Vita vya Ukraine: Wimbi la mashambulizi 'makubwa' yakumba miji mikubwa Ukraine ikiwemo Kyiv

Chanzo cha picha, EPA
Urusi imeanzisha mashambulizi makubwa ya makombora kote Ukraine, ukiwemo katika mji mkuu wa Kyiv, na kusababisha kukatika kwa umeme na maji, maafisa wa Ukraine wamesema.
Takriban milipuko miwili iliripotiwa huko Kyiv. Mkazi mmoja aliambia BBC kuwa wilaya yake sasa haina umeme.
Katika mji wa kaskazini-mashariki wa Kharkiv, vifaa muhimu vya miundombinu vilipigwa, viongozi wa eneo hilo walisema.
Mashambulizi hayo yanakuja baada ya Urusi kuilaumu Ukraine kwa shambulio la ndege isiyo na rubani dhidi ya meli zake katika Bahari Nyeusi katika eneo lililotawaliwa la Crimea.
Siku ya Jumatatu asubuhi, mashambulizi ya makombora pia yaliripotiwa katika eneo la kati la Vinnytsia, pamoja na Dnipropetrovsk na Zaporizhzhia kusini-mashariki, na Lviv magharibi mwa Ukraine.
Kituo cha kuzalisha umeme cha Dnipro katika eneo la Zaporizhzhia pia kiliripotiwa kuathirika.
Huko Kyiv, kituo ambacho kinasimamia vyumba 350,000 kiliharibiwa, na wahandisi walitumwa haraka kurejesha usambazaji.
Haikujulikana mara moja ikiwa kuna majeruhi.

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakaazi katika maeneo yanayoshambuliwa walihimizwa kusalia kwenye makazi, huku kukiwa na hofu kwamba huenda mashambulizi zaidi yakafuata.
Msemaji wa Jeshi la Wanahewa la Ukraine Yuriy Ihnat aliiambia TV ya Ukraine kwamba Urusi imetumia washambuliaji wake wa kimkakati kutekeleza mashambulizi yake "makubwa".
Idadi kubwa ya makombora ya Urusi yaliangushwa, maafisa wa Ukraine walisema.
Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya Rais Volodymyr Zelensky, alisema kuwa "Warusi walioshindwa wanaendelea kupigana dhidi ya vitu vya amani".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alisema kuwa "badala ya mapigano kwenye uwanja wa vita, Urusi inapambana na raia".
Wakati huo huo, balozi wa Marekani nchini Ukraine, Bridget Brink, alisema kupitia Twitter: "Kama mamilioni ya raia wa Ukraine, timu yetu ya @USEmbassyKyiv kwa mara nyingine inajificha huku Urusi ikiendelea na mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya watu wa Ukraine katika juhudi za kuiacha nchi hiyo baridi na giza tunapokaribia msimu wa baridi."

Chanzo cha picha, UKRAINE'S DIGITALISATION MINISTRY
Urusi hadi sasa haijatoa maoni yoyote kuhusu mashambulizi ya hivi punde yaliyoripotiwa.
Siku ya Jumamosi, meli moja ya kivita ya Urusi iliharibiwa katika mji wa bandari wa Sevastopol katika shambulio la ndege isiyo na rubani, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema. Pia ilishutumu wataalamu wa Uingereza kwa kuwafunza wanajeshi wa Ukraine ambao walifanya shambulizi huko Crimea - peninsula ya kusini mwa Ukraine, iliyotwaliwa na Urusi mnamo 2014.
Moscow haikutoa ushahidi wowote kuunga mkono madai yake.
Ukraine haijazungumzia suala hilo, huku wizara ya ulinzi ya Uingereza ikisema Urusi "inaendesha madai ya uwongo kwa kiwango kikubwa".















