José Eduardo dos Santos: Aliyeongoza mipango ya kuleta amani licha ya dosari zake

José Eduardo dos Santos alikabidhi madaraka mwaka wa 2017 baada ya miaka 38 kama rais.

Chanzo cha picha, Reuters

José Eduardo dos Santos, rais wa pili wa Angola ambaye alitawala taifa hilo lenye utajiri wa madini kwa takriban miongo minne, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79, serikali inasema.

Alifariki nchini Uhispania ambako alipatiwa matibabu baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo. Dos Santos atakumbukwa kwa kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda mrefu mwanzoni mwa miaka ya 2000 - wafuasi wake walimwita "mbunifu wa amani".

Lakini urithi wake umechafuliwa na viwango vya juu vya ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu alipokuwa madarakani.

Akiwa amehitimu katika uhandisi wa petroli katika Umoja wa Kisovieti mwaka wa 1969, Dos Santos alikuwa na umri wa miaka 37 tu alipokuwa rais wa Angola muongo mmoja baadaye, kufuatia kifo cha rais wa kwanza, António Agostinho Neto.

Wakati huo, miaka minne tu baada ya kupata uhuru mwaka 1975, nchi hiyo ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya makundi mawili yaliyokuwa yakipigania ukoloni wa Ureno - MPLA ya Dos Santos na Unita.

Vita hivyo vilidumu kwa miaka 27 na kuangamiza nchi. Takriban watu 500,000 wanaaminika kufariki katika mzozo huo.

Pia ilivutia mataifa ya kigeni, huku Afrika Kusini - wakati huo ikiwa chini ya utawala wa wazungu wachache - kutuma wanajeshi kuunga mkono Unita, wakati vikosi vya Cuba viliingilia kati upande wa serikali.

Dos Santos na kiongozi wa Unita Jonas Savimbi (kulia), walioonekana hapa mwaka 1995, walisifiwa kwa hatua zao za kuelekea amani.

Chanzo cha picha, AFP

Dos Santos aliongoza nchi ya chama kimoja lenye mwelekeo wa Umaksi hadi kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti na mwisho wa Vita Baridi vilisabaisha MPLA na Unita kutia saini makubaliano ya amani.

Ilishuhudia Dos Santos na Jonas Savimbi wa Unita wakikabiliana katika chaguzi za kwanza za vyama vingi nchini Angola tangu uhuru.

Dos Santos alimshinda Savimbi kwa tofauti ndogo, na kusababisha duru ya pili kuitishwa, lakini Savimbi aliigomea, na kuchagua kuchukua tena silaha.

Zaidi ya muongo mmoja baadaye, Februari 2002, wanajeshi wa Dos Santos walimuua Savimbi na makubaliano ya amani baadaye yakajadiliwa na uongozi mpya wa Unita.

"Hakuna risasi moja zaidi, tunapaswa kuwahifadhi watu hai na kujadili amani," Dos Santos alisema wakati huo, alipokuwa karibu kutangaza rasmi mwisho wa vita. Kwa hivyo, nchi mpya ilizaliwa. Kujenga upya na maridhiano yalikuwa malengo makuu ya Dos Santos.

Wakati huo, alifurahia umaarufu mkubwa, kama ilivyooneshwa na ushindi wa MPLA katika uchaguzi wa 2008 na 82% ya kura.

th

Upendeleo kwa familia

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, katika miaka iliyofuata, shutuma za ufisadi wa hali ya juu, hasa katika sekta ya mafuta, usimamizi mbovu wa uchumi na kukandamiza upinzani wa kisiasa ulitawala utawala wake.

Dos Santos, ambaye alipata sifa ya kuwa rais asiye na hisia, alisema machache sana juu ya mambo haya hadharani, huku hali ya kutoridhika na utawala wake kulikua.

Ilisababisha kuongezeka kwa usalama wake wa kibinafsi na wa familia. Katika moja ya mahojiano yake ya nadra ya kwenye televisheni, mwaka 2013, Dos Santos aliiambia idhaa ya Kireno ya SIC kwamba Angola ilikuwa imara kabisa, na kwamba makundi yanayopinga utawala wake yalikuwa madogo sana na "yanatambulika vyema".

Kufikia wakati huo, upendeleo ulikuwa tayari umeenea. Aliteua wanafamilia na marafiki wa karibu katika nyadhifa kubwa serikalini, akiwemo mwanawe José Filomeno dos Santos, anayejulikana pia kama Zenu, kama mkuu wa Mfuko wa Fedha wa Angola, na baadaye, binti yake Isabel dos Santos kama mkuu wa kampuni ya mafuta ya Sonangol.

Alisemekana kuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika. Kwa kuongezeka, ilionekana kana kwamba Angola ilikuwa inageuka kuwa ya udikteta, huku wanasiasa wa upinzani, wanaharakati wa haki za kiraia na waandishi wa habari wakiteswa na hata kuuawa.

Mojawapo ya kesi ambazo zilijulikana sana duniani kote, na kwa hakika kuathiri urithi wa Dos Santos, ilikuwa ni kukamatwa kwa wanaharakati 17 ambao walituhumiwa kwa "uhalifu wa uasi" na kupanga njama ya mapinduzi.

Dos Santos alidhani Joao Lourenço (Kulia) asingemtikisa

Chanzo cha picha, AFP

Mnamo 2017, miaka 38 baada ya kula kiapo cha kwanza, Dos Santos aliwashangaza Waangola wengi kwa kujiuzulu.

Alimchagua Waziri wake wa zamani wa Ulinzi, João Lourenço, kuwa mrithi wake.

Mwaka mmoja baadaye, Dos Santos pia alijiuzulu kama kiongozi wa MPLA.

Katika hotuba yake ya mwisho kwa chama, alikiri kuwa alifanya makosa katika kipindi kirefu alichokuwa madarakani.

"Makosa ni sehemu muhimu ya mchakato wa kuboresha, kwa hivyo inasemekana tunajifunza kutokana na makosa," aliuambia umati. Dos Santos pia alisema aliondoka madarakani akiwa ameinua kichwa chake - na alipewa cheo cha "rais mstaafu" na chama chake. Lakini msimamo wake ulikuwa dhaifu.

Kufungwa kwa mtoto wake

Akiwa amedhamiria kupambana na ufisadi nchini Angola, Bw Lourenço aliyechaguliwa hivi karibuni alimgeukia kiongozi wake wa zamani na kumlenga Dos Santos - sio moja kwa moja, bali kupitia watoto wake.

Mwanawe Zenu, kwa mfano, alifungwa jela miaka mitano kwa ulaghai baada ya $500m (£378m) kuhamishwa kutoka benki ya kitaifa ya Angola hadi akaunti nchini Uingereza.

Binti yake, Isabel, amepigwa marufuku kuingia Marekani kwa "kuhusika katika ufisadi mkubwa", kulingana na idara ya serikali ya Marekani.

Mnamo 2020, BBC iliripoti kuhusu nyaraka zilizofichuliwa ambazo zilifichua jinsi alivyojitajirisha kupitia madai ya kuinyonya nchi yake kwa ufisadi.

Wakati huo, Bi Dos Santos alisema madai dhidi yake ni ya uongo kabisa na kwamba kulikuwa na uwindaji uliochochewa kisiasa na serikali ya Angola.

Dos Santos

Chanzo cha picha, Getty Images

Mara tu baada ya kuondoka madarakani, Dos Santos alienda uhamishoni huko Barcelona, ​​Uhispania, ambako aliripotiwa kutibiwa kwa muda mrefu hali ya afya ambayo haikuwahi kuthibitishwa rasmi na wanafamilia wake, licha ya kuripotiwa kwa vyombo vya habari vya Angola kwa miaka mingi.

Alizuru Angola mara ya mwisho mnamo Septemba 2021, ambapo alikaa hadi mwanzoni mwa mwaka 2022. Wakati akiwa nchini humo, alikutana na Rais Lourenço mara mbili katika makazi yake rasmi.

Hatahivyo, mikutano hii haikuleta ahueni yoyote kwa nasaba ya Dos Santos, wala kufuta doa kwenye urithi wake. Kwa kuleta amani nchini Angola angeweza kukumbukwa kama shujaa wa taifa, lakini muda wake mrefu madarakani, hatua za uonevu alizoanzisha na ufisadi chini ya ulinzi wake uliharibu sifa hiyo.