Je ni kweli wanajeshi wa NATO wanapigana Ukraine?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Urusi Vladimir Putin anasema kuna vitengo vya kijeshi nchini Ukraine "chini ya amri ya washauri wa Magharibi".
Madai kama hayo pia yameonekana kwenye televisheni na mitandao ya kijamii ya Urusi kwamba wanajeshi wa Nato wanahusika kikamilifu katika vita hivyo.
Nchi wanachama wa Nato zimekuwa zikitoa msaada wa silaha na vifaa, lakini zimesema hazipeleki wanajeshi nchini Ukraine, nchi ambayo si mwanachama wa muungano huo.
Tumeangalia ushahidi uliotolewa kwa madai haya ya wanajeshi wa Nato kuwa nchini Ukraine.
Je madai hayo ni yapi?
Katika hotuba yake ya kitaifa tarehe 21 Septemba, Rais Putin alisema: "Utawala wa Kyiv umezindua magenge mapya ya mamluki wa kigeni na wanaharakati, vitengo vya kijeshi vilivyofunzwa kutokna na viwango vya Nato na chini ya amri ya washauri wa Magharibi."
Inajulikana kuwa wapiganaji wa kigeni wamejiunga na vitengo vya kijeshi vya Ukraine. Hata hivyo, madai yanatolewa na maafisa wa Urusi na vyombo vya habari vya kuwahudumia wanajeshi wa Nato nchini Ukraine.
Mnamo Septemba 13, Ruslan Ostashko, mmiliki wa Vremya Pokazhet (Time Will Tell) kwenye Channel One ya Urusi alisema: "Katika mpango mkuu wa mambo, askari wa UKraine wapo zaidi kwa kuonekana, kwa kuchukua picha na kupakia video kwa TikTok, lakini, ni wanajeshi wa Nato wanaopigana huko."

Chanzo cha picha, Channel One
Katika kipindi chote , picha zilizochukuliwa kutoka kwa mitandao ya kijamii za wageni wanaodaiwa kupigana nchini Ukraine zilionyeshwa kama "ushahidi" wa Nato kuwa nchini Ukraine.
Andrei Marochko, msemaji wa jeshi la nchi inayojiita Luhansk People's Republic (LPR) mashariki mwa Ukraine, ameliambia shirika la habari la Urusi RIA Novosti: "Mashirika yetu ya kijasusi yalifichua kuwasili kwa maafisa wa kawaida wa Nato katika eneo la Kharkiv.
"Madhumuni ya ziara yao katika eneo hili ni kuandaa mwingiliano kati ya vitengo vya kigeni na vya Ukraine."
Bw Marochko pia ameambia runinga ya serikali ya Urusi kwamba maafisa wa Nato wamefika Kramatorsk, mji ulio katika eneo la Donetsk nchini Ukraine.
Madai mengine kwa ujumla zaidi juu ya uwepo wa wapiganaji wa kigeni na hawahusishwi moja kwa moja na Nato .
Kwa mfano, Vladimir Kornilov, mwandishi wa gazeti la RIA Novosti, amesema kumekuwa na "ongezeko kubwa la picha za video za watu ambao wamekuja 'kuikomboa' Izyum, huku wakidaiwa kuzungumza Kiingereza."
Ni ushahidi gani unaotolewa?
Ni muhimu kuweka tofauti kati ya wapiganaji hao wa kigeni ambao wamesafiri kwa uhuru hadi Ukraine na wanajeshi waliotumwa na nchi wanachama wa Nato
Vyombo vya habari vya Urusi havijatoa ushahidi wa kuwepo kwa maafisa wa Nato nchini Ukraine, na badala yake vimetaja kuwepo kwa wapiganaji wa kigeni kwenye uwanja wa vita.
Mmoja wa wapiganaji wanaoonyeshwa kwenye kipindi cha televisheni cha Vremya Pokazhet ni Malcolm Nance, afisa wa zamani wa jeshi la wanamaji wa Marekani, ambaye amekuwa akichapisha mara kwa mara video zake akiwa Ukraine katika miezi ya hivi karibuni.
Video moja, iliyoangaziwa katika kipindi hicho, inamwonyesha Bw Nance akiwa na kibatari nyuma yake, akirusha kile anachokielezea kama "kombora la kwanza la silaha kubwa iliyounganishwa, ardhini."

Chanzo cha picha, Twitter
Akiwa na zaidi ya wafuasi milioni moja kwenye Twitter, kuna wachache sana ambao wanaweza kuona kuwa siri kuhusu uwepo wa Bw Nance nchini Ukraine.
Kwa sasa hatumikii katika jeshi la Marekani na mnamo mwezi Aprili, alichapisha mtandaoni kwamba amejiunga na Jeshi la Kigeni la Ukraine.
Mtu wa pili aliyetambuliwa katika mitandao ya kijamii inayoiunga mkono Urusi ni Mmarekani mwingine, Rob-Roy Lane, ambaye alikulia katika jimbo la Idaho nchini Marekani.
Bw Lane pia huchapisha mara kwa mara video zake mtandaoni akiwa na kikosi cha kijeshi cha Ukraine na kutaja wafanyakazi wengine wa kujitolea wa kigeni katika timu hiyo. Video hizi zimesamabzwa sana kwenye chaneli za mitandao ya kijamii zinazoiunga mkono Urusi.

Chanzo cha picha, Twitter
Picha ya Rob-Roy Lane. Maandishi "Kuwepo kwa mamluki wa Kimarekani katika kikundi cha Izyum cha Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine kulithibitishwa."
Hakuna ushahidi mtandaoni wa kupendekeza kuwa ana uzoefu wowote wa kijeshi hapo awali. Wizara ya Ulinzi ya Marekani haijajibu maombi ya maoni yake kuhusu kuhusika kwake na vikosi vya kijeshi vya Marekani.
Katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii, Bw Lane anawataja wanachama wengine kadhaa katika kitengo chake wakiwemo raia wawili wa Uingereza.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema haitazungumzia rekodi za huduma za maafisa wa kijeshi wa zamani, au kuhusu shughuli zao katika maeneo yenye migogoro.
Je Nato inatoa usaidizi gani?
Nchi wanachama wa Nato zinatoa kiasi kikubwa cha msaada wa kisasa wa silaha na vifaa kwa Ukraine, huku Marekani ikiwa mfadhili mkuu zaidi.
Vifaa hivi ni pamoja na mifumo kadhaa ya silaha ambayo inaaminika kuwa na jukumu muhimu katika mzozo hadi sasa, kama vile kurusha roketi za masafa marefu na silaha za kukinga mashambulizi ya vifaru.
Na pia kumekuwa na uvumi wa vyombo vya habari vya Magharibi kwamba wanachama wa Nato wamekuwa wakisaidia kwa akili na malengo ya kijeshi.

Kuna takriban wanajeshi 40,000 wa Nato walioko katika nchi wanachama katika kanda hiyo, kama vile katika mataifa ya Baltic na Poland, na wanajeshi wengine 300,000 wakiwa katika hali ya tahadhari kujibu uvamizi wa Urusi.
Mafunzo ya kina ya vikosi vya Ukraine na wanachama wa Nato yamekuwa yakifanyika nje ya nchi hiyo, lakini hakuna nchi mwanachama wa Nato imesema kuwa imechangia wanajeshi kupigana nchini Ukraine.
"Hakuna ushahidi wa vikosi vya Nato vya ardhini kushiriki Ukraine," anasema Edward Arnold kutoka Taasisi ya Huduma ya Royal United (Rusi), taasisi ya ulinzi na usalama.
"Wala makamanda wa Nato wanaoongoza vitengo vya Ukraine kwenye uwanja wa vita," anaongeza. "Pia kuna uwezekano mdogo sana wa hili kutokea katika siku zijazo kwani Nato inajaribu kupunguza hatari za kuongezeka."













