Mpina aenguliwa rasmi kuwania urais Tanzania

Muda wa kusoma: Dakika 2

Tume huru ya uchaguzi Tanzania (INEC) imeeleza mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina hapaswi kuwania urais Tanzania.

INEC pia imefuta barua yake ya awali iliyohusu urejeshaji wa fomu za uteuzi na kumzuia asifike ofisi ya tume hiyo, huku chama chake kikiri kupokea barua hiyo.

Msajili wa Vyama vya Siasa alitangaza jana kuwa uteuzi wa Mpina kupitia chama chake hicho kipya, haujakidhi matakwa ya kikanuni, kufuatia pingamizi lililowasilishwa na mwanachama wa chama hicho, Monalisa Ndala.

Katika uamuzi uliotolewa Agosti 26, 2025 Msajili alibainisha kuwa Mpina hakutimiza vigezo vya uanachama kwa mujibu wa kanuni za chama, akisema kuwa alijiunga ACT-Wazalendo nje ya muda uliopangwa na hivyo hakustahili kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho.

Kwa mujibu wa malalamiko ya Monalisa aliyoyawasilisha kwa Msajili, mgombea huyo alikiuka sheria ya chama cha ACT Wazalendo kwa kutokuwa mwanachama wa chama hicho siku saba kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza.

Monalisa anasema mwisho wa kuchukua fomu za uteuzi wa mgombea urais ndani ya chama ulikuwa Mei 25, 2025, kabla ya Mpina kuwa mwanachama hivyo mgombea huyo alikuwa nje ya muda kimchakato wa kikanuni za kiuchaguzi.

"Mpina alipata uanachama wa ACT - Wazalendo Agosti 5, 2025, siku moja kabla ya kutangazwa kwenye Mkutano mkuu wa chama hicho wa Agosti 6, 2025, kinyume na kanuni zetu zinavyotaka, hakukuwa na ushahidi wa kikao chochote cha chama kilichorekebisha ratiba rasmi ya kuchukua na kurejesha fomu", ilisema sehemu ya taarifa ya Monalisa kuhusu uamuzi wa Msajili.

Hata hivyo, uongozi wa ACT-Wazalendo kupitia Katibu Mkuu, Ado Shaibu, umetangaza kushtushwa na uamuzi huo na kueleza kuwa tayari wameanza mchakato wa kufungua kesi Mahakama Kuu ili kupinga hatua ya Msajili, wakidai imekiuka taratibu na kuingilia mchakato wa ndani wa chama.

"Chama cha ACT Wazalendo kinaweka msimamo kuwa hakitofuata maelekezo ya Msajili wa Vyama vya siasa juu ya suala hili" inasema taarifa ya ACT na kuongeza kuwa katika kesi itakayofungua itaweka zuio dhidi ya utekelezaji wa uamuzi huu hadi kesi ya msingiisikilizwe.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), uteuzi rasmi wa wagombea urais umefanyikaa Jumatano August 27, 2025.

Wataalamu wa sheria wameeleza kuwa hata kama Tume itakubaliana na maamuzi ya Msajili, Mgombea huyo bado ana nafasi ya kwenda Mahakamani kuomba zuio la utekelezaji wa uamuzi wa Msajili pamoja na Tume hadi pale shauri la msingi litakaposikilizwa.