Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanaume anayedaiwa kufariki miaka 50 iliyopita, amerejea
Joseph Odongo alikuwa na umri wa miaka 30 alipoiacha familia yake katika kijiji cha Riwa eneo la Homa Bay mwaka 1972. Kwa miaka 50 familia yake haikujua alikokuwa hadi tarehe 14 mwezi huu aliporejea akiwa na umri wa miaka 81.
Gazeti la Daily Nation, ambalo liliandika habari hii, lilisema kuwa alirudi na kukuta mali yake ambayo ni moja ya ardhi aliyorithi kutoka kwa wazazi wake ilichukuliwa na watu wa familia ambao wameshafariki.
Alisema sababu ya yeye kukaa mbali kwa miaka 51 ni kutaka kuepusha mzozo kati yake na familia yake.
Odongo ambaye jina lake ni Osir Komollo anasema alikuwa akiishi katika mji wa pwani wa Mombasa kipindi ambacho alikuwa mbali na familia yake na walikuwa wakimtafuta. Alikuwa akiishi katika nyumba inayomilikiwa na raia wa kigeni.
"Kule nilikuwa nasimamia nyumba, na nilihisi faraja nilipokuwa Mombasa, jambo ambalo lilikuwa tofauti nilipokuwa katika mji wangu wa Homa Bay," anasema Odongo.
Watu wenye umri wa miaka 60 katika kijiji hicho hawakuweza kumtambua aliporudi. Chifu wa kijiji aliwauliza wazee wakati mwanamme huyo alipoingia ofisini kwake akitaka kuelezwa ilipo nyumba ya familia yake.
Odongo alisema alichukua uamuzi wa kuhama baada ya mzozo na mmoja wa ndugu zake ambaye kwa sasa ameaga dunia. Wanafamilia wengine pia walikufa wakati akiwa hayupo. Kakake alishtakiwa kwa kuhusika na kifo cha Odongo.
Aliamua kwenda eneo la mbali sana na alipozaliwa ili familia yake isimfuate. Wazazi wake walipofariki na kutalakiana na mkewe, Odongo aliamua kuhama baada ya miezi michache.
Aliiambia familia yake anakwenda katika fukwe za Sikri - ambayo iko kilomita chache kutoka nyumbani kwao. Wana familia walidhani angerudi baada ya siku chache, lakini wiki ziligeuka kuwa miezi, na miezi ikageuka kuwa miaka.
Tangu wakati huo, ikawa vigumu kuwasiliana naye, na ikawa vigumu kujua aliko. Hatimaye familia ilitangaza kwamba amefariki.
Daudi Oketch aliyekuwa jirani anasema - watu wa kijiji hicho walidhani Odongo aliliwa na mamba.
"Mazungumzo ya mwisho na familia yake ni kwamba anakwenda ufukweni. Mwishowe tuliamua kwamba ameliwa na mamba," anasema Oketch.
Shemeji yake mwenye umri wa miaka 90 anasema kuwa Odongo alipokelewa vyema na familia ilialika majirani wote kwenye karamu. Walipoungana tena aliiambia familia yake alikuwa akiishi Mombasa wakati wa kutengana kwao.
Aliongeza kuwa maisha katika eneo la pwani ya Kenya yalikuwa rahisi, alisahau haraka shida alizokumbana nazo alipokuwa akiishi Homa Bay. Mara kwa mara, mtu aliyemfanyia kazi alikuwa akienda Ulaya, na Odongo hubaki peke yake nyumbani.
"Wazo lilinijia mara moja, ambalo ni kurudi kijijini. Niliacha kila kitu nilichokuwa nacho, pamoja na mshahara wangu."
Wakati huo Odongo hakuwa ameoa ingawa aliwahi kuwa na ndoto ya kuoa. Mmoja wa wazee wa kijiji hicho alisema “familia yake imuozeshe ili asiwe mtu wa kukaa peke yake, na apate msaada unaohitajika.”