China yafanya mazoezi ya kushambulia 'maeneo muhimu' Taiwan

Chanzo cha picha, Reuters
China imefanya mazoezi ya kijeshi ya mashambulizi ya usahihi kulenga maeneo muhimu ya Taiwan na maji yanayoizunguka wakati wa siku ya pili ya mazoezi ya kijeshi.
Mazoezi hayo - ambayo Beijing imeyaita "onyo kali" kwa kisiwa hicho kinachojitawala - ni jibu kwa rais wa Taiwan kutembelea Marekani wiki iliyopita.
Wakati jeshi la China ilifanya mazoezi kuzunguka kisiwa hicho, Marekani iliitaka China kuonyesha kujizuia.
Taiwan ilisema angalau ndege 71 za China ziliruka kuzunguka kisiwa hicho siku ya Jumamosi.
Taiwan pia ilisema ndege 45 za kivita ama zilivuka mstari wa kati wa mlango bahari wa Taiwan - mstari usio rasmi wa kugawanya eneo la Taiwan na China - au ziliruka hadi sehemu ya kusini-magharibi ya eneo la utambulisho wa ulinzi wa anga wa Taiwan.
Meli tisa za China pia zilionekana. Operesheni hiyo iliyopewa jina la "Upanga wa Pamoja" na Beijing, itaendelea hadi Jumatatu.
Maafisa wa Taiwan wamekasirishwa na operesheni hiyo.
Siku ya Jumamosi maafisa wa ulinzi mjini Taipei waliishutumu Beijing kwa kutumia ziara ya Rais Tsai wa Marekani kama "kisingizio cha kufanya mazoezi ya kijeshi, ambayo yamevuruga pakubwa amani, utulivu na usalama katika eneo hilo".
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika siku moja ya mazoezi, meli moja ya Uchina ilirusha silaha ilipokuwa ikisafiri karibu na kisiwa cha Pingtan, sehemu ya karibu zaidi ya Uchina na Taiwan.
Baraza la Masuala ya Bahari la Taiwan, ambalo linasimamia Walinzi wa Pwani, lilitoa picha za video zinazoonyesha moja ya meli zake ikifuata meli ya kivita ya China, ingawa haikusema eneo hilo ni gani.
Katika picha hiyo baharia anasikika akiiambia meli ya Uchina kupitia redio: "Unaharibu sana amani, utulivu na usalama wa eneo hilo. Tafadhali geuka mara moja na uondoke. Ikiwa utaendelea tutachukua hatua za kuwafukuza."
Picha zingine zilionyesha meli ya kivita ya Taiwan, Di Hua, ikiandamana na meli ya Walinzi wa Pwani katika kile afisa wa Walinzi wa Pwani anaita "mkwamo" na meli ya Uchina.
Wakati mazoezi ya Wachina yalipokwisha Jumamosi jioni, maafisa wa ulinzi huko Taipei walisema upangaji wa ndege za kivita ulianza tena mapema Jumapili asubuhi.
Maafisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani wameitaka China kutotumia vibaya ziara ya Rais Tsai nchini Marekani, na wametoa wito wa "kuzuiwa na kusiwe na mabadiliko katika hali ilivyo sasa".
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje alisema Marekani "inafuatilia kwa karibu vitendo vya Beijing" na kusisitiza kuwa Marekani ina "rasilimali na uwezo wa kutosha katika eneo hilo ili kuhakikisha amani na utulivu na kutimiza ahadi zetu za usalama wa taifa".
Marekani ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Taipei na kuipendelea Beijing mwaka 1979, lakini inalazimika kwa sheria kuipa Taiwan njia ya kujilinda.
Rais wa Marekani Joe Biden amesema mara kadhaa kwamba Marekani ingeingilia kati iwapo China itashambulia kisiwa hicho, lakini ujumbe wa Marekani umekuwa wa kusuasua.
Katika mkutano wa Jumatano huko California, Bi Tsai alimshukuru Spika wa Bunge la Marekani Kevin McCarthy kwa "uungwaji mkono usioyumba" wa Marekani, akisema ulisaidia "kuwahakikishia watu wa Taiwan kwamba hatujatengwa na hatuko peke yetu".
Hapo awali Bw McCarthy alikuwa amepanga kwenda Taiwan mwenyewe, lakini akachagua kufanya mkutano huo huko California ili kuepusha mvutano kati yake na China.
Vyombo vya habari vya serikali ya China vilisema mazoezi ya kijeshi, ambayo yanatarajiwa kufanywa hadi Jumatatu, "yatapanga wakati huo huo kushika doria na kusonga katika kisiwa cha Taiwan, kuunda mazingira ya pande zote na kujilinda".
Imeongeza kuwa "mizinga ya roketi ya masafa marefu, meli za kivita majini, boti za makombora, wapiganaji wa jeshi la anga, washambuliaji wa mabomu, washambuliaji na wa kujaza mafuta" wote wametumwa na jeshi la China.
Lakini katika mji mkuu wa Taiwan Taipei, wakaazi walionekana kutokerwa na ujanja wa hivi karibuni wa China.
"Nadhani WaTaiwani wengi wameizoea kwa sasa, hisia ni kama, tunarudia tena!" Jim Tsai alisema Jumamosi.
Wakati huo huo, Michael Chuang alisema: "Wao [China] wanaonekana kupenda kufanya hivyo, kuzunguka Taiwan kama ni yao. Nimeizoea sasa.
"Wakivamia hatuwezi kutoroka hata hivyo. Tutaona siku zijazo itakuwaje."
Wakati huo huo, Michael Chuang alisema: "Wao [China] wanaonekana kupenda kufanya hivyo, kuzunguka Taiwan kama ni yao. Nimeizoea sasa.
Hali ya Taiwan imekuwa ya utata tangu 1949, wakati Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Uchina vilipounga mkono Mkomunisti wa China na chama cha serikali tawala ya zamani ya nchi hiyo kilipojiondoa kisiwani humo.
Tangu wakati huo Taiwan imejiona kuwa nchi huru, yenye katiba yake na viongozi wake.
Uchina inaliona kama jimbo lililojitenga ambalo hatimaye litawekwa chini ya udhibiti wa Beijing - kwa nguvu ikiwa ni lazima.
Rais Xi Jinping amesema "kuungana tena" na Taiwan "lazima kutekelezwa".















