Kwanini unapaswa kubadilisha mashuka ya kitandani mara kwa mara?

    • Author, Jasmin Fox-Skelly
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Juu ya mashuka yetu na mito ni mahali tunapotumia theluthi moja ya maisha yetu ya kila siku. Baada ya siku ndefu, hakuna kitu kizuri kama kujitupa juu ya kitanda, kuegemeza kichwa chako kwenye mto laini na kujikunyata ndani ya shuka laini.

Lakini jambo la kuogofya kuhusu kitanda chako ni kwamba kuna mamilioni ya bakteria, fangasi, wadudu na virusi. Kila mmoja wao anadhani kitanda chako ni peponi kwake; mahali penye joto ambapo wanaweza kukua, pamejaa jasho, mate, chembechembe za ngozi zilizokufa na ndio chakula kwa ajili yao.

Mfano, vijidudu vidogo sana vinavyoishi kwenye vumbi. Tunamwaga seli za ngozi milioni 500 kwa siku, vijidudu hivyo hula seli hizo. Kwa bahati mbaya, vidudu hivyo na mabaki yake (kinyesi) vinaweza kusababisha mzio, pumu na ukurutu.

Mashuka ya kitanda ni kimbilio la bakteria pia. Mwaka 2013, watafiti katika Taasisi ya Pasteur de Lille huko Ufaransa walichunguza mashuka ya kitanda cha hospitali na kugundua yamejaa bakteria wa Staphylococcus, ambao hupatikana zaidi kwenye ngozi ya binadamu.

Ingawa spishi nyingi za staphylococcus hazina madhara, lakini baadhi, kama vile S. aureus, wanaweza kusababisha maambukizi ya ngozi, chunusi na hata nimonia kwa wagonjwa walio na kinga dhaifu.

"Watu hubeba bakteria wengi katika ngozi zao," anasema Manal Mohammed, mwanabiolojia wa Chuo Kikuu cha Westminster nchini Uingereza.

"Ingawa bakteria hawa kwa kawaida hawana madhara, ila wanaweza kusababisha ugonjwa mbaya ikiwa wataingia mwilini kupitia majeraha ya wazi, ambayo ni ya kawaida katika hospitali," anasema Manal.

Vitanda vya hospitali

Mwaka 2018, wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Ibadan nchini Nigeria walipata bakteria wa E. koli katika mashuka ya kitanda cha hospitali ambayo hayajafuliwa, pamoja na bakteria wengine wa pathogenic wanaojulikana kusababisha maambukizi ya njia ya mkojo, nimonia, kuhara, homa ya uti wa mgongo na sumu katika damu.

Mwaka 2022, watafiti walikusanya sampuli kutoka vyumba vya wagonjwa waliolazwa hospitalini kwa ugonjwa wa mpox. Waligundua kuwa kitendo cha kubadilisha shuka la kitanda hutoa chembe za virusi kwenye hewa.

Mwaka 2018, mfanyakazi wa afya wa Uingereza inaaminika alipata ugonjwa huo baada ya kuambukizwa virusi wakati akibadilisha mashuka ya kitanda cha mgonjwa.

"Mashuka ya hospitalini huoshwa kwenye maji makali ya moto, ambayo huua bakteria wengi," anasema David Denning, profesa wa magonjwa ya kuambukiza katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza.

Isipokuwa bakteria wa C. difficile, ambaye husababisha kuhara, hasa kwa watu wazee. Kuosha kunaweza kuharibu nusu ya bakteria C. difficile, lakini seli za bakteria hao ni vigumu kufa. Hata hivyo, viwango vya maambukizi ya C. difficile vimepungua nchini Uingereza.

Bila shaka, kuna uwezekano mkubwa wa kupata bakteria wa pathogenic katika kitanda cha hospitali ambapo mgonjwa amelala kuliko katika kitanda cha mtu mwenye afya.

Vitanda vya Nyumbani

Mwaka 2013, kampuni ya vitanda ya Marekani ya Amerisleep ilichukua sampuli kutoka katika foronya ambayo haikuwa imeoshwa kwa wiki moja. IIikuwa na takribani bakteria milioni tatu kwa kila nchi ya mraba - takribani mara 17,000 zaidi ya bakteria waliopo kwenye sinki la choo.

Mwaka 2006, Denning na wenzake walikusanya mito sita kutoka kwa marafiki na familia. Mito hiyo ilikuwa ikitumika mara kwa mara na ilikuwa na umri wa kati ya miezi 18 na miaka 20. Mito yote ilikuwa na fangasi, hasa aina ya Aspergillus fumigatus - ambao hupatikana kwa wingi kwenye udongo.

"Unazungumza mabilioni au matrilioni ya chembe za fangasi kwenye kila mto," anasema Denning.

"Chanzo cha kupatikana fangasi wengi ni kwa sababu wengi wetu tunatokwa na jasho usiku. Pia sote tuna wadudu wa vumbi vitandani mwetu, na kinyesi cha wadudu hao hutoa chakula kwa fangasi. Na kisha jioni mto hupata joto kwa sababu kichwa chako hulala hapo, kwa hivyo kuna unyevu, kuna chakula, na kuna joto.”

Kwa kuwa wengi wetu huwa hatuoshi mito yetu, fangasi huishi katika hali ya utulivu na wanaweza kuishi kwa miaka. Hata kama utaosha foronya, fangasi wanaweza kuishi katika halijoto ya hadi nyuzi joto 50C (122F), na kwa vyovyote vile kuosha mito au foronya kunaweza kuifanya iwe na unyevu zaidi, na hivyo kuruhusu kukua zaidi.

Athari za kiafya

Kwa kuzingatia muda ambao watu hutumia kulala, na ukaribu wa mto kwa mdomo, mazingira hayo yana athari kwa watu wenye ugonjwa wa kupumua, haswa pumu na maambukizi kwenye pua.

Takribani nusu ya watu walio na pumu kali wana mzio na vimelea vya Aspergillus fumigatus, vimelea vinavyoweza kusababisha ugonjwa sugu wa mapafu kwa watu ambao hapo awali waliugua TB au ugonjwa wa mapafu unaohusiana na uvutaji sigara.

Kulingana na Denning, 99.9% ya watu walio na mfumo mzuri wa kinga ya mwili wanaweza kustahimili kuvuta vimelea vya A. fumigatus, kwa watu walio na kinga dhaifu, fangasi hao wanaweza kuuzidi nguvu ulinzi dhaifu wa mwili na kusababisha maambukizi ya kutishia maisha.

"Ikiwa una saratani ya damu, au umepandikizwa kiungo, au una bahati mbaya ya kuwa umeishi na Covid au mafua kwa muda mrefu, vimelea hivyo vinaweza huingia kwenye mapafu na kuendelea huharibu tishu za mapafu," anasema Denning.

Kipi cha kufanya?

Ikiwa kuosha mito, mashuka na foronya haisaidii, kuna chochote tunaweza kufanya? Kulingana na Denning, ikiwa huna pumu, au ugonjwa wa mapafu au kupumua, basi unapaswa kubadilisha mto wako kila baada ya miaka miwili. Lakini watu ambao wanakabiliwa na hali hizi wanapaswa kununua mto mpya kila baada ya miezi mitatu hadi sita.

Linapokuja suala la mara ngapi unapaswa kuosha foronya za kitanda na mashuka, wataalam wengi wanapendekeza kufanya hivyo kila baada ya wiki moja. Pamoja na kupiga pasi ili kupunguza idadi ya bakteria.

"Ikiwa huna muda wa kufanya hivyo, basi piga pasi mashuka na foronya zako. Sisi sote tuna bakteria katika miili yetu, kwa hivyo kwa mtu mwenye afya njema haileti tatizo sana," anasema Denning.

"Lakini ikiwa wewe ni mgonjwa na una hatari nyingine, au una mtoto anayejikojolea - basi unapaswa kuwa mwangalifu zaidi kuhusu kuosha kwa kutumia maji moto makali."

Kulala na mnyama (paka au mbwa) kitandani pia kunaongeza idadi ya bakteria na fangasi, kulala kabla ya kuoga, kulala na soksi chafu au kulala ukiwa umejipodoa au na losheni kwenye ngozi yako na pia kula vitafunio kitandani.

"Sisemi kwamba watu wasile kitandani lakini ikiwa utafanya hivyo basi kuosha shuka mara kwa mara ni muhimu, na kuosha kila wiki ndio njia salama," anasema Denning.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah