Watoto wawili waliotoroka wamerudi nyumbani baada ya miaka 13

sd

Chanzo cha picha, NARESH PARAS

Maelezo ya picha, Nita Kumari, mama yao, akionyesha picha za watoto wake
    • Author, Geeta Pandey
    • Nafasi, BBC

Kaka na dada waliondoka nyumbani kwao na kupotea. Wamerudi nyumbani baada ya miaka 13. Mkasa huu unaonekana ni kama filamu, lakini ni kisa cha kweli kilitokea.

Kilikuwa ni kipindi cha kiangazi Juni 2010. Baada ya kuchoka kupigwa na wazazi wao, Rakhi mwenye umri wa miaka 11 na mdogo wake wa kiume Bablu mwenye umri wa miaka 7 waliondoka nyumbani kwao.

Walikuwa na azma ya kwenda kukaa nyumbani kwa bibi yao. Nyumba ya bibi yao ilikuwa umbali wa kilomita moja kutoka nyumbani kwao.

Nini kilitokea?

Kisa hiki kinaanzia mwaka 2010. Katika jiji la Agra, Neetu Kumari na Santosh walikuwa na watoto wawili, Bablu na Rakhi. Wazazi hao walikuwa wanalisha familia yao kwa kufanya kazi za vibarua.

Juni 16, 2010, Neetu Kumari alirudi nyumbani kwake. Alijaribu kutafuta kazi siku hiyo lakini hakupata kazi. Akiwa amekasirika, Neetu Kumari alimpiga mtoto wake.

Rakhi na Bablu walikasirishwa na jambo hilo na kuamua kuondoka nyumbani kwao na kwenda nyumbani kwa bibi yao.

Bablu anasema, "Baba yangu alikuwa akinipiga kwa sababu sikuwa nasoma vizuri. Ndipo Rakhi akanijia na kusema twende tukaishi na bibi. Nilikubali haraka."

Watoto hao waliondoka nyumbani na kupotea njiani. Baada ya kupotea mwendesha rikwama aliwachukua na kuwashusha kwenye kituo cha reli.

Mwanamke anayefanya kazi katika kituo cha watoto yatima aliwaona watoto hao. Naye alikuwa akisafiri katika treni ambayo watoto hao walikuwa wamepanda.

Treni hiyo ilipofika jiji la Meerut, karibu kilomita 250 kutoka nyumbani kwao, mwanamke huyo aliwakabidhi watoto hao kwa polisi. Polisi waliwapeleka kwenye kituo cha watoto yatima cha serikali.

“Tulikuwa tunawaambia tunataka kurudi nyumbani, tulijaribu kuwaeleza kuhusu wazazi wetu, lakini si polisi wala mamlaka ya kituo cha watoto yatima waliotusikiliza wala kutafuta familia yetu,” anasema Bablu.

Kwa muda ndugu wote wawili walikaa katika kituo kimoja cha watoto yatima lakini baadaye walitengana.

Rakhi alipelekwa kwenye kituo cha wasichana kinachoendeshwa na shirika lisilo la serikali na karibu na Delhi. Miaka michache baadaye, Bablu alihamishiwa katika kituo kingine cha watoto yatima cha serikali huko Lucknow, mji mkuu wa jimbo la Uttar Pradesh.

x

Chanzo cha picha, NARESH PARAS

Maelezo ya picha, Neetu Kumari akiwa na watoto wake waliorejea nyumbani baada ya miaka 13

Kaka na dada wakutana tena

fgv

Chanzo cha picha, NARESH PARAS

Maelezo ya picha, Neetu Kumari, watoto wake wawili na mwanaharakati wa kijamii Paras
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati wowote afisa yeyote, mwanaharakati au mwandishi wa habari alipotembelea kituo cha watoto yatima, Bablu alikuwa akiwaambia kuhusu Rakhi. Alitamani kukutana na Rakhi tena.

Mwaka wa 2017. Mwanamke kutoka kituo cha watoto yatima aliamua kumsaidia. Bablu alimwambia kwamba dada yake amepelekwa katika kituo kikubwa cha watoto yatima cha wasichana.

Bablu anasema, "nilikwenda katika kila kituo cha watoto yatima huko Noida na Greater Noida (kitongoji cha Delhi). Niliuliza kama kuna msichana anayeitwa Rakhi, na hatimaye baada ya jitihada nyingi nikampata Rakhi."

Bablu anaongeza, "nataka kuiambia serikali ni ukatili sana kutenganisha ndugu. Kaka na dada wanapaswa kuwekwa kwenye vituo vya karibu."

Baada ya Bablu kumpata Rakhi, walikuwa wakizungumza kwenye simu mara kwa mara. Kila mazungumzo kuhusu nyumbani yanapoibuka, Rakhi alihisi hatoweza kamwe kurudi nyumbani.

Bablu anasema, "alikuwa akisema ni miaka kumi na tatu sasa. Sidhani kama tunaweza kujua mama yetu alipo."

Lakini hakukuwa na shaka akilini mwa Bablu. Siku zote alimwambia, "nimefurahi sana tumekutana tena na ninaamini tutampata mama yetu pia siku moja."

Bablu anasema mahali alipokuwa akiishi, mlinzi na wavulana wakubwa walikuwa wakimpiga mara kwa mara. Alijaribu kukimbia mara mbili, lakini alirudi kwa hofu.

Kwa upande wake Rakhi anasema, shirika lililokuwa likimlea lilimtunza vyema, "walinitunza vizuri. Hakuna mtu aliyenipiga, nilitendewa vyema. Nilisoma shule nzuri, nilipata huduma nzuri za afya."

Juhudi za kuunganishwa na familia zakwama

Mwezi Desemba 20, 2023 mwanaharakati wa haki za watoto katika jiji la Agra, Naresh Paras alipokea simu kutoka kwa Bablu. Bablu akamuuliza, "nimesikia mmeziunganisha familia nyingi. Je, mtanisaidia kuitafuta familia yangu?"

Paras, amekuwa akifanya kazi na watoto tangu 2007, anasema “halikuwa jambo rahisi.”

Watoto wote wawili walikuwa hawakumbuki jina la baba yao na majina yao yalikuwa tofauti kwenye kadi zilizotolewa na serikali. Hawakujua wanatoka jimbo gani au wilaya gani.

Kulingana na rekodi zao katika kituo cha watoto yatima, wamesajiliwa kuwa wametokea jiji la Bilaspur huko Chhattisgarh. Kwa hiyo Paras aliwasiliana na vituo vya watoto yatima na polisi huko Bilaspur, lakini hakufaulu.

Juhudi za kuwatafuta wazazi zaendelea

dc

Chanzo cha picha, NARESH PARAS

Maelezo ya picha, Hati ya malalamiko yaliyowasilishwa na wazazi wa Bablu na Rakhi kwa polisi mwaka 2010

Kisha Paras alipata taarifa muhimu kutoka kwa Bablu. Bablu alipopanda treni, alikumbuka kuona injini mbovu ya treni nje ya kituo. Paras alielewa itakuwa ni kituo cha treni cha Agra Cantonment.

Paras alikwenda kituo cha polisi cha Jagdishpura. Mwezi Juni 2010, Santosh aliripoti kuhusu watoto wake kutoweka katika kituo hicho cha polisi.

Paras alipojaribu kufuatilia familia hiyo, akagundua kuwa familia hiyo haiishi tena mahali pamoja.

Wakati huohuo, Rakhi alikumbuka jina la mama yake na kumwambia Paras kuna alama ya kuungua kwenye shingo ya mama yake.

Katika jiji la Agra, vibarua hukusanyika kila asubuhi katika eneo maalumu katika jiji kwa matumaini ya kupata kazi.

Paras alijaribu kumtafuta mama wa watoto hao katika eneo hilo, lakini hakumpata. Ingawa baadhi ya vibarua walisema wanamfahamu na watamwambia.

Mara tu Neetu Kumari alipojua kuwa watoto wake wamepatikana, alifika kituo cha polisi cha Tadak. Aliwasiliana na Paras.

Walikutana baada ya miaka 13

cv

Chanzo cha picha, NARESH PARAS

Maelezo ya picha, Naresh Paras anampigia simu Bablu simu ya video na Neetu Kumari anaangua kilio

Paras alikutana na Neetu Kumari na kumuonyesha picha za watoto hao na nakala ya rikodi za polisi. Kisha alizungumza na Bablu na Rakhi kupitia video na wote walijuana.

Neetu Kumari aliiambia Paras kuwa, "alijuta kumpiga Rakhi. Nimejaribu sana kuwatafuta watoto wangu.’’

Neetu Kumari alisema, "nilikopa pesa nikaenda huko Patna baada ya kusikia watoto wangu wanaonekana wakiomba mitaani, lakini sikuwakuta. Nilikwenda kwenye mahekalu, misikiti na makanisa kuwaombea usalama watoto wangu."

“Sasa watoto wangu wameungana tena nami na nimepata maisha mapya."

Rakhi anasema, ninahisi kama sinema. Maana sikuwahi kufikiria ningeweza kumuona mama yangu tena. Nina furaha sasa.

Bablu anasema, "ni ajabu sana kwamba Paras alichukua wiki moja tu kuipata familia yangu. Niliwaomba polisi na wafanyakazi wa NGO mara nyingi, lakini hawakuwahi kunisaidia. Nina furaha kukutana na mama yangu sasa."

Mama yake alipomuona Bablu alimsogelea huku akilia na kumuuliza, “mbona uliniacha?” Bablu akasema, “mama sikukuacha, nilipotea.”

Pia Unaweza Kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah