Raila Odinga:Mahakama ya Juu zaidi itakubali maombi yetu kwa sababu tuna ushahidi thabiti

Na Richard Kagoe

BBC News, Nairobi

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga anasema ana imani kuwa Mahakama ya Juu itakubali maombi yao akitaja ushahidi thabiti katika kesi ya kupinga kutangazwa kwa mpinzani wake William Ruto kuwa Rais mteule kufuatia uchaguzi wa Agosti 9.

Bw Odinga anasema ataheshimu matokeo ya uamuzi wa mahakama. Anasema uamuzi huo unaweza kuwa na athari kubwa katika michakato ya uchaguzi kote barani Afrika.

Anasema mustakabali wa demokrasia barani Afrika uko hatarini akitoa mfano wa kurudi nyuma katika baadhi ya nchi za Afrika.

Akisisitiza kwamba wana Imani kwamba walishinda uchaguzi huu kwa kura nyingi zaidi, Raila amesema kwamba tatizo lilitokea wakati wa kurusha matokeo.

‘’Kulikuwa na tofauti kubwa kuhusu matokeo yaliokuwa katika sava ya Tume ya uchaguzi IEBC na matokeo yaliokuwa yakitoka katika vituo vya kupiga kura’’, alisema Raila

Raila amesema kwamba kulikuwa na uvamizi katika sava ya tume ya uchaguzi kutoka katika vituo vya kupigia kura na kwamba matokeo kutoka vituo vya kupigia kura yalikuwa yanavamiwa na kubadilishwa kabla ya kufikia sava ya Tume ya Uchaguzi.

Amesema kwamba ni hatua hiyo iliosaidia kuongezwa kwa kura za mpinzani wake huku kura zake zikipunguzwa, ushahidi anaosema kwamba umewasilishwa mbele ya mahakama.

Alisema kwamba pingamizi hiyo dhidi ya uchaguzi haisaidii Wakenya pekee, bali pia Jumuiya ya Afrika na dunia kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa kumepatikana tiba ya wizi wa kura.

Alipoulizwa iwapo yuko tayari kukubali uamuzi wa mahakama, Raila amesema kwamba ndio atakubali kwani sio mara ya kwanza kukubali matokeo.

Anasema kwamba mwaka 2007 kulikuwa na mahakama ambayo haikuwa huru , tukakataa kwenda mahakamni na matokeo yakawa ghasia za baada ya uchaguzi zilizosababisha maafa mengi.

‘’Mwaka 2017, kura iliibiwa na mahakama ikakubaliana na sisi ikaitisha marudio tukaona kwamba ni makosa kurudia uchaguzi huo ilhali makosa hayajarekebishwa, hatuwezi kufanya kitu vile tulifanya hapo mbeleni na kuratajia matokeo tofauti , huo ni ujinga na ndio maana tukasusia huo uchaguzi’’, alisema Kiongozi huyo wa Muungano wa Azimio.

''Mara hii alisema Muungano wa Azimio unatarajia mahakama itatoa uamuzi ikubaliane na sisi na vilevile itoe uamuzi wa marekebisho''.

Hatahivyo aliongezea kwamba Muungano huo hauwezi kutoa masharti kwani mahakama hiyo ina uhuru kutoa uamuzi wanaoona ni sawa.

Mwanasiasa huyo aliongezea kwamba kesi hiyo ni mfano kwa ulimwengu mzima na kwamba mwishowe ni wananchi ndio watakaofaidika.