa mfano, vijana wenye umri wa 15-24 wako kwenye hatari kubwa ya maambukizi ya VVU, huku wanawake wakitajwa kuchangia kwa asilimia 80 ya maambukizi mapya. licha ya kupungua kwa yamepungua kwa wastani wa 2.6%. Hili linahusishwa na kupungua kwa matumizi sahihi na salama ya kondomu kama ilivyoeleza mwaka jana na Kaimu Mganga Mkuu nchini Tanzania, Dk. Ziada Sellah.
Kwa mujibu wa ripoti za serikali nchini Uganda, watu wanne kati ya 100 wameambukizwa HIV, huku eneo la Fort portal ni wastani wa watu 12 kati ya 100 wameambukizwa. Licha ya kupiga hatua katika kuunguza maambukizi ya ukimwi kwa asilimia 60% katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Kenya bado haijafikia lengo lake la kupunguza ugonjwa huo kwa 75% kufikia mwaka 2025.
Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) nchini Tanzania, Dkt. Zeye Nkomela, aliwahi kueleza hivi karibuni kuwa: "Bado kuna dhana potofu na unyanyapaa kuhusu matumizi ya kondomu. Hii inasababisha baadhi ya watu kujihusisha na ngono isiyo salama.
Kama kondomu ingepatikana kila mahali, kwa urahisi na kutumika ipasavyo kwa usahihi na usalama, zana hii ingekuwa muarobaini wa muhimu wa kudhibiti maambukizi na kulinda afya ya kizazi cha sasa na kijacho duniani kote.