'Najihisi kama malaika wa kifo': Afisa anayefahamisha familia za Waisraeli kwamba jamaa wao amekufa

Rafael akizungum

Chanzo cha picha, Handout

Maelezo ya picha, Rafael ameishi nchini Israel kwa miaka 20 na amehudumu jeshini tangu 2009
    • Author, Julia Braun
    • Nafasi, BBC World Service
    • Akiripoti kutoka, São Paulo

Familia ya Waisraeli wote wanaokufa katika operesheni za kijeshi au katika mashambulizi yanayotajwa kuwa ya kigaidi na serikali yao hupokea usaidizi maalum, unaojumuisha kutembelewa na afisa wa jeshi ili kutoa taarifa rasmi kuhusu kifo hicho.

Lakini tangu uvamizi wa Hamas uliposababisha vifo vya zaidi ya watu 1,400 nchini humo, huduma hizi zimekuwa zikizidiwa kuliko hapo awali. Kama matokeo, maafisa kutoka Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) ambao kwa kawaida hawafanyi kazi na familia za waathiriwa waliitwa kwa kazi hii.

Rafael*, ambaye anatoka Brazil, ni mkuu wa jeshi na alikuwa mmoja wa wale walioitwa. Tangu Ijumaa iliyopita (13 Oktoba), amekuwa akitembelea walau familia tatu kwa siku kuleta habari kuhusu kifo cha mpendwa.

"Ninapobisha kwenye milango ya familia hizi, ninahisi kama malaika wa kifo," aliambia BBC.

"Lakini najua kuwa kazi hii ni muhimu sana, kwani inatoa fursa kwa familia kuwa na uhakika juu ya kile kilichotokea kwa mpendwa wao na kuweza kuzika."

Hii ni mara ya kwanza Rafael anatekeleza jukumu hili. Baada ya kuhudumu katika

Akiwa katika jeshi la Israeli kwa miaka 14, Mbrazil huyo kutoka Rio de Janeiro kwa kawaida anafanya kazi katika masuala ya kisheria na IDF.

"Kuna watu katika jeshi ambao hufanya jukumu hili mara kwa mara, lakini idadi ya vifo ilifikia kiwango kikubwa, idadi ya maofisa waliopewa mafunzo ya aina hii haikutosha," anasema.

Mwanajeshi huyo anasema alipitia mafunzo ya saa nne kabla ya kuanza kazi hiyo. “Katika maandalizi yetu walisema, hasa katika siku za kwanza, tunaweza kuyumba sana, kupoteza hamu ya kula na kushindwa kulala,” anasema. "Na hiyo inafanyika - ni vigumu kulala na kula."

"Lakini kwa kweli naendelea kula chakula na kujaribu kulala, kwa sababu najua kuwa nisipofanya hivi kutakuwa na familia moja, mbili, tatu, nne, tano zaidi ambazo hazitapokea habari kuhusu jamaa zao."

Magari yaliyochomwa na kuharibiwa karibu na tamasha la muziki lililoshambuliwa na Hamas

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Magari yaliyochomwa na kuharibiwa karibu na tamasha la muziki lililoshambuliwa na Hamas
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Rafael anasema kwamba baadhi ya ziara ambazo zilikuwa na athari kubwa kwake ni za kufika katika nyumba za familia zenye watoto na vijana.

Katika moja wapo ya ziara hizo, ilimbidi kutoa habari za kifo cha msichana wa miaka 17 kwa baba yake. Alikuwa na mpenzi wake kwenye ufuo karibu na Ukanda wa Gaza wakati wanandoa hao waliposhambuliwa na Hamas.

"Tulipomjulisha baba huyu habari, alisema kuwa siku moja kabla alimuona bintiye kwenye runinga, miongoni mwa watu ambao pengine walitekwa nyara," Rafael anakumbuka.

"Alisema alikuwa na tumaini - ikiwa kuna mtu anaweza kutumaini mtoto kutekwa nyara - kwamba bado yuko hai."

Katika safari nyingine, aliwatembelea wazazi wa mwanamke mwenye umri wa miaka 30 ambaye aliuawa katika nyumba yake mwenyewe. Mume wake hayupo.

“Waliwaacha mapacha wawili wenye umri wa miezi 10 ambao walinusurika tu kwa sababu wazazi wao walifanikiwa kuwaweka ndani ya kizimba na kufunga chumba kabla ya magaidi hao kufika,” asema.

"Imekuwa ngumu sana; kila wakati nafikiria kuhusu familia. Ni wazazi ambao hawatawaona tena watoto wao, ni watoto ambao watakua bila wazazi wao."

Meja Rafael akiwa na sare za kazi

Chanzo cha picha, Handout

Maelezo ya picha, "Ni vigumu kulala," Rafael anasema

Kulingana na Rafael, familia nyingi za waathiriwa wa shambulio la Oktoba 7 watalazimika kusubiri kwa muda kabla ya kupokea habari kuhusu wapendwa wao.

“Kuitambua miili hiyo ni ngumu, kwani baadhi yao hawatambuliki kabisa, matokeo ya uthibitisho wa vifo unachukua muda kufika,” anasema.

"Kuna zaidi ya watu 600 wamepotea na wengi wao, kwa bahati mbaya, wamekufa, lakini utambuzi wa miili bado haujawezekana."

Uvamizi wa tarehe 7 Oktoba unachukuliwa kuwa shambulio kubwa zaidi ambalo Israeli imekabiliana nayo katika istoria yake.

Wapiganajia wa Hamas walivunja uzio unaotenganisha Gaza na Israel katika maeneo mbalimbali, kuvamia vijiji na kuua takriban watu 1,400. Inakadiriwa kuwa karibu watu 200 walitekwa nyara.

Wapiganaji pia walirusha maelfu ya makombora kutoka Ukanda wa Gaza, ambayo baadhi yalipiga miji ya mbali kama Tel Aviv na Jerusalem.

Nyumba iliyochomwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nyumba iliyochomwa moto huko Kibbutz Be'eri, karibu na Ukanda wa Gaza, baada ya shambulio la Hamas.

Kama hatua ya kulipiza kisasi, Israel ilianzisha mfululizo wa mashambulizi ya anga dhidi ya Ukanda wa Gaza katika siku zilizofuata. Idadi ya waliofariki mjini Gaza kutokana na mashambulizi ya Israel ilifikia watu 2,700 siku ya Jumatatu (16 Oktoba).

Kwa mujibu wa mamlaka ya Palestina, karibu watu 1,000 wamepotea katika vifusi vya majengo yaliyolipuliwa.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, wanajeshi wa nchi hiyo pia walitangaza kuwa wanajiandaa kwa mashambulizi mapya dhidi ya Gaza ya nchi kavu, baharini na angani.

Israel imewaambia Wapalestina 1.1m wanaoishi kaskazini mwa Gaza kuhamia kusini ili kuepuka mashambulizi yanayotarajiwa.

Mgogoro wa kibinadamu katika ardhi ya Palestina unazidi kuwa mbaya na kuna hofu ya mzozo huo kusambaa na kuhusisha nchi zingine katika eneo hilo, kama vile Lebanon na Iran.

*BBC imebana jina la ukoo la mwanajeshi huyo kwa sababu za kiusalama.