Prigozhin azikwa kando ya baba yake katika mazishi ya kibinafsi, bila heshima za kijeshi

Chanzo cha picha, Shutterstock
Mkuu wa Kikundi cha Wagner, Yevgeny Prigozhin, alizikwa katika ibada ya mazishi ya kibinafsi huko St. Petersburg, kulingana na ofisi yake ya waandishi wa habari.
Aliongeza kuwa mazishi yaliyofanyika katika jiji lake, yalifanyika "kwa siri", na wale wote waliotaka kumuaga walitakiwa kutembelea makaburi ya "Porokhovskoye".
Hapo awali, maafisa wa Urusi walithibitisha kifo cha mkuu wa kundi hilo baada ya kufanya uchambuzi wa vinasaba wa miili kumi iliyopatikana kwenye ndege iliyoanguka mnamo Agosti 23 karibu na Moscow, na Kremlin ilikanusha "uvumi" ulioibuka kuwa ndiyo iliosababisha ajali hiyo.
Lakini idadi kadhaa ya waangalizi wa Urusi, ndani na nje ya nchi, wamemuelezea Prigozhin, 62, kama "mtu aliyekufa akitembea" tangu "uasi" aliouongoza dhidi ya Urusi mwezi Juni mwaka jana.
Katika uchambuzi wa Steve Rosenberg, mhariri wa BBC wa Huduma ya Kirusi, anasema kwamba Yevgeny Prigozhin alikuwa mtu wa siri, mara nyingi alificha utambulisho wake kwa kuvaa wigi na ndevu bandia.
Na anasema: Mitaa ya St. Petersburg ilijaa uvumi juu ya mahali pa kuzikwa kiongozi wa kikundi hicho.
Hakuna tangazo rasmi lililotolewa kuhusu wakati na mahali ambapo mazishi yangefanyika, hata kwenye mitandao ya kijamii. Angalau makaburi manne tofauti yalizungumziwa kama uwezekano wa mahali pa kuzikwa, na mwishowe alizikwa kwenye kaburi. Hakuna anayejua.
"Mwishoni, wawakilishi wa Prigozhin walisema kwamba mkuu wa Wagner alikuwa amezikwa kwenye Makaburi ya Porokhovsky nje kidogo ya St. Petersburg karibu na marehemu baba yake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hakukuwa na heshima za kijeshi kwa mkuu huyo wa Wagner na inasemekana watu wachache walihudhuria."
"Tuliambiwa nje ya kaburi hilo lilikuwa limefungwa rasmi kwa siku hiyo, kwa hivyo hatukuweza kuingia," anasema Rosenberg.
"Kulikuwa na mistari mirefu ya polisi kando ya uzio wa mzunguko na katika eneo lote la makaburi, pamoja na mbwa kadhaa wa kunusa, maafisa wa ndege zisizo na rubani na polisi wa kutuliza ghasia".
Kwa upande wake, Kremlin ilizingatia Uasi wa Wagner, ulioandaliwa na Prigozhin kuwa "uhaini".
Na tovuti ya Kirusi "MSK1" ilinukuu maafisa wa makaburi wakisema kwamba mazishi yalifanyika mnamo 13:00 GMT Jumanne, na maafisa walisema: "Hivi ndivyo jamaa wa Prigozhin walivyotaka."
Tovuti hiyo pia ilisema kwamba Prigozhin alizikwa karibu na kaburi la baba yake, na kuongeza kuwa bendera nyeusi, njano na nyekundu ya Wagner iliwekwa kwenye tovuti ya kundi hilo.
Shirika la habari la Fontanka la Saint Petersburg liliripoti kwamba vizuizi vya chuma viliwekwa kwenye lango, kwani inaaminika kuwa viongozi wanajiandaa kufanya "hija kubwa" kwenye kaburi la Prigozhin.

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa upande mwingine, mazishi ya Valery Chekalov, naibu wa kwanza wa Prigozhin, ambaye pia alikuwa ndani ya ndege iliyoanguka, yalifanyika Jumanne kwenye makaburi ya Severno huko St. Petersburg.
Mtu huyo mwenye umri wa miaka 47 anaaminika kuendesha biashara ya Prigozhin isiyo ya kijeshi,
ambayo serikali za Magharibi zinasema inatumika kufadhili kundi hilo.
Mapema siku hiyo, msemaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin, Dmitry Peskov, alisema kiongozi wa Kremlin hatahudhuria mazishi ya Prigozhin, ingawa wapiganaji wa Wagner walikuwa na jukumu muhimu katika uvamizi wa Urusi huko Ukraine mwezi Februari 2022.
Putin alikaa kimya kwa karibu saa 24 baada ya ajali hiyo, na siku iliyofuata alituma rambirambi kwa familia za waathiriwa wote, akielezea Prigozhin kama "mtu mwenye talanta" ambaye "alifanya makosa makubwa maishani."
Mnamo mwezi Juni, Prigozhin, mtu mwaminifu wa wakati mmoja wa Putin, aliongoza "maasi" dhidi ya majenerali wawili wakuu wa vikosi vya jeshi la Urusi.
Kundi lake lilichukua udhibiti wa jiji la "Rostov-on-Don" kusini mwa Urusi, na walikuwa wakiandamana kuelekea Moscow, na hawakuzuia "uasi" huo hadi kilomita 200 (maili 125) kutoka mji mkuu.
Putin alitaja mapinduzi ya wakati huo kama "uhaini" na "kuchomwa kisu mgongoni", lakini makubaliano yalifikiwa baadaye kwa wapiganaji wa Wagner kujiunga na vitengo vya jeshi la kawaida la Urusi au kuhamia Belarus, mshirika wa Urusi.
Hata hivyo, kumekuwa na uvumi kwamba vikosi vya usalama vya Urusi vilihusika kwa namna fulani katika ajali hiyo ya ndege.
CBS, mshirika wa BBC katika vyombo vya habari nchini Marekani, alinukuu maafisa wa Marekani wakisema uwezekano mkubwa wa kusababisha ajali hiyo ni mlipuko uliotokea kwenye ndege hiyo ya kibinafsi.
.












