Kivuli cha vita na Israel chawagubika Walebanon walio na wasiwasi

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Hugo Bachega
- Nafasi, BBC Middle East correspondent
- Akiripoti kutoka, Beirut
Wiki mbili zilizopita, Hassan Nasrallah, katibu mkuu wa muda mrefu wa Hezbollah mwenye ushawishi mkubwa, alitoa hotuba kwa njia ya televisheni kutoka eneo lisilojulikana nchini Lebanon kumuenzi Taleb Abdallah, afisa mkuu wa kundi hilo aliyeuawa kwenye mashambulizi ya Israel katika ghasia za sasa.
Bw Nasrallah, ambaye alizungumza kwa takribani saa moja, alisisitiza kwamba wanamgambo wa Lebanon wanaoungwa mkono na Iran na chama cha kisiasa hawataki vita vya pande mbili na Israel lakini, endapo itatokea, watapigana "bila vikwazo au sheria".
Pia alisema Hezbollah imetuma "sehemu tu" ya kitengo cha jeshi lake, na kuonya "adui" "kutarajia uwepo wetu ardhini, baharini na angani". Jambo la kushangaza ni kwamba hata aliitishia Cyprus, mwanachama wa Umoja wa Ulaya, ikiwa itaruhusu eneo lake kutumiwa na Israel kuanzisha mashambulizi dhidi ya kundi hilo.
Wafuasi, waliokusanyika katika maonyesho yaliyoandaliwa na Hezbollah, walimkatisha mara kadhaa kwa makofi ya kishindo, wakiimba "Labbaika ya Nasrallah", kumaanisha "Tuko kwenye huduma yako, Nasrallah".
Sio tu maneno yalionekana kuongezeka. Siku zilizopita, Hezbollah ilikuwa imejibu mauaji ya tarehe 12 Juni ya Abdallah, ambaye pia anajulikana kama Abu Taleb, kwa msururu wa shambulio la makombora kuelekea kaskazini mwa Israel. Zaidi ya watu 200 walifukuzwa kazi kwa siku moja, kulingana na jeshi la Israel, na kusababisha uharibifu mdogo.
Lilikuwa ni shambulizi kali zaidi tangu kuanza kwa uhasama mwezi Oktoba, likizusha hofu kwamba mapigano hayo yanaweza kusababisha mgogoro mkubwa zaidi.

Chanzo cha picha, EPA
Kwa miezi kadhaa, swali la iwapo Lebanon itaingizwa kwenye vita vingine limetawala maisha katika nchi hii. Ni kile ambacho watu mara nyingi huelezea kama "hali", wasiwasi wa mara kwa mara ambao kivuli chake kinatanda kila mahali.
Lakini Walebanon wameendelea na maisha yao ya kawaida, taswira ambayo ilinaswa kikamilifu katika picha ya waotaji jua wasio na wasiwasi huko Tiro mwezi uliopita huku moshi mwingi ukifuka kwa mbali baada ya shambulio la Israel.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mvutano, ambao tayari umekuwepo, uliongezeka zaidi baada ya hotuba ya Bw Nasrallah. Nilipokuwa nikimtazama kwenye TV, niliona kupitia dirishani mwanamume aliyekuwa akiweka mabango ya rangi ya waridi na buluu kwenye kuta huko Ashrafieh, eneo maarufu la Beirut mashariki, akitangaza karamu.
“Tukifunga maisha yetu... nchi itasimama. Lazima tuendelee,” mratibu, Raymonda Chamoun mwenye umri wa miaka 35, aliniambia siku chache baadaye. “Tunaweza kufanya nini? Tutalifikiria likitokea."
"Nina begi la kutoka [katika nyumba yangu] mambo yakibadilika. Limekuwa karibu na mlango wangu, ndani ya begi hilo kuna vitu muhimu. Maji, huduma ya kwanza, chaja ya simu. Wazazi wangu walinifundisha hivyo kitambo sana, kwa sababu walizaliwa na kukua wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchni Lebanon."
Mashambulizi ya Hezbollah yalianza tarehe 8 Oktoba, siku moja baada ya shambulio baya la Hamas dhidi ya Israel.
Kundi hilo limesema operesheni hiyo, ya kuwaunga mkono Wapalestina wakati wa vita vya Israel dhidi ya Hamas, itakomehshwa wakati vita vitakapositishwa huko Gaza.
Marekani imeongoza juhudi za suluhu la kidiplomasia katika mvutano lakini Hezbollah na Israel zimeonyesha nia ya kuepusha mzozo mkubwa. Hali hii ikigeuka inaweza kuwa mbaya kiuhalisia.
Ghasia nyingi zimesalia katika maeneo ya mpakani, ingawa shambulio la Israel limezidi kulenga shabaha ndani ya Lebanon. Mashambulizi ya Hezbollah pia yamefika mbali hadi Israel. Kufikia sasa, zaidi ya watu 400 wameripotiwa kuuawa nchini Lebanon, wengi wao wapiganaji wa Hezbollah, na 25 nchini Israel, wengi wao wakiwa wanajeshi.
Kusini mwa Lebanon, ngome ya Hezbollah, takriban wakazi 90,000 wamekimbia, kulingana na Umoja wa Mataifa. Vijiji ni tupu na nyumba na majengo mengine yameharibiwa. Mashamba yamechomwa na fosforasi nyeupe iliyoangushwa na Israel, katika hatua inayoonekana kuwa jaribio la kuunda eneo maalum na kuzuia uwepo wa kikundi huko.
Nyumba ya Kameli Hammaid huko Meiss El Jabal, ng'ambo ya mpaka kutoka mji wa Kiryat Shmona wa Israel, ilikuwa imejengwa na mababu zake, ikiwa na miti ya mizeituni kwenye bustani na ukumbi mkubwa wa mkutano.
"Ilikuwa mahali ambapo kila watu vijijini wangekusanyika," Kameli aliniambia huko Beirut, anakoishi.
Alionyesha picha za uharibifu ambao, alisema, ulisababishwa na roketi mbili za Israel. Roshani ya ghorofa ya pili ilianguka, na kuharibu kila kitu.
“Naenda kulala na kuamka nikibubujikwa na machozi. Hii ndiyo historia ya familia yangu,” Kameli, mshonaji nguo wa miaka 54 alisema. "Nina wasiwasi kuwa mambo yanaweza kuharibika bila shaka nina wasiwasi." Lakini hakuna kitu ambacho angeweza kufanya - "ni kuomba Mungu tu".
Nchini Israel, ambapo maelfu ya watu wamehamishwa kutoka jamii za kaskazini, na maeneo makubwa ya ardhi kuharibiwa na moto uliochochewa na roketi za Hezbollah, mamlaka zinakabiliwa na shinikizo kubwa kuchukua hatua. Lakini maafisa wa Magharibi wanasema hakuna uamuzi wowote ambao umefanywa.

Chanzo cha picha, Reuters
Kupunguzwa kwa operesheni za kijeshi za Israeli huko Gaza kunaweza kusababisha wanajeshi zaidi kutumwa kwenye mpaka wa kaskazini. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema usalama utarejeshwa "kwa njia moja au nyingine", na kwamba jeshi "limejiandaa kwa hatua kali", ingawa baadhi ya matamshi yake ya hivi majuzi yamekuwa yakiashiria makabiliano.
Hezbollah, inayoonekana kuwa adui wa kutisha zaidi kuliko Hamas, imekuwa ikijiandaa kwa mzozo mwingine na Israel tangu mzozo wao wa mwisho mwaka 2006. Kundi hilo lina takriban roketi na makombora 150,000, kulingana na makadirio ya mataifa ya Magharibi, ambayo yanaweza kuzishinda mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga ya Israel.
Silaha hizo ni pamoja na ndege zisizo na rubani na makombora yanayoongozwa kwa usahihi yenye uwezo wa kushambulia ndani ya Israel. Hezbollah pia inategemea maelfu ya wanaume ambao wana uzoefu w vita kutokana na mapigano katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, na Hassan Nasrallah ameionya Israel kutarajia "mshangao" endapo watafanya mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi ya Israel.
Makundi mengine yanayoungwa mkono na Iran katika eneo hilo, sehemu ya kile Tehran inachokiita "Mhimili wa Upinzani", yameapa kujiunga na vita. "Vita huenda visitokee lakini haviepukiki," afisa mkuu wa Hezbollah aliniambia.
Lebanon, wakati huo huo, imekuwa katika hali ya mgogoro wa kudumu kwa zaidi ya nusu muongo. Mnamo 2020, ilikumbwa na janga la Covid-19; kisha, ikafuatiwa na mlipuko wa bandari ya Beirut.
Uchumi umeporomoka, huku asilimia 80 ya watu wakikadiriwa kuwa katika umaskini. Hakujawa na rais kwa takriban miaka miwili kwa sababu ya mizozo ya kisiasa inayoonekana kutoisha.
Vita vyovyote vinaweza kuwa mbaya kwa nchi, na serikali ina ushawishi mdogo - ikiwa upo - juu ya kundi ambalo, kama Hamas, linachukuliwa kuwa shirika la kigaidi na Uingereza, Marekani na wengine.
"Kinachotokea tayari kinatuathiri sisi sote," Faad Assaf, mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 48, aliniambia hivi majuzi. Duka alilofanya kazi huko Hamra, Beirut, lilikuwa tupu. "Tunaogopa kizazi kipya. Hatutaki waishi yale tuliyopitia - vita."
Kama Raymonda Chamoun, mratibu wa chama, alivyosema: "Hali ya jumla nchini ni ya uchovu. Watu wamechoka.”
Taarifa ya ziada ya Leena Saidi
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah












