Al-Shabab: Vifo kwenye Shambulio katika hoteli nchini Somalia vyafikia 12- ripoti

Maafisa wa usalama wanasema watu 12 wameuawa baada ya wanamgambo wa al-Shabab kuvamia hoteli moja katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Polisi walisema washambuliaji walilipua vilipuzi viwili nje ya hoteli hiyo kabla ya kuingia ndani ya jengo hilo na kufyatua risasi.

Wanaripotiwa kujufungia kwenye ghorofa ya juu ya Hoteli ya Hayat, saa chache baada ya mashambulizi kuanza.

Kitengo maalum cha polisi kinasemekana kuwaokoa makumi ya wageni na wafanyikazi kutoka hoteli hiyo.

"Vikosi vya usalama viliendelea kuwadhibiti magaidi ambao wamezingirwa ndani ya chumba katika jengo la hoteli. Wengi wa watu waliokolewa, lakini takriban raia wanane walithibitishwa kufariki kufikia sasa," alisema afisa mmoja, Mohamed Abdikadir.

Hapo awali, tovuti yenye uhusiano na al-Shabab ilisema kundi la wanamgambo "wameingia kwa nguvu" katika hoteli hiyo na walikuwa "wakifanya ufyatuaji risasi kiholela".

Hayat inaelezewa kama eneo maarufu kwa wafanyikazi wa serikali kuu ambao hufanya mikutano huko

Watu tisa walijeruhiwa na kubebwa hadi nje ya hoteli hiyo, mkuu wa huduma za ambulansi , Aamin mjini Mogadishu, Abdikadir Abdirahman aliliambia shirika la habari la Reuters hapo awali.

Picha ambazo hazijathibitishwa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionekana kuonyesha moshi ukifuka kutoka hotelini huku kelele na kishindo kikubwa kikisikika.

"Magari mawili ya mabomu yalilenga Hotel ya Hayat," afisa wa polisi aliambia shirika la habari la Reuters katika taarifa. "Moja liligonga kizuizi karibu na hoteli, na kisha jingine likakagonga lango la hoteli. Tunaamini wapiganaji wako ndani ya hoteli."

Washirika wa al-Qaeda, al-Shabab wamehusika katika mzozo wa muda mrefu na serikali ya kuu ya Somalia .

Kundi hilo linadhibiti sehemu kubwa ya kusini na kati mwa Somalia lakini limeweza kueneza ushawishi wake katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali yenye makao yake makuu mjini Mogadishu.

Katika wiki za hivi majuzi wapiganaji wenye mfungamano na kundi hilo pia wameshambulia maeneo kwenye mpaka wa Somalia na Ethiopia, jambo ambalo limezua wasiwasi kuhusu uwezekano wa mkakati mpya wa al-Shabab.

Shambulio hilo la Ijumaa ni la kwanza kufanywa na kundi hilo katika mji mkuu tangu rais mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, kuchaguliwa mwezi Mei.