Kufumbua fumbo la maelfu ya makaburi ya dinosaria kwenye 'Mto wa Kifo'

- Author, Rebecca Morelle & Alison Francis
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Makaburi mengi yako chini ya miteremko ya msitu wa jimbo la Alberta, huko Canada. Makaburi haya sio ya wanadamu, ni ya dinosaria (dinosaurs), ambao waliishi mamilioni ya miaka iliyopita, na sio kaburi moja au wawili, ni maelfu ya dinosaria wamefukiwa hapa, baada ya janga kubwa kutokea.
Timu ya wanakiolojia ilikwenda Pipestone Creek kutatua fumbo la miaka milioni 72; juu ya jinsi gani dinosaria walikufa wote kwa pamoja!
Walianza kufichua siri hii kwa mapigo ya nyundo nzito, kwani inahitaji nguvu kubwa kuvunja safu nene ya miamba. Profesa Emily Beamforth, aliongoza timu hiyo.
Timu yao ilipoanza kuondoa tabaka za udongo na vumbi polepole, mifupa ikaanza kuonekana mbele yao, huku mbwa wa Profesa Beamforth, aitwaye Easter, akiwa amesimama akitazama, ili abweke kuwaonya ikiwa dubu atatokea.
Timu ya BBC ilisafiri hadi Pipestone Creek ili kujionea ukubwa wa makaburi haya ya kihistoria na kujifunza jinsi watafiti wanavyokusanya ushahidi.
Mifupa hii yote ni ya dinosaria. Wanyama hawa inasemekana waliishi miaka milioni 72 iliyopita. Walikuwa na urefu wa mita tano na uzani wa tani mbili. Wanyama hawa walikuwa na vichwa vikubwa na pembe tatu.
Msimu wa Uchimbaji

Msimu wa kuchimba, unaoendelea hadi vuli kila mwaka, umeanza. Profesa Beamforth anakadiria kuwa kuna takriban mifupa 300 kwa kila mita ya mraba. Ndio maana eneo hili linaitwa Mto wa Kifo.
Kufikia sasa, timu yake imechimba eneo lenye ukubwa wa uwanja wa tenisi, lakini mifupa hii imeenea kwa umbali wa kilomita moja kwenye mlima.
Wanaakiolojia wanaamini dinosaria hawa walikuwa wakihama kwa msimu kutoka kusini hadi kaskazini wakiwa katika kundi kubwa, walikuwa wakirudi kwenye maeneo yenye joto zaidi baada ya kukaa kwenye maeneo ya baridi.
Wakati huo, hali ya hewa katika eneo hili ilikuwa ya joto zaidi kuliko ilivyo leo, na kulikuwa na misitu minene na malisho au majani ambayo yalitoa chakula cha kutosha kwa wanyama hawa wanaokula mimea.
Mifupa ya maabara

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika eneo jingine. Baada ya mwendo wa saa mbili kwa gari, tulifika Deadfall Hills. Tukatembea kwa miguu katika msitu mnene, kuvuka mto unaotiririka kwa kasi, na kupita kwenye miamba inayoteleza.
Hakuna haja ya kuchimba hapa kwa sababu mifupa mikubwa ipo kwenye miamba kwenye ufuo karibu na ukingo wa mto, na maji yanayotiririka yameisafisha.
Kwa mbali, tunaona mgongo mkubwa, huku mbavu na mabaki ya meno pia yametawanyika kwenye matope.
Mwanaakiolojia Jackson Swider ndiye msimamizi wa makusanyo katika Jumba la Makumbusho la Dinosaur la Philip J. Curie lililo karibu na Grand Prairie, ambapo mifupa ya wanyama hawa wakubwa hupelekwa kusafishwa na kuchambuliwa.
Timu hii imekusanya mifupa 8,000 ya dinosaria kwa miaka mingi na uwanja wa maabara umejaa mabaki ya wanyama hawa; kuna mifupa ya dinosaria ya kila kizazi.
Kuwa na idadi kubwa kama hiyo ni muhimu kwa watafiti kujifunza kuhusu biolojia ya dinosaria, jinsi spishi hiyo ilivyokua, na aina mbalimbali zilizokuwepo.
Wanaweza pia kuchunguza tofauti kati yao ili kuona jinsi dinosaria mmoja anaweza kutofautiana na mwingine. Mfano dinosaria wa eneo hili hawakuwa na pembe tatu, walikuwa na mbili tu.
Janga la ghafla

Profesa Beamforth anasema: 'Tunafikiri hili lilikuwa kundi linalohamahama katika msimu ambao walipatwa na tukio baya, ambalo ama liliharibu kundi zima au sehemu kubwa ya kundi.'
Ushahidi unaonyesha tukio hilo linaweza kuwa ni mafuriko ya ghafla. Labda dhoruba iliyopiga milima, ikashusha mkondo wa maji mkubwa, kung'oa miti na kubeba mawe.
Profesa Beamforth anaamini 'wanyama hawa hawakuweza kukimbia kwa kasi kutokana na wingi wao, walikuwa wazito na hawakuwa waogeleaji wazuri.'

Miamba inayopatikana kwenye eneo hili imebeba mashapo yanayotokana na mtiririko wa maji. Siku hiyo ambayo ilikuwa ya kutisha kwa dinosaria ilikuwa ni mbaya kwao.
Profesa Beamforth anasema: 'Tunajua kila tunapokuja hapa, tuna uhakika wa asilimia 100 tutapata mifupa. Na kila mwaka tunapata kujifunza kitu kipya.'
'Ndiyo maana tunarudi tena na tena, kwa sababu bado tunagundua mambo mapya.'















