Mkenya alivyopata kiwewe kutokana na kazi aliyofanya katika kampuni ya AI

..

Chanzo cha picha, bbc

Maelezo ya picha, Mophat Okinyi mwenye umri wa miaka 27 anasema kufanya kazi katika AI kumemtia kiwewe

Wafanyakazi wa Kenya wameelezea shinikizo la akili na athari za kisaikolojia zilizowakabili ili kuhakikisha teknolojia ya Akili Bandia AI iko salama.

Programu ya Akili Bandia (AI) imeenea kwa kasi ulimwenguni kote na ili kufanya programu za gumzo kama vile ChatGPT kuwa salama, wasimamizi wameajiriwa ili kuhakikisha AI inaweza kutambua maudhui makali na kuhakikisha kuwa hayaonyeshwi kwa watumiaji.

Ni tasnia inayokua kwa kasi na yenye thamani ya mabilioni ya dola inayoajiri maelfu ya watu katika maeneo yenye mapato ya chini kama vile Afrika, India na Ufilipino na vilevile nchi zilizo kwenye hatua za juu za uvumbuzi wa teknolojia kama vile Uchina na Marekani.

Lakini mchakato huo wa kuunda vichujio hivi vya usalama unaweza kuwaathiri wale wanaotazama nyenzo za picha.

"Ninahisi kama maisha yangu yote yameisha," Mophat alisema. “Tumaini langu limetoweka, ni kana kwamba nimepoteza kila kitu.

.
Maelezo ya picha, Mkenya huyo alifanya kazi kama mfuatiliaji wa lebo ya data na kuripoti maudhui makali

Gharama ya Akili Bandia

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 27 alisema tatizo la kiakili alilopata lilimbadilisha, na kugharimu ndoa yake na urafiki na kumwacha na huzuni.

Wenzake wengine pia waliripoti kuwa na tatizo la kiakili.

Mophat alifanya kazi na kampuni ya Sama, ambayo ilipewa kandarasi na kampuni ya ChatGPT.

Yeye na wenzake walipewa jukumu la kuripoti nyenzo chafu ili kuzuia chatbot kuwapatia watumiaji - huku Mophat, mwenye jukumu la kusimamia data akitazama nyenzo zote zilizo na lebo na kuhakikisha kuwa ni sahihi.

Anasema kila siku ni lazima asome vifungu vya maandishi vinavyozungumzia vurugu, chuki, kujidhuru na maudhui ya ngono.

"Yalikuwa maandishi ya kutisha sana," alisema. "Baada ya kusoma maandishi haya kwa miezi minne, fikra zangu zilibadilika ‘’

"Kutokana na mabadiliko ya tabia nilipoteza familia yangu, mke wangu, na hadi sasa bado nina huzuni."

.
Maelezo ya picha, Mophat anasema amehuzunika kutokana na kusoma maandishi kuhusu vurugu, matamshi ya chuki na kujidhuru kila siku.

Ombi la Bunge

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mophat ameungana na waweka lebo wengine kuwasilisha malalamishi katika bunge la Kenya kuchunguza hali ya ajira katika makampuni ya teknolojia ya Kenya ambayo yanatumiwa na makampuni makubwa ya teknolojia ya kigeni kwa ukadiriaji wa nje na kazi nyingine za AI.

Anasema hawakufunzwa vya kutosha kukabiliana na viwango vya maudhui makali waliyokumbana nayo wala kutoa msaada wa kutosha wa ushauri wa kitaalamu - tuhuma ambazo Sama anakanusha vikali.

Mwanasaikolojia na mtaalamu wa PTSD Dkt. Veronicah Ngechu alieleza kuwa kufichuliwa kwa maudhui makali mtandaoni kulijulikana kama kiwewe cha awamu ya pili na kunaweza kuongeza madhara zaidi.

"Kiwewe cha awamu ya pili huwa kina madhara zaidi kwa sababu ya kutokuwa na msaada wa karibu’’,alisema.

“Kwa sababu unaona hakuna msaada wowote, huna mtu wa kuripoti kwake, hakuna unachoweza kufanya kuhusu hilo.

"Na kwa sababu ni ukadiriaji wa yaliyomo kuna hali ya kutotabirika, haujui utaona nini, haujui jinsi itaongezeka."

Dkt. Ngechu anasema dalili za kiwewe cha pili zinaweza kujumuisha ndoto mbaya, kuepusha kuwasiliana na watu, kukosa huruma na kuwa na wasiwasi au fadhaa kwa jambo lolote ambalo linaweza kusababisha kumbukumbu ya kile wanachosema au kusoma.

Alisema ni 'lazima' kampuni zitoe msaada wa ushauri.

"Ili kuhakikisha kuwa haiathiri utendakazi wao, ubora wa maisha yao."

Madai ya unyanyasaji wa wasimamizi wa maudhui nchini Kenya si mapya.

Mwezi Mei zaidi ya wasimamizi 150 wa maudhui wa Kiafrika ambao wametoa huduma kwa zana za AI zinazotumiwa na makampuni kadhaa makubwa ya teknolojia walipiga kura kuanzisha Muungano wa Wasimamizi wa Maudhui wa kwanza.

Na ni aina hii ya utambuzi na uelewa ambao Mophat anataka kutoka kwa makampuni makubwa ya teknolojia na mabilioni ya watumiaji wao.

"Watu wanapaswa kujua kwamba watu waliofanya majukwaa yao kuwa salama ni wasimamizi wa maudhui, kwa sababu watu wengi hawajui uwepo wa kundi hilo la watu."

.
Maelezo ya picha, Mwajiri wa zamani wa Mophat anasema msaada wa kisaikolojia unatolewa kwa wafanyakazi

Sama amepinga madai yote hayo na kusema waombaji wote wa kazi walipitia mchakato wa “kuhakiki uthabiti” na kuonyeshwa mifano ya maudhui watakayofanyia kazi.

Kampuni hiyo pia ilisema kabla ya kuanza mradi huo, wafanyikazi waliombwa kukagua na kusaini fomu ya idhini ili kujijumuisha au kujiondoa, suala ambalo lkinaangazia kwamba yale yaliomo yanaweza maudhui makali..

"Kwa washirika waliofaulu ambao walichaguliwa kwa mradi huo, msaada wa kisaikolojia ulitolewa wakati wote wa ushiriki wao," msemaji alisema.

"Sama inadumisha utaalamu kwa wafanyikazi wa afya ambao hutoa huduma za ushauri wa kisaikolojia, ambazo zinaweza kupatikana 24/7, mahali au kupitia mpango wa bima ya afya ya kampuni."

Kwa sasa, Mophat anasubiri kusikia iwapo ombi hilo litasikilizwa bungeni. Na anapojaribu kufanyia kazi afya yake ya akili, anapata faraja kutoka kwa kazi yake kama msimamizi wa data.

Anafikiria kutasaidia kupona kwake: 'Ninajivunia sana. Nilihisi kama askari. Sasa ChatGPT ni salama kwa kila mtu kutumia kwa sababu mimi na wenzangu tuliamua kuchukua gharama yake ‘’, alisema.