Israel na Hezbollah: Israel inakabiliwa na adui mwenye silaha na hasira

Chanzo cha picha, EPA
Na Jeremy Bowen
Mhariri wa Maasuala ya Kimataifa - Jerusalem
Viongozi wa Israel wamefurahishwa na hatua za mashambulizi dhidi ya Hezbollah, ambayo yalianza kwa milipuko ya pagers na redio za upepo na baadaye kuhamia kwenye mashambulizi makubwa na ya anga.
Waziri wa ulinzi Yoav Galant hakusita kusifu mashambulizi ya anga ya Jumatatu, akisema: "Operesheni ya leo ilikuwa kamilifu. Hii ilikuwa wiki mbaya zaidi kwa Hezbollah tangu kuanzishwa kwake, na matokeo yanajionyesha yenyewe."
Galant amesema mashambulizi hayo ya anga yaliharibu maelfu ya roketi ambazo zingeweza kuwaua raia wa Israel, huku mamlaka za Lebanon zikisema Israel iliwaua zaidi ya raia 550, wakiwemo watoto 50, wakati wa operesheni ya kijeshi. Idadi hii ni sawa na nusu ya idadi ya watu waliouawa nchini Lebanon wakati wa vita vya mwezi mzima kati ya Israel na Hezbollah mwaka 2006.
Israel inaamini kuwa shambulio hilo kali litailazimisha Hezbollah kufanya makubaliano, na kumlazimisha kiongozi wa chama hicho, Hassan Nasrallah, na washirika wake pamoja na wafuasi wake nchini Iran, kulipa gharama kubwa ya vita, na kukiri kwamba "upinzani [wa Hezbollah] una madhara makubwa sana."
Wanasiasa na majenerali wa Israel wanahitaji ushindi. Baada ya karibu mwaka mmoja wa vita, Gaza ni mahali ambapo kumekuwa pagumu kukomboa. Wapiganaji wa Hamas bado wanaibuka kutoka kwenye mahandaki na vifusi ili kuwalenga wanajeshi wa Israel, na bado wanashikilia mateka wa Israel.
Hamas iliishangaza Israel mwezi Oktoba mwaka jana, lakini Waisraeli hawakuona Hamas kama tisho kubwa, na hilo lilikuwa na matokeo mabaya. Nchini Lebanon, hali ni tofauti.
Jeshi la Israel na shirika la ujasusi la Mossad walikuwa wakipanga vita dhidi ya Hezbollah tangu vita vya mwisho vilipomalizika mwaka 2006.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anaamini mashambulizi ya sasa yanapiga hatua kubwa kuelekea lengo lake la kubadili uwiano na mamlaka mbali na Hezbollah.
Netanyahu anataka kuizuia Hezbollah kurusha roketi katika mpaka na kuingia Israel, wakati jeshi la Israel linasema mpango huo unalenga kulilazimisha kundi la Hezbollah kurudi nyuma mbali na mpakani na kuharibu vituo vyake vya kijeshi vinavyotishia Israel.
Gaza nyingine
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wiki iliyopita nchini Lebanon kumekuwa na sura ya vita sawa na vile vya Gaza, huku Israel ikitoa onyo kwa raia kama ilivyo katika Ukanda wa Gaza kuondoka kwenye maeneo yanayokaribia kushambuliwa, na kulilaumu kundi la Hezbollah kama ilivyo kwa Hamas , kwa kuwatumia raia kama ngao ya binadamu.
Baadhi ya wapinzani, pamoja na maadui wa Israel, walisema maonyo hayo hayakuwa wazi na hayakuzipa familia muda wa kutosha wa kuyahama makazi yao. Sheria za vita zinahitaji ulinzi wa raia na kuzuia matumizi ya nguvu ya jumla na yasiyo ya kawaida.
Baadhi ya mashambulizi ya Hezbollah dhidi ya Israel yamelenga maeneo ya raia - kinyume na sheria za ulinzi wa raia - pamoja na jeshi la Israel.
Israel na washirika wake wakuu wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, wanaliliorodhesha kundi la Hezbollah kama kundi la kigaidi.
Israel inasisitiza kuwa jeshi lake linazingatia maadili ya vita na kuheshimu sheria, lakini serikali nyingi duniani kote zimelaani mwenendo wake huko Gaza, na vita vipya vya mpakani vitaongeza mjadala juu ya mwenendo wa Israeli.
Tukiangalia milipuko ya hivi karibuni ya pager na Redio za upepo, Israel inasema shambulio hilo lililenga wanajeshi wa Hezbollah ambao walikuwa na vifaa hivyo (afisa wa Israel aliiambia BBC kwa masharti ya kutotajwa jina), lakini haikuweza kujua ni wapi vifaa hivyo vililipuliwa, vikiwajeruhi na kuwaua raia na watoto majumbani, madukani na maeneo mengine ya umma.
Mawakili wakuu wanasema hii inathibitisha kuwa Israeli ilikuwa inatumia "nguvu nyingi" bila kutofautisha kati ya wapiganaji na raia, ukiukaji wa sheria za vita.
Mapigano kati ya Israel na Hezbollah yalianza miaka ya 1980, lakini vita vya sasa vya mpakani vilianza siku moja baada ya Hamas kuishambulia Israel mnamo Oktoba 7, wakati Hassan Nasrallah alipowaamuru watu wake kuanza mashambulizi ya mpakani kila siku, kuwaunga mkono Hamas. Hii ilisababisha kuzingirwa kwa vikosi vya Israeli na kuwalazimisha watu 60,000 katika miji ya mpakani kuondoka majumbani mwao upande wa Israeli.
Vita vya awali
Baadhi ya kauli katika vyombo vya habari vya Israel zimelinganisha athari za mashambulizi ya anga dhidi ya uwezo wa Hezbollah na vita vya kushtukiza ambavyo Israel ilianzisha dhidi ya Misri mnamo Juni 1967, wakati Israeli ilifanya uvamizi maarufu ambao uliharibu jeshi la anga la Misri wakati ndege zake zilikuwa zimejipanga ardhini. Katika siku sita zilizofuata, Israel iliishinda Misri, Syria na Jordan, na ushindi huo umechangia mgogoro wa sasa, huku Israel ikiutwaa Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, Ukanda wa Gaza na milima ya Golan.
Hata hivyo kauli hizi zinapingwa na baadhi wanaosema matukio hayo hayawezi kulinganishwa kwani Lebanon na vita dhidi ya Hezbollah ni vitu viwili tofauti. Israel imekumbwa na pigo kubwa, lakini hadi sasa haijazuia uwezo wa Hezbollah kuilenga Israel.
Vita vya awali vya Israel na Hezbollah vilikuwa vya kuvutia, kamwe havikusababisha ushindi wa maamuzi kwa upande wowote, na vita hivi vinaweza kuendelea katika mtindo huo huo.
Shambulio la Israel limetokana na dhana kwamba Hezbollah itaanguka wakati fulani, kuondoka kwenye mpaka na kuacha kuishambulia Israel. Waangalizi wengi wa Hezbollah wanaamini kuwa haitakoma, kwa kuzingatia kuwa kupigana na Israel ndio sababu kuu ya kuwepo kwa Hezbollah.
Hii inamaanisha kuwa Israel, ambayo haikubali kushindwa, italazimika kuongeza vita zaidi, na ikiwa Hezbollah itaendelea kutishia kaskazini mwa Israeli, na kulifanya kuwa eneo hatari sana kwa raia wa Israeli ambao hawawezi kurudi nyumbani, Israeli italazimika kuamua juu ya mashambulizi ya ardhini, labda kuchukua udhibiti wa ukanda wa mpaka ili kutumika kama eneo la amani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Israel iliwahi kuivamia Lebanon. Mwaka 1982, vikosi vyake vilivamia Beirut katika jaribio la kuzuia uvamizi wa Wapalestina dhidi ya Israel, lakini walilazimika kurudi nyuma kutokana na hasira za ndani na nje. Baada ya vikosi vya Israel kuchukua udhibiti wa eneo la Beirut, washirika wake walifanya mauaji dhidi ya raia wa Palestina katika kambi za wakimbizi za Sabra na Shatila mjini Beirut.
Hadi miaka ya 1990, Israel bado ilikuwa imekalia eneo kubwa la Lebanon kwenye mpaka. Majenerali wa Israel wa leo walikuwa maafisa vijana ambao walipigana vita vya umwagaji damu dhidi ya Hezbollah.
Mwaka 2000, Ehud Barak, aliyekuwa waziri mkuu wa Israel na mkuu wa zamani wa jeshi la Israel, alijiondoa katika kile kinachoitwa "eneo la usalama," akisema kuwa mapambano hayo hayataifanya Israel kuwa salama, na ingegharimu maisha ya idadi kubwa ya wanajeshi wake.
Mwaka 2006, uvamizi wa Hezbollah katika mpaka uliokumbwa na ghasia uliua na kuwateka wanajeshi wa Israel, na baada ya vita kumalizika, Hassan Nasrallah alisema hangeruhusu uvamizi huo kama angejua kile ambacho Israel inaweza kufanya.
Ehud Olmert, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel, aliamua kwenda vitani. Awali, Israel ilitarajia kwamba nguvu za anga zingezuia mashambulizi ya roketi dhidi ya Israel, lakini wakati hilo halikutokea, vikosi vya ardhini na vifaru viliondoka, na kuacha nyuma janga kwa raia wa Lebanon. Hata hivyo, Hezbollah iliendelea kurusha makombora dhidi ya Israel.
Vita vya sasa na vijavyo
Viongozi wa Israel wanatambua kuwa vita nchini Lebanon vinaleta changamoto kubwa ya kijeshi kuliko kupambana na Hamas katika Ukanda wa Gaza. Hezbollah ilianza kufanya mipango yake mwishoni mwa vita vya mwaka 2006, na itapigana katika eneo lake la kusini mwa Lebanon, ambalo limejipenyeza katika milima ambayo inatumika kwa mbinu za kivita za msituni.
Israel haijaweza kuharibu mahandaki yote ambayo Hamas imechimba Gaza, na katika maeneo ya mpakani ya kusini mwa Lebanon, Hezbollah imetumia miaka kumi na minane iliyopita kuandaa mahandaki na maeneo ya kivita katika miamba. Hezbollah sasa ina silaha nyingi zinazosambazwa na Iran, na tofauti na Hamas huko Gaza, inaweza kupokea silaha zaidi kupitia Syria.
Kituo cha mafunzo ya kimkakati cha kimataifa, ambacho ni kituo cha utafiti chenye makao yake mjini Washington, DC, kinakadiria kuwa Hezbollah ina wapiganaji 30,000 na hadi 20,000 wa akiba, wengi wao wakiwa wamefunzwa kama vitengo vidogo, na wengi wao wana uzoefu wa mapigano walioupata wakati wa kuunga mkono utawala wa Assad nchini Syria.
Makadirio mengi yanasema Hezbollah ina kati ya makombora 120,000 na 200,000, kuanzia silaha za masafa marefu hadi silaha za masafa marefu ambazo zinaweza kushambulia miji ya Israel.

Chanzo cha picha, Getty Images
Israel huenda ikabashiri kwamba Hezbollah haitatumia silaha hizo zote, ikihofia kwamba jeshi la anga la Israel litafanya nchini Lebanon kile ilichokifanya Gaza, na kugeuza miji yote kuwa vifusi na kuwaua maelfu ya raia.
Iran huenda isitake Hezbollah kuweka wazi silaha inazotaka kuzitumia kama kinga dhidi ya shambulio la Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran. Hezbollah inaweza kulazimika kutumia silaha zake nyingi kabla ya Israel kuziangamiza.
Wakati vita vya Gaza vikiendelea na ghasia zikiongezeka katika Ukingo wa Magharibi, Israel pia italazimika kufikiria kufungua mlango wa tatu ikiwa itaivamia Lebanon. Israel ina wanajeshi waliofunzwa vizuri na wenye vifaa vya kutosha, lakini vikosi vya akiba vinavyotoa nguvu kubwa ya mapigano ya Israel tayari vinahisi matatizo baada ya mwaka mmoja wa vita.
Mkwamo wa diplomasia
Washirika wa Israel, wakiongozwa na Marekani, hawataki Israel izidishe vita na Hezbollah au kuivamia Lebanon, na kusisitiza kuwa diplomasia pekee ndiyo inayoweza kuufanya mpaka huo kuwa salama vya kutosha ili kuruhusu raia kurejea majumbani mwao. Mjumbe wa Marekani aliidhinisha makubaliano yaliyotokana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1701 lililomaliza vita vya mwaka 2006.
Lakini mikono ya wanadiplomasia imefungwa kwa kukosekana kwa usitishaji mapigano Gaza. Nasrallah anasema Hezbollah haitaacha kuishambulia Israel hadi vita vya Gaza vitakapomalizika, na kwa sasa Hamas wala Waisraeli hawako tayari kufanya makubaliano muhimu ambayo yatasababisha usitishaji mapigano huko Gaza na kubadilishana mateka wa Israel kwa wafungwa wa Kipalestina.
Wakati mashambulizi ya anga ya Israel yakiendelea dhidi ya Lebanon, raia ambao tayari wanahangaika kuzihudumia familia zao huku uchumi ukiporomoka wanakabiliwa na hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu siku zijazo. Hofu inavuka mstari wa mbele, kama Waisraeli wanavyotambua kwamba Hezbollah inaweza kusababisha uharibifu zaidi kwao kuliko ilivyokuwa katika mwaka uliopita.
Israel inaamini kuwa ni wakati wa kuwa jasiri na kuisukuma Hezbollah mbali na mipaka yake, lakini inakabiliwa na adui mkaidi, mwenye silaha na mwenye hasira. Huu ni mgogoro mkubwa zaidi katika mwaka mrefu wa vita, na kwa sasa hakuna kitu cha kuuzuia kuwa hata mbaya zaidi.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla












