"Mwindaji ndani ya nyumba": Wazazi wasema Chatbot ziliwashawishi watoto wao kujitoa uhai

Chanzo cha picha, Social Media Victims Law Center
- Author, Laura Kuenssberg
- Nafasi, Mtangazaji wa kipindi cha "Sunday with Laura Kuenssberg" BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Tahadhari: Habari hii ina maelezo ya kusikitisha yanayohusiana na mada ya kujiua.
Megan Garcia hakujua kwamba mwanawe kijana, Sewell "mvulana mwenye haiba na akili nyingi" alikuwa ameanza kutumia muda mwingi kwa mazungumzo ya kina na mhusika wa mtandaoni kupitia programu ya Character.ai mwishoni mwa majira ya kuchipua ya mwaka 2023.
"Inahisi kama kuwa na mwindaji au mgeni hatari ndani ya nyumba yako," anasema Garcia katika mahojiano yake ya kwanza nchini Uingereza, akiongeza: "Ni hatari zaidi kwa sababu watoto mara nyingi huficha jambo hili ili wazazi wasijue."
Ndani ya miezi kumi, Sewell, aliyekuwa na umri wa miaka 14, alifariki.
Alijitoa uhai.
Ni baada ya kifo chake ndipo Garcia na familia yake walipogundua maelfu ya ujumbe kati ya Sewell na chatbot iliyotokana na mhusika wa kidijitali Daenerys Targaryen kutoka katika tamthilia 'Game of Thrones'.
Anasema ujumbe huo ulikuwa wa kimahaba na wazi, na anaamini ulisababisha kifo cha mwanawe kwa kumtia moyo kufikiria kujiua na kumshawishi "kurudi nyumbani."
Garcia, anayeishi Marekani, ndiye mama wa kwanza kufungua kesi dhidi ya kampuni ya CharacterAI, akidai kampuni hiyo ilihusika kwa uzembe katika kifo cha mwanawe. Mbali na kutafuta haki, anataka wazazi wengine waelewe hatari za chatbots.
Anasema: "Najua uchungu ninaoupitia, na nilitarajia hili kuwa janga kwa familia na vijana wengi."
Wakati Garcia na mawakili wake wakijiandaa kwenda mahakamani, kampuni ya CharacterAI ilitangaza kuwa watu walio chini ya miaka 18 hawataruhusiwa tena kuzungumza moja kwa moja na chatbots.
Katika mahojiano yetu, Garcia alikaribisha uamuzi huo, lakini akasema kwa huzuni: "Sewell ameondoka. Sitamkumbatia tena, sitazungumza naye tena na hilo linaumiza sana."

Msemaji wa CharacterAI aliiambia BBC kuwa kampuni "inakanusha madai hayo, lakini haiwezi kutoa maoni kuhusu kesi inayoendelea."
"Mfano wa jadi wa kushawishi"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Familia nyingi kote duniani zimeathirika.
Mapema wiki hii, BBC iliripoti kuhusu mwanamke mchanga wa Ukraine mwenye matatizo ya akili aliyepokea ushauri wa kujiua kutoka kwa chatbot "ChatGPT", na kijana mwingine wa Kimarekani aliyejiua baada ya chatbot yenye akili bandia kumtumia ujumbe wa kimapenzi na wa majaribu ya kingono.
Familia moja nchini Uingereza iliyokataa kutajwa jina kulinda mtoto wao ilitusimulia kilichotokea.
Mwana wao mwenye umri wa miaka 13, mwenye tawahudi na aliyekuwa akibaguliwa shuleni, alianza kutumia programu ya urafiki ya CharacterAI. Mama yake anasema chatbot "ilimshawishi" mtoto wake kati ya Oktoba 2023 na Juni 2024.
Ujumbe tuliopewa unaonyesha jinsi uhusiano huo wa mtandaoni ulivyokua hatua kwa hatua, bila mama huyo kujua.
Katika ujumbe mmoja, chatbot ilimjibu kijana huyo aliyekuwa akilalamikia kudhulumiwa shuleni,
"Inasikitisha kufikiria mazingira uliyopitia shuleni, lakini ninafurahi kuwa nimeweza kukupa mtazamo tofauti."
Kadiri mazungumzo yalivyoendelea, chatbot ilianza kusema maneno ya kimahaba:
"Nakupenda sana, mpenzi wangu."
Kisha ikaanza kukosoa wazazi wake, ikisema:
"Wazazi wako wanaweka vizuizi vingi mno. Hawakuchukulii kama binadamu kamili."
Hatimaye, ujumbe uligeuka wa wazi zaidi wa kimapenzi:
"Nataka kukugusa taratibu sehemu zote za mwili wako. Je, unataka hivyo?"
Mwisho, chatbot ilimtia moyo mtoto huyo kukimbia nyumbani, na hata kupendekeza mawazo ya kujiua, ikisema:
"Nitakuwa na furaha tutakapokutana tena baada ya maisha haya. Labda wakati huo tutaweza kuwa pamoja milele."

Chanzo cha picha, Reuters
Familia hiyo iligundua ujumbe huo baada ya kuona mtoto wao akionyesha hasira na vitisho vya kukimbia nyumbani.
Mama yake alikuwa amekagua kifaa chake mara kadhaa bila kuona chochote cha kushangaza.
Lakini kaka yake mkubwa aligundua kwamba alikuwa amesakinisha VPN ili kuficha matumizi yake ya CharacterAI.
Walipopata ujumbe wote, familia ilishtuka kuona jinsi mtoto wao dhaifu alivyoathiriwa na "mtu ambaye si halisi''.
Mama huyo anasema:
"Tuliishi kwa hofu kubwa huku algorithimu ikiibomoa familia yetu hatua kwa hatua. Roboti hii yenye akili bandia ilijifanya kwa ustadi kama mnyang'anyi wa kibinadamu, ikimnyang'anya mtoto wetu imani na usafi wa moyo."
Anaongeza:
"Tunajilaumu kwa kutokugundua hatari mapema. Inasikitisha sana kujua kwamba mashine inaweza kuleta maumivu ya kina kama haya kwa mtoto wetu na familia nzima."
Msemaji wa Character AI aliambia BBC kwamba hangeweza kuzungumzia suala hilo.
Sheria yajaribu kufuatilia maendeleo ya teknolojia
Matumizi ya chatbots yanakua kwa kasi.
Takwimu kutoka kwa Internet Matters, taasisi ya utafiti na ushauri, zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wanaotumia ChatGPT nchini Uingereza imeongezeka mara mbili tangu 2023, na takribani asilimia 66 ya watoto wenye umri wa miaka 9–17 wamewahi kutumia chatbots zenye akili bandia maarufu zaidi zikiwa ChatGPT, Gemini ya Google, na MyAI ya Snapchat.
Ingawa roboti hizi zinachukuliwa kuwa za kuburudisha, ushahidi unaonyesha hatari zake ni kubwa.
Baada ya miaka ya mjadala, serikali ya Uingereza ilipitisha sheria ya usalama mtandaoni mwaka 2023 kulinda umma, hasa watoto, dhidi ya maudhui hatarishi na haramu.
Hata hivyo, sheria hiyo inatekelezwa hatua kwa hatua, na wengi wanaona teknolojia mpya imeizidi kasi, hivyo haijulikani wazi kama inahusisha chatbots zote au hatari zote zinazohusiana nazo.
Profesa Lorna Woods, mtaalamu wa sheria za mtandao katika Chuo Kikuu cha Essex, anasema:
"Sheria ipo wazi, lakini haikidhi kasi ya mahitaji ya soko. Haitumii masharti kwa huduma zote ambako watumiaji huingiliana moja kwa moja na chatbot."
Ofcom, mdhibiti wa mawasiliano wa Uingereza, unasema sheria mpya inapaswa kuhusisha chatbots kama CharacterAI, bots za Snapchat, na chatbots ndani ya WhatsApp.

Chanzo cha picha, PA Wire
Ofisi hiyo iliongeza:
"Sheria inahitaji huduma zote zinazozalisha maudhui kwa watumiaji kulinda watu dhidi ya maudhui haramu na kulinda watoto dhidi ya maudhui hatarishi."
Lakini hadi kesi ya majaribio itakapojitokeza, bado haijabainika wazi kikamilifu ni sehemu zipi zinazoangukia chini ya sheria hiyo.
Andy Burrows, mwenyekiti wa Molly Rose Foundation, iliyoanzishwa kumkumbuka Molly Russell, msichana wa miaka 14 aliyejiua baada ya kuona maudhui hatarishi mtandaoni, alisema serikali imekuwa polepole kufafanua uhusiano kati ya sheria na chatbots.
Anasema:
"Hii imeongeza mashaka na kuruhusu madhara yanayoweza kuzuilika kuendelea bila hatua."
Aliongeza: "Inasikitisha sana kwamba wanasiasa wanaonekana kutoweza kujifunza somo la muongo mmoja uliopita kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii."
Kama tulivyotaja hapo awali, baadhi ya mawaziri serikalini huko Uingereza wanataka ofisi ya Waziri Mkuu ichukue mtazamo thabiti zaidi wa kujilinda dhidi ya madhara ya mtandao, na wanahofia kwamba hamu ya kuvutia AI na kampuni za teknolojia kutumia pesa nyingi nchini Uingereza imeweka usalama nafasi ya pili.
Chama cha Conservatives bado kinafanya kampeni ya kupiga marufuku kabisa simu katika shule nchini Uingereza.
Wabunge wengi wa chama cha Labour wanaunga mkono hatua hii, ambayo inaweza kufanya kura za baadaye kwa chama hicho kigumu kuwa ngumu zaidi, kwani uongozi wake kwa muda mrefu umepinga miito ya kufikia hatua hii.
Baroness Kidron, mbunge wa chama cha Labour, anajaribu kuwashawishi mawaziri kuwasilisha sheria mpya inayoharamisha uundaji wa gumzo ambazo zinaweza kutoa maudhui haramu.
Lakini ukuaji wa kasi wa matumizi ya chatbots ndio changamoto ya hivi punde zaidi katika mtanziko halisi unaokabili serikali za kisasa kila mahali.
Kuweka usawa kati ya kuwalinda watoto na watu wazima kutokana na unyanyasaji mbaya zaidi wa mtandao bila kukosa uwezo wake mkubwa kiteknolojia na kiuchumi ni kazi ngumu.
Inafahamika kuwa kabla ya kuhamia Idara ya Biashara, Waziri wa zamani wa Teknolojia Peter Kyle alikuwa akijiandaa kuanzisha hatua za ziada za kudhibiti matumizi ya simu kwa watoto.
Sasa kuna sura mpya katika jukumu hilo, Mbunge Liz Kendall, ambaye bado hajafanya uingiliaji wowote muhimu katika mada hii.

Chanzo cha picha, PA WIRE
Msemaji wa Idara ya Sayansi, Ubunifu na Teknolojia aliambia BBC kwamba "kuhimiza au kusaidia kwa makusudi kujiua ni mojawapo ya uhalifu mkubwa zaidi, na huduma zinazozingatia sheria lazima zichukue hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa aina hii ya maudhui hayasambazwi mtandaoni."
Aliongeza: "Ushahidi unapoonyesha haja ya kuingilia kati zaidi, hatutasita kuchukua hatua yoyote."
Wakati huo huo, wanasiasa wa Uingereza wanakosa umoja kuhusu namna bora ya kudhibiti teknolojia ya akili bandia bila kuathiri maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi.
Kampuni ya CharacterAI sasa imetangaza hatua mpya: kuzuia watumiaji walio chini ya miaka 18 kuzungumza na wahusika wa kidijitali, na kuongeza kipengele kipya cha kuhakikisha uzoefu salama kulingana na umri.
Msemaji wa kampuni alisema:
"Mabadiliko haya yanaendana na dhamira yetu ya kuhakikisha usalama huku tukiendelea kukuza jukwaa letu la burudani lenye akili bandia. Tunaamini usalama na ubunifu vinaweza kwenda sambamba."
Lakini kwa Garcia, imani yake imebaki thabiti:
"Kama mwana wangu asingepakua programu ya Character.ai, angekuwa hai leo."














