Mwamba mkubwa ulioua Dinosaria haukuwa peke yake

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Georgina Rannard
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Mwamba mkubwa (asteroid) ambao uligonga dunia na kuwaangamiza Dinosaria ama Dinosa miaka milioni 66 iliyopita, haukuwa peke yake, wanasayansi wamethibitisha.
Mwamba wa pili, uilianguka baharini karibu na pwani ya Afrika Magharibi na kuunda bonde kubwa katika kipindi hicho hicho.
“Lilikuwa janga," wanasayansi wanasema, na lilisababisha tsunami ya mita 800 kwenda juu na kusababisha bonde kubwa (kreta) katika bahari ya Atlantiki.
Dk Uisdean Nicholson kutoka Chuo Kikuu cha Heriot-Watt, aligundua bonde la Nadir kwa mara ya kwanza mwaka 2022, lakini haikujuulikana ni kwa namna gani shimo hilo lilivyoundwa.
Sasa Dkt Nicholson na wenzake wana uhakika kwamba bonde hilo la kilomita 9, lilisababishwa na mwamba ulioanguka chini ya bahari.
Hawajui tarehe kamili ya tukio hilo, na wala hawajui ikiwa lilitokea kabla au baada ya mwamba mkubwa ulioweka bonde la Chicxulub lenye upana wa kilomita 180 huko Mexico. Ambalo lilimaliza uhai wa dinosa.
Wanasema mwamba wa pili ulitokea mwishoni mwa kipindi cha Cretaceous (miaka milioni 65.5 iliyopita) wakati dinosa walipopotea. Mwamba huo ulipoingia kwenye angahewa ya dunia, ulitengeneza jiwe la moto.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Fikiria mwamba huo ukigonga mji wa Glasgow na wewe uko Edinburgh, karibu kilomita 50. Jiwe la moto la karibu mara 24 ya ukubwa wa Jua – linatosha kuteketeza miti na mimea ya Edinburgh," anasema Dk Nicholson.
Mlipuko mkubwa sana hufuata, kabla ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7 katika kipimo cha Richter.
Kiasi kikubwa cha maji kiliondoka chini ya bahari, na baadaye kilirudi na kuunda alama za kipekee chini ya sakafu ya bahari.
Ni kawaida kwa miamba mikubwa kama hii kuanguka nje ya mfumo wetu wa jua. Lakini watafiti hawajui kwa nini miamba miwili ilipiga dunia katika muda wa kukaribiana.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwamba uliounda bonde la Nadir lenye upana wa karibu mita 450-500, wanasayansi wanaamini uligonga dunia kwa kasi ya kilomita 72,000 kwa saa.
Tukio la karibuni zaidi kama hilo ni la Tunguska la 1908 wakati mwamba wa mita 50 ulipolipuka angani juu ya nchi ya Siberia.
Mwamba wa Nadir ulikuwa sawa na ukubwa wa mwamba wa Bennu, ambao kwa sasa ndiyo mwamba hatari zaidi unaozunguka karibu na dunia.
Wanasayansi wanasema tarehe inayokadiriwa ambapo Bennu unaweza kupiga dunia ni 24 Septemba 2182, kulingana na Nasa. Lakini hayo ni makadirio tu.
Ili kuelewa zaidi bonde la Nadir, Dk Nicholson na timu walichanganua data kutoka kampuni ya kijiofizikia iitwayo TGS.
Mabonde mengi humomonyoka lakini hii limejihifadhi vyema, ikimaanisha kuwa wanasayansi wanaweza kuangalia zaidi viwango vya mawe madogo madogo.
"Hii ni mara ya kwanza tumeweza kuona ndani ya bonde kama hii" anasema Dk Nicholson, akiongeza kuwa kuna mashimo 20 tu ya baharini lakini hakuna hata moja ambalo limechunguzwa kwa kina kama hii.
Utafiti wao ulichapishwa katika jarida la Nature Communications Earth & Environment.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na khaririwa na Seif Abdalla












