'Mke wangu alinibaka kwa miaka kumi'

Visa vingi kuhusu unyanyasaji wa majumbani vinahusisha wanawake kama waathiriwa. Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban asilimia 33 ya wanawake duniani hupitia ukatili wa kimwili na kingono wakati fulani wa maisha yao.

Ukatili wa majumbani dhidi ya wanaume ni jambo lisilo semwa sana katika jamii nyingi. Waathiriwa hujikuta wanakabiliana na shida hiyo peke yao.

Lakini mwanaume mmoja kutoka Ukraine, amezungumza na BBC kuhusu ukatili alioupitia katika ndoa yake. Simulizi ifuatayo ni ya maneno ya mtu huyo:

Mara ya kwanza

Sijui kama marafiki zangu waliwahi kutilia shaka. Kila kitu kilionekana kiko vizuri kutokea nje. Vicheko, marafiki, pesa nyingi, furaha, yote yalikuwepo. Tulisafiri nusu ya ulimwengu pamoja.

Sikuwa na haja ya kumuogopa wakati wa kusafiri. Hakunitenda vibaya mbele ya macho ya watu.

Lakini hivi karibuni niligundua kuwa mke wangu wa zamani alikuwa akinibaka kwa miaka kumi. Ira alikuwa mpenzi wangu wa kwanza. Tulikutana tukiwa na miaka 20.

Wazazi wangu waliniambia hapo awali kwamba ukianza kuchumbiana na mtu, hamia nyumba nyingine. Hiyo inamaanisha, ikiwa ninataka uhusiano naye, lazima niondoke katika nyumba ya familia yangu.

Baada ya kupata pesa za kutosha ndipo nilipoweza kuingia kwenye uhusiano.

Ndipo pia nilifanya ngono na Ira kwa mara ya kwanza. Tulipofanya ngono mara ya kwanza, mchakato mzima ulichukua saa tano. Ingawa nilikuwa na maumivu wakati huo na baadaye.

Alikuwa na hamu ya kuona manii yakitoka. Alikuwa akinisugua - kwa wastani, hii inachukua saa moja hadi saa mbili. Baada ya siku chache nilianza kusema 'hapana'. Lakini, hakuacha. Hapo ndipo ikawa ubakaji.

Hotelini

Nikapata safari ya nje ya nchi kikazi. Kwa kuogopa kumpoteza Ira, nilimwomba aende nami. Kwa kuwa kazi ni ngumu, nilihitaji kupumzika – lakini yeye anataka ngono.

Nilikuwa nikisema kwamba ninahitaji kupumzika. Lakini angenipiga. Mimi sikumfanya chochote. Nilikuwa nikivumilia, nikidhani ni makosa kumpiga mwanamke. Mama na baba walinilea hivyo.

Nilikuwa najihisi dhaifu. Sikuweza kuikimbia hali hiyo. Nilionewa. Baada ya kazi, nilikuwa na hofu kurudi hotelini. Kwa hiyo nilikuwa nikienda kwenye maduka na kukaa huko hadi yanapofungwa. Baada ya hapo nilikuwa nikizurara katika mji.

Niliishi maisha ya kufanya chochote Ira alichotaka. Hali ilikuwa mbaya zaidi siku za wikendi.

Ndani ya Ndoa

Mwanzoni nilifanya majaribio mengi ili kumuacha. Hatimaye nilikata tamaa. Alilazimisha tufunge ndoa. Ingawa sikuipenda, tulifunga ndoa.

Ira alikuwa na wivu kwa kila mtu. Hata kwa marafiki na familia yangu. Hupiga simu popote nilipo. Huuliza nimekwenda wapi na kwa kwanini. Siku zote ilibidi nipatikane.

Lakini yeye alikwenda popote bila mimi. Mimi ni kama mdori wa kumfurahisha yeye wakati wote. Ira hana kazi. Mimi ndiye ninayepata pesa.

Yeye akipika, akisafisha nyumba. Tulikodi nyumba kubwa yenye bafu mbili. Aliamua kwamba tunapaswa kulala katika vyumba tofauti.

Ikiwa nitafanya kitu kibaya, angenifokea na kunipiga. Haya yalikuwa yakitokea kila baada ya siku kadhaa. Haijalishi ni nini kilitokea, lakini daima mimi ndiye mkosa.

Nakumbuka nikitoka peke yangu na kulia ndani ya gari. Hunifuata na kunitazama. Niliporudi nyumbani, nilijihurumia. Lakini, hilo halikumzuia kurudia kufanya atakavyo.

Kila siku maisha yakawa ni hayo. Haijalishi nilipata mateso kiasi gani, hakuna kitu kilibadilika. Ili kuepuka haya yote, nilikuwa nikitumia saa 10-14 kila siku ofisini. Nilikuwa nikienda kazini wikendi na likizo pia. Watu wengine hutumia dawa ili kuondosha mawazo. Watu kama mimi hufanya kazi katika ofisi.

Kuishi kwa ajili ya Mtu

Kwa wale ambao wako katika hali kama yangu. Huwa hatuoni njia ya kutokea. Hatufikirii kwamba kuna uwezekano wa kutoka na tunaweza kuwa na furaha tena.

Pia tunafanya mambo tusiyoyapenda. Tunafanya vitu kwa ajili ya watu. Mimi sikuishi kwa ajili yangu, niliishi kwa ajili yake. Nilifikiri kwamba nilipaswa kujitolea kwa mahusiano haya yote.

Kwa miaka mitatu au minne ya mwisho ya uhusiano wetu, nilikuwa na hofu ya ngono. Wakati wowote Ira akinilazimisha, nilikuwa napata hofu kubwa.

Nilikuwa nikirudi nyuma kwa woga. Kujificha. Nilikuwa nikiikimbia nyumba au kutoka kwenye chumba hicho.

Ira alikuwa akifikiri kwamba tulikuwa na matatizo katika ngono kwa sababu yangu. Mara kwa mara akinipeleka kwa mtaalamu wa ngono. Nikisema sipendi kitu anafikiri sipendi ngono. Nilinyamaza kimya kuhusu unyanyasaji na ubakaji niliokumbana nao.

Nilitokaje?

Yalikuwa ni majira ya baridi. Nilikuwa kitandani kwa wiki mbili kwa sababu ya homa. Ndipo nilipogundua kwamba maisha yangu hayakuwa na thamani na hakuna mtu ambaye anajali ikiwa ningefia huko.

Nilipokuwa katika mtandao, niliweka mjadala. Hakuna anayejua maelezo ya mwenzie hapo. Kila kitu ni siri. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kumwambia mtu kilichokuwa kikiendelea kwangu.

‘Kwanza acha kukaa kimya kwenye mambo kama hayo na anza kusema hapana'. Tangu wakati huo nilianza kusema 'hapana' zaidi na zaidi.

Baada ya hapo nilikwenda kwa mtaalamu wa ushauri. Mimi na Iran tulianza kuzungumza katika vikao hivyo. Hakuweza kuingilia ninapozungumza katika vikao. Niliweza kuzungumza unyanyasaji ninao pitia.

Alikuwa na hasira na mimi. Alisema mimi ni mwongo. Lakini, baada ya hapo aliomba talaka. Sidhani kama alifanya hivyo kwa sababu aliipenda. Alifanya hivyo ili kunifanya nishindwe kusema. Nilijua hiyo ni nafasi pekee. Ndiyo maana nilikubali.

Karatasi za talaka zilinijia baada ya mwezi mmoja. Hiyo ilikuwa siku ya furaha zaidi maishani mwangu.

Nilirudi kwa wazazi wangu. Niliacha kazi na kukaa nyumbani kwa wiki kadhaa. Kuogopa kwamba anaweza kuwa nje mahali fulani na kunitazama.

Siku nyingine alirudi. Mlango wangu ulianza kugongwa kwa teke. Alipiga kelele kutoka nje.

Haukuwa Mwisho

Ilibidi niwaambie wazazi wangu. Lakini, tangu utotoni nimekuwa na tabia ya kuficha mambo. Sikujua hata jinsi ya kuwaambia marafiki zangu juu ya kile kilichokuwa kinanipata.

Hakuna vikundi vyovyote vinavyoweza kukusaidia. Huku Ukraine kuna vikundi tu kwa wanawake. Nilipata kikundi kutoka San Francisco kwenye mtandao.

Hata kama nataka kwenda mahakamani dhidi yake. Wanasheria walisema kuna uwezekano wa hilo. Lakini, sihitaji kufanya hivyo nataka tu akubali makosa yake na kuomba msamaha.

Bado siendi kazini. Sasa sijui ninaishi kwa malengo gani. Sijafanya chochote ndani ya mwaka. Najua kuwa sitaingia kwenye uhusiano tena na sitapata watoto. Nimekata tamaa kabisa.

Maisha yangu yaliharibika kwa sababu nilikaa kimya kwa muda mrefu. Mtu aliye katika hali kama yangu anaweza kuwa mahali fulani sasa. Unaweza kusoma hadithi yangu.

Kwa nini waathiriwa huficha?

Alyona Krivulyak, mshauri wa Population Fund ya Umoja wa Mataifa anasema mambo haya:

Watu wanaokulia katika familia zilizo na unyanyasaji wa nyumbani wana uwezekano mkubwa wa kuishi kama wazazi wao. Wanaogopa kuwa wapweke na nani atawajali. Watu wa karibu watawafikiria nini? Watoto wanahitaji mama na baba.

Katika hatua za kwanza kuna unyanyasaji wa kisaikolojia. Ni vigumu kuufahamu. Waathiriwa wanazoea unyanyasaji huo polepole. Wanapoteza uwezo wao wa kutathmini na kugundua hali zao.

Waathiriwa wanaweza kukosa namna ya kuwaacha wanyanyasaji wao. Pengine wanawategemea kifedha. Kwa mfano, wale ambao ni wajawazito na walio na watoto wadogo wanaweza kuogopa kwamba watapata shida ikiwa wataachana na wenzi wao.

Hata kama wanalalamika, wanaweza kukutana na jibu kwamba 'haya yote ni matatizo ya familia'. Matumaini yao yanaweza kupotea.

Wanaume ambao ni waathiriwa wa kesi kama unyanyasaji wa nyumbani hawataki siri za zitoke. Na husitasita kufika mahakamani.

Yulia Klimenko, mtaalamu wa magonjwa ya akili, anasema kuwa jamii inawazuia wanaume kueleza matatizo hayo kwa hoja kuwa ‘mwanaume hapaswi kulia' au 'wanaume wana nguvu kimwili'.