Nchi 10 ambazo watu wanaishi muda mrefu zaidi na kile tunachoweza kujifunza

Chanzo cha picha, Getty Images
Lucile Randon alikuwa mtu mzee zaidi duniani alipofariki Januari akiwa na umri wa miaka 118.
Mtawa huyo Mfaransa anayejulikana kama Sister André alishuhudia vita viwili vya Dunia, kutua kwa wanadamu kwenye mwezi, na enzi ya kidijitali.
Hadithi yake bado ni ya kipekee, ikizingatiwa kwamba wastani wa kuishi duniani ni miaka 73.1.
Hata hivyo, kila siku inayopita watu wanaishi muda mrefu na wastani wa maisha marefu unatarajiwa kuzidi77 katikati ya karne hii, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.
Kadri umri wa kuishi unavyoongezeka, kiwango cha watoto wanaozaliwa pia kinapungua, jambo ambalo linatufanya kuwa watu wenye umri mkubwa zaidi.
Dunia tayari inakaliwa na watu wengi zaidi ya miaka 65 kuliko chini ya miaka mitano, ingawa hali inatofautiana sana kutoka nchi moja hadi nyingine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati Monaco umri wa kuishi ni miaka 87, katika Jamhuri ya Chad, nchi maskini iliyoko Afrika ya Kati, ni karibu miaka 53.
Baada Monaco, inafuata na mikoa maalum ya utawala ya China Hong Kong na Macao, huku nafasi ya nne inashikiliwa na Japan, ambayo ni nchi iliyo na idadi kubwa ya watu wanaoishi kwa muda mrefu zaidi miongoni mwa mataifa yenye nguvu duniani.
Orodha hiyo imekamilishwa na Liechtenstein, Uswizi, Singapore, Italia, Korea Kusini na Uhispania, kulingana na ripoti ya UN ya Makadirio ya Idadi ya Watu Duniani.
Ukiachilia mbali magonjwa ya milipuko na vita vya dunia, umri wa kuishi umeongezeka kwa kasi kote duniani katika kipindi cha miaka 200 iliyopita na maendeleo ya chanjo na viuavijasumu, dawa bora, usafi wa mazingira, chakula, na hali ya maisha.
"Maamuzi ya busara"
Ijapokuwa kenetiki ni mojawapo ya sababu zinazoamua zaidi, maisha marefu kawaida huhusishwa na hali ya maisha ya mahali ambapo mtu alizaliwa na maamuzi yao kama mtu binafsi.
Si tu kuhusu kupata mfumo bora wa afya na mlo bora, lakini pia kuhusu kile ambacho wataalam wanakiita "maamuzi ya busara" katika suala la kuwa na mlo kamili, kupata usingizi wa kutosha, kudhibiti viwango vya msongo wa mawazo au kufanya mazoezi.
Nchi ambazo zina watu walioishi kwa miaka mingi zaidi wa zina kitu kimoja ambacho kinajitokeza miongoni mwazo: kiwango cha juu cha mapato. Lakini kuna kitu kingine kinachowaunganisha: idasi.
Patrick Gerland, mkuu wa kitengo cha Makadirio ya Idadi ya Watu na katika Umoja wa Mataifa, anaonya kwamba kuna nchi zilizopo kwenye orodha hiyo kama vile Monaco au Liechtenstein ambazo ni ndogo sana, kiasi kwamba haziwakilishi idadi ya watu tofauti kuliko mataifa mengine.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Zinaonekana kama nchi za kipekee, lakini kwa kweli ni aina ya idadi ya watu bandia. Sio mchanganyiko wa watu bila mpangilio kama inavyotokea katika sehemu nyingine za dunia."
"Wanachoshiriki ni kiwango cha juu cha maisha, upatikanaji wa huduma bora za afya na elimu, lakini sio uteuzi wa kijenetiki," anasema Gerland katika mazungumzo na BBC Mundo.
Tofauti zinaweza kuonekana kati ya nchi na pia ndani ya nchi moja. Pale ambapo kuna ukosefu wa usawa zaidi, pengo la umri wa kuishi kati ya makundi ya kijamii huongezeka.
"Nchi nyingi za Skandinavia, kwa mfano, ni jumuiya zenye usawa zaidi zenye umri mrefu wa kuishi," anaongeza.
Ukanda wa bluu au "paradiso za maisha marefu"
Kanda za bluu ni idadi ndogo sana ambapo watu wanaishi muda mrefu zaidi kuliko watu wengine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Miongo michache iliyopita, mwanademografia Michel Poulain na mtaalamu wa gerontologist Gianni Pes walijitolea kuchunguza mahali ambapo watu wazee waliishi ulimwenguni.
Wangechora duara kwenye ramani yenye alama ya buluu nene katika miji ambayo watu walifikia umri wa miaka 100.
Hivyo ndivyo walivyoona kwamba moja ya sehemu za ramani iliyotiwa rangi ya buluu ilikuwa eneo la Barbagia, kwenye kisiwa cha Italia cha Sardinia, na wakaishia kuiita "eneo la bluu". Tangu wakati huo, jina hilo limehusishwa na maeneo ambayo wenyeji wanafurahia maisha marefu ya ajabu katika hali nzuri ya maisha.
Kulingana na utafiti huu, mwanahabari Dan Buettner alikusanya timu ya wataalamu kutafuta jamii nyingine ambapo jambo kama hilo lilirudiwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Matokeo yake, waligundua kwamba, pamoja na Sardinia, kulikuwa na kanda nyingine nne za bluu: kisiwa cha Okinawa huko Japan, mji wa Nicoya huko Costa Rica; kisiwa cha Icaria, huko Ugiriki; na jumuiya ya Waadventista wa Loma Linda huko California.
Hapana shaka kwamba fursa ya chembe za urithi ni muhimu ili kuishi muda mrefu zaidi huku tukihifadhi uwezo mwingi wa kimwili na kiakili.
Lakini kikundi cha wanasayansi (kilichoundwa na madaktari, wanaanthropolojia, wanademografia, wataalamu wa lishe, wataalam wa magonjwa) walishangaa ni vitu gani vingine vinavyoathiri maeneo ya bluu.
Na wakaenda kusafiri sehemu mbalimbali za dunia.
Miaka michache baadaye, Buettner alichapisha mnamo 2008 kitabu chake "The Blue Zones: Lessons for Living Longer from the People Who have Lived the Longest" na kuanzia hapo akajitolea kuendeleza dhana hii.
Walakini, sio kila mtu anayekubaliana na taarifa za mwandishi, kwani wanaona kuwa taarifa zake nyingi zinatokana na uchunguzi, badala ya masomo ya kisayansi ya muda mrefu.
Kanda za bluu zinafanana nini?
Buettner na timu yake walipata mifumo ya kawaida katika jumuiya zilizosomwa ambayo inaweza kueleza kinadharia kwa nini watu hao wana maisha marefu na ubora bora wa maisha kuliko ulimwengu wote. Miongoni mwao ni yafuatayo:

Chanzo cha picha, Getty Images
Wana kusudi maishani: "ikigai", neno la Kijapani linalotumiwa kurejelea "sababu za kuwa" au kwa usahihi zaidi, sababu ambazo zinatufanya tunaamka kila asubuhi.
- Wanakuza uhusiano wa kifamilia.
- Wanapunguza msongo wa mawazo kwa kukatiza mdundo wa kawaida wa utaratibu ili kutoa nafasi kwa shughuli nyingine ambazo ni sehemu ya mazoea ya kawaida ya kijamii. Kwa mfano, kuchukua kulala katika jamii za Mediterranean, kuomba katika kesi ya Waadventista, kufanya sherehe ya chai kwa wanawake katika Okinawa.
- Wanakula bila kushiba: tu hadi 80% ya uwezo wetu kwa wakati wowote.
- Wana lishe bora inayojumuisha mboga nyingi, kunde, na matunda.
- Wanakunywa pombe kwa wastani.
- Wanafanya mazoezi ya kawaida ya mwili kama sehemu ya shughuli za kila siku, kama vile kutembea.
- Wana hisia kali za jumuiya na kushiriki katika miduara ya kijamii ambayo inakuza tabia nzuri.
- Wao ni sehemu ya vikundi vinavyokuza imani au dini
Yote haya katika muktadha unaojumuisha, kati ya mambo mengine, hali ya hewa ya kirafiki, asili ya kuzaa, chakula cha afya na kitamu kinachoweza kufikiwa, maisha ya jamii, umbali kutoka kwa vituo vikubwa vya mijini.
Ingawa ili kuwa sehemu ya ukanda wa samawati lazima uwe umezaliwa ndani yake na uwe mwanachama hai wa jumuiya hiyo, kuna uwezekano kwamba baadhi ya mifumo hii inayojirudia inaweza kuwa ya manufaa kwa wale wanaopenda kuishi maisha marefu na bora.
Usiwe Mpweke
Zaidi ya vikwazo vya kiuchumi au mpango wako wa chembe za urithi, baadhi ya mambo ambayo hayajazingatiwa sana, wataalam wanasema, ni jinsi ya kuwasiliana na watu wengine na kupata kusudi maishani.
Hii, ambayo inaweza kuonekana rahisi, ni moja ya changamoto kubwa kwa wale ambao wana nia ya kuwa na ubora wa maisha kwa muda mrefu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wataalamu kama vile Luigi Ferrucci, mkurugenzi wa kisayansi wa Taasisi ya Kitaifa ya Kuzeeka, wanasema kwamba watu wazima wenye afya bora huwa na shughuli za kimwili, hutumia wakati nje na wana uhusiano mkubwa na marafiki na familia.
Ambapo wataalam hawajaweza kukubaliana ni juu ya ni kwa kiasi gani gvinasaba vya mtu na mtindo wa maisha huathiri maisha marefu.
Utafiti fulani unapendekeza kwamba chembe za urithi huchangia takriban 25% ya maisha marefu, huku nyinginezo zinahusiana na mambo kama vile mahali ambapo mtu anaishi, kile anachokula, mara ngapi anafanya mazoezi, na mfumo wake wa usaidizi kupitia marafiki au familia.
Walakini, uzito wa bahati nasibu ya maumbile katika maisha marefu na yenye afya bado ni suala la mjadala katika jamii ya kisayansi.












