Ndondi Zanzibar: Marufuku ya miaka 60 kuisha kupitia mechi

Chanzo cha picha, Azam Media
Mashabiki wa ndondi visiwani Zanzibar wanatarajiwa kufurahia pambano la kwanza katika takriban miongo sita siku ya Jumapili baada ya marufuku ya muda mrefu kuondolewa.
Marufuku ya miaka ya 1960 ilifuatia mapinduzi ya Rais wa kwanza wa kisiwa hicho Abedi Amani Karume, akitaja sababu za kitamaduni.
Tukio hilo linaendana na msukumo wa kimkakati wa Rais wa sasa Hussein Mwinyi wa kukuza utalii na maendeleo ya michezo.
Bondia wa Zanzibar, Hamis Muay Thai atamenyana na Ibrahim Mjender katika pambano la kihistoria la raundi nane lisilo la ubingwa wa uzito wa juu.
Hamis Muay Thai, ambaye alianza maisha yake ya mapigano kwa mafanikio mengi kama kickboxer, atakuwa akicheza kwa mara ya kwanza ulingoni akiwa bondia.
Kijana mwingine wa nyumbani Musa Nassor "Banja" pia atajimwaya uwanjani. Atapigana na Dullah Mbabe kutoka Bara, huku Karim Mandonga, bondia wa Tanzania mwenye mvuto akimenyana na Osman Muller Junior kutoka Zanzibar katika pambano jingine.
Kutakuwa na jumla ya mechi nane za ndondi kwa jumla.
Wakati mapinduzi ya Januari 1964 yalipomaliza utawala wa Sultani wa Zanzibar na serikali yake ya Waarabu walio wengi, watu wa karibu wa Rais wa wakati huo Karume wanasema waliuona mchezo wa ngumi kama "unyama" kwa hoja kwamba mapigano yalikuwa ya wanyama.
Marufuku hiyo, hata hivyo, haikuathiri Tanzania Bara.
Tanganyika na Zanzibar ziliungana mwezi Aprili 1964 na kuunda nchi ambayo sasa inaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Matokeo ya utafiti wa miezi sita uliofanywa mwaka 2021 yalionyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa Zanzibar waliunga mkono kurejeshwa kwa ndondi.

Chanzo cha picha, Azam Media
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bondia wa Tanzania, Karim Mandonga, amekuwa akionyesha mbwembwe zake kwenye ufukwe wa Bahari Hindi
Zanzibar inajaribu kufungua milango yake kwa dunia ili kuvutia wawekezaji na watalii kutoka nje ya nchi. Sera ya Rais wa sasa Mwinyi ya Uchumi wa Bluu inajumuisha msisitizo katika utalii na michezo.
Hivi karibuni bondia wa kike wa Uingereza Natasha Jones alitawazwa kuwa balozi wa heshima wa Zanzibar katika utalii wa michezo.
“Ni heshima kubwa na nitajitahidi kadri niwezavyo kwa wananchi wa Zanzibar ili niwawakilishe kwa njia nzuri lakini pia kukuza kila kitu ambacho tayari wanacho,” alisema Jones bondia bingwa.
Mabondia hao wote wamelipwa ada zao za kushiriki, ingawa hakutakuwa na zawadi yoyote.
Tukio hilo muhimu litafanyika katika Uwanja wa Mao Tse Tung siku ya Jumapili na litaonyeshwa moja kwa moja kwenye TV.
Halka Ahmed, mtayarishaji mchanga wa maudhui alisema amefurahishwa sana.
"Hii itawavutia vijana wenzangu ambao wanataka kweli kuwa mabondia wa kulipwa Zanzibar".
Wenyeji wengine wengi pia wanatarajia kufufua mchezo wa ngumi Zanzibar.
"Hii ni hatua ya kihistoria," alisema Sandaland Omari, mmiliki wa duka la michezo.












