Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tundu Lissu atangaza kuishtaki Tigo, serikali ya Tanzania
- Author, Florian Kaijage na Sammy Awami
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Tanzania
- Author, Sammy Awami
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Makamu Mwenyekiti wa chama cha upinzani Chadema nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema amemuelekeza mwanasheria wake Bob Amsterdam kuanza taratibu za kuishtaki kampuni ya Millicom ambayo ilikuwa kampuni mama ya simu za mkononi ya Tigo kwa pamoja na serikali ya Tanzania kwa tuhuma za kuhusika na jaribio la kutoa uhai wake.
Lissu ameyasema hayo baada ya mahakama moja nchini Uingereza kuelezwa kuwa kampuni ya mawasiliano ya Tigo (ambayo ilikuwa ikimilikiwa kwa wakati huo na Millicom) ilitoa taarifa za mawasiliano na nyendo za mwanasiasa huyo kwa saa 24 siku chache kabla ya tukio la kushambuliwa kwake.
Septemba 7, 2017 Lissu alishambuliwa kwa risasi zipatazo 16 aliporeja kutoka kwenye kikao cha Bunge, akiwa katika uwanja wa makazi yake na viongozi wengine eneo la Area D, jijini Dodoma, na baadaye kufanyiwa upasuaji mara 25 nchini Kenya na Ubelgiji.
Wakati huo Tundu Lissu alikuwa mbunge wa Singida Mashariki mkoni Singida, katikati mwa Tanzania kupitia Chadema.
Hata hivyo, amesema hajui tarehe rasmi ya kuanza kwa kesi hiyo kwani mawakili wake wanahitaji kukusanya ushahidi wa kutosha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jioni hii, Lissu ameeleza kwanini hakuwahi kufungua kesi dhidi ya Millicom.
"Sikwenda mahakamani kwasababu sikuwa na ushahidi wa kutosha. Lakini sasa tunao ushahidi unaotosheleza kufungua kesi" amesema Lissu.
Ushahidi wa kuhusika kwa kampuni ya Millicom umekuja baada ya kesi iliyofunguliwa Mwaka 2019 dhidi ya kampuni hiyo nchini Uingereza na aliyekuwa mtumishi wa kampuni hiyo.Lissu amelilaumu jeshi la polisi kwa kutokufanya uchunguzi wa tukio aliloliita la kigaidi.
"Hadi leo sijaitwa na polisi kuulizwa niliona nini. Wakati mimi niliwaona vijana wawili. Mtumishi wangu wa ndani aliyepo Dodoma na mtumishi wa Tulia Ackson aliyempeleka kwenye gari" alisema Lissu aliyedai anaamini polisi hawajawahi hata kufungua jalada.
Mwanasiasa huyu amesema tukio hilo limeacha hofu kwa watoto wake na mke wake ambao amesema wameshindwa kurudi nchini Tanzania kwa takribani miaka mitano sasa.
Kadhalika amemtuhumu Mkuu wa mkoa wa Arusha wa sasa, Paul Makonda kuratibu mpango wa kutaka kumuua kwa sababu ya kuipinga serikali ya Rais wa wakati huo, John Magufuli, wakati huo Makonda akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Hata hivyo Lissu hakutoa ushahidi wa Makonda kuhusika huku akidai tu Makonda alikuwa jijini Dodoma wakati wa tukio hilo la jaribio la mauaji dhdi ya mwanasiasa huyo.
Jitihada za BBC kumpata msemaji wa Serikali ya Tanzania, Thobias Makoba ama msemaji wa Jeshi la polisi, David Misime hazikufanikiwa kwani hawakupokea simu zao wala kujibu ujumbe wa BBC.