Adanganya amefariki ili apate pesa za bima kulipa madeni

    • Author, Shankar Vadishetti
    • Nafasi, BBC

Mfanyabiashara mmoja wa nafaka wa miaka mingi alikuwa na deni. Alipambana sana kujiondoa kwenye mtego wa madeni bila mafanikio.

Ndiposa, alipofirikia kwamba ikiwa atajifanya ameaga dunia na madai ya pesa za bima yakiwasilishwa, atapata pesa za kulipa madeni yake.

Kwa sababu hiyo aliamua kuiba maiti. Lakini jambo hilo lilipobainika, tabasamu lake lilipungua na sasa anasubiri kesi mahakamani.

Jina la mfanyabiashara huyo ni Ketamallu Venkateswara Rao almaarufu Pusaiya. Mkasa wake umezusha mjadala mkubwa huko Andhra Pradesh, nchini India.

Je, polisi waliitatuaje kesi hii?

Kwa mujibu wa polisi, Januari 26 maiti ya mwanaume ilipatikana karibu na shamba la mkulima aitwaye Ketamallu Gangarao wa kijiji cha Veerampalam.

Mwili wake ukiwa umeungua vibaya, karibu na transfoma ya umeme. Viatu na vitu vingine vilivyopatikana karibu na maiti ya mtu huyo, vilitambuliwa kuwa ni vya Ketamallu Venkateswara Rao almaarufu Pusaiah.

Kwa haraka haraka, ilikisiwa kwamba huenda alikufa kutokana na moto wa tansfoma. Polisi wa eneo hilo waliisajili kesi hiyo.

Wakati mkewe na watoto wake wakiomboleza, ghafla Pusaiah alipiga simu. Jambo lililomshtua kila mtu.

Polisi walisema Pusaiya alisema kwa njia ya simu kwamba yuko hai, lakini kuna watu walimshambulia vibaya. Kisha walimtupa karibu na kijiji cha Rajamahendravaram.

Ulikuwa mwili wa nani?

Polisi wanasema Pusaiah alitumia maiti ya mtu mwingine kujifanya amefariki. Kulingana na polisi, Januari 23, Pusaiya aliwasiliana na watu fulani huko Bommur ili apate maiti.

Katika eneo hilo, mwanaume wa umri wa miaka 53 kwa jina la Nellie Vijayaraju alikuwa ameaga dunia huko Old Bommur na familia yake iliuzika mwili katika makaburi ya Old Bommur.

Mnamo tarehe 25, mwili wa Vijayaraju ulifukuliwa na vijana waliotambulika kwa majina ya Vande Srinu na Chira Chinni.

Pusaiah aliwaambia polisi, maiti hiyo ilipelekwa Veerampalam mnamo tarehe 26 asubuhi na kuteketezwa kwa moto kwa kutumia petroli. Kisha watu hao waliondoka na viatu vya Pusaiah na simu vikaachwa kando ya maiti.

Kulingana na ushahidi uliopatikana hapo, wanakijiji waliamini mwili huo ni wa Pusaiya na wakatoa taarifa kwa uongozi wa eneo hilo.

Kwa upande mwingine, watu waliokuwa wakishirikiana na Pusaiah, walikuwa wakimpa taarifa ya matukio yanayoendelea karibu na nyumba yake huko Veerampalam.

Aliposikia kwamba mkewe alikuwa akilia kwa uchungu, Pusaiya alimtuma Talari Subbarao wa kijiji cha Pidingoya kumfariji.

Talari Subbarao alimweleza mkewe kuwa Pusaiya yuko hai na alishambuliwa na baadhi ya vijana wasiojulikana. Kadhalika, aliwapigia simu jamaa zake kuwaeleza kuwa yuko hai.

Siri yafichuka

Pusaiah alidanganya amefariki ili apate pesa za bima, na pia aliiba mwili uliozikwa.

Pusaiya aliwaambia polisi watu wasiojulikana walimvamia na kumteka nyara na kumjeruhi. Lakini kwa kuwa hakuna jeraha lililoonekana, polisi walitilia shaka na kumhoji.

Hatimaye ukweli ukafichuka. Yeye na washtakiwa wengine watatu walikamatwa Januari 30. Pamoja na simu mbili za rununu na gari.

BBC imeelezwa na polisi kuwa washtakiwa wamefikishwa mahakamani na hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah