Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini mji wa Goma nchini DRC ni muhimu na kwa nini waasi wa M23 wanautaka?
Mji wa Goma ulio mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umekuwa tena kitovu cha mzozo wa kikanda uliodumu kwa miongo kadhaa. Mapigano kati ya kundi lenye silaha linalojulikana kwa jina la M23 na jeshi la Congo yamezidi katika eneo hilo, na kuwafukuza zaidi ya watu 400,000 kutoka makwao tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Lakini kwanini Goma - mji mkuu wa mkoa huo - ni mji unaopiganiwa ?
M23 ni akina nani?
Kundi la M23 ni kundi lenye silaha ambalo lilijitenga na jeshi la Kongo miaka kumi iliyopita kwa madai ya kuwalinda Watutsi ambao kwa muda mrefu walikuwa wakilalamikia mateso na ubaguzi. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa kundi hilo linaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, ambayo pia inaongozwa na Watutsi, jambo ambalo serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha mara kwa mara.
Rwanda imesema hapo awali kwamba mamlaka nchini DR Congo inashirikiana na baadhi ya waliohusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Mwaka 2012, waasi waliikalia Goma kwa siku 10 kabla ya kuiacha kufuatia shinikizo la kimataifa.
Baada ya hayo, kundi la M23 lilipata pigo baada ya kushindwa vibaya na jeshi la Kongo likisaidiwa na jeshi la kimataifa ambalo lilishuhudia kufurushwa kwao kutoka nchini humo. Wapiganaji wa M23 kisha walikubali kushirikishwa tena katika jeshi kwa ahadi kwamba Watutsi watalindwa.
Lakini, mwaka 2021, kundi hilo lilichukua tena silaha, likisema ahadi zilikuwa hazijatimizwa.
M23 tangu wakati huo wamechukua udhibiti wa maeneo mengi zaidi katika eneo la mashariki kuliko hapo awali. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema Rwanda ina hadi wanajeshi 4,000 wanaofanya kazi pamoja na M23 mashariki mwa Kongo DR.
Eneo la Goma
Likiwa kwenye ufuo wa kaskazini mwa Ziwa Kivu kwenye mpaka wa Rwanda, Goma daima imekuwa kitovu muhimu cha kisiasa na kibiashara.
Mji huo una watu zaidi ya milioni moja na kuufanya kuwa moja ya miji yenye watu wengi zaidi Kongo. Kutokana na udongo wake wa volkeno, wenye rutuba kihistoria mji huo umekuwa kituo cha biashara chenye shughuli nyingi na nchi jirani ya Rwanda.
Goma ni mojawapo ya miji mikuu ya uchimbaji madini inayosambaza madini yanayohitajika sana kimataifa kama vile dhahabu, bati, kobalti na koltani na ina barabara muhimu za kimkakati za usafiri wa barabarani na angani. Pia ina kambi kubwa ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa suala ambalo limevutia biashara nyingi, mashirika ya kimataifa na balozi.
Utajiri wa Goma
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inakadiriwa kumiliki asilimia 70 ya madini ya cobalt duniani, madini muhimu katika kuwezesha betri za lithiamu-ion katika simu za mkononi, magari ya umeme na aina nyingi za sigara za kielektroniki.
Huku ulimwengu unapojitolea kupunguza utoaji wa gesi chafuzi kwa kuhama kutoka kwa nishati ya kisukuku, kuna ongezeko la mahitaji ya vyanzo safi vya nishati.
Tishio la vita vipya vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linaweza kuvuruga ugavi wa kimataifa, kupanda kwa bei na kusababisha uhaba katika tasnia ya teknolojia na nishati safi.
Je, Goma ikitekwa?
Rais wa Kongo Félix Tshisekedi mwaka 2023 alisema kuwa "Goma haitatekwa kamwe". Ahadi zake za kuhakikisha kuwa mji huo hauna waasi zilikuwa juu kwenye orodha yake ya ahadi kwa watu wa Kongo, ikimaanisha kutekwa kwa Goma kungemuathiri kisiasa kiongozi huyo aliyechaguliwa tena.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekata uhusiano wote na nchi jirani ya Rwanda, jambo ambalo limesababisha onyo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwamba mzozo wa sasa unaweza kuhatarisha kuongezeka kwa vita vya kikanda.
Kuongezeka kwa mzozo kunaweza pia kusababisha uhaba wa rasilimali za kibinadamu ambazo tayari zimepungua kutokana na machafuko mengine.
Wakati M23 inasonga mbele katika eneo la mashariki, maelfu katika vijiji vidogo wanayahama makazi yao na kuelekea katika hospitali za karibu huko Goma, jambo ambalo linawalemea.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeonya juu ya kuongezeka kwa hatari kwa raia huku jeshi la Kongo likipambana na waasi wa M23. Kundi la misaada ya kibinadamu linashutumu pande zote mbili kwa kutekeleza unyanyasaji mkubwa dhidi ya raia.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla