Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Nimekataliwa na makumi ya wanaume kwa ajili ya mahari'
Mahari imemepigwa marufuku kisheria nchini India tangu 1961, lakini familia ya bibi harusi bado inatarajiwa kutoa zawadi ya pesa taslimu, nguo na vito kwa familia ya bwana harusi.
Sasa, mwalimu mwenye umri wa miaka 27 katika jiji la Bhopal ameanzisha ombi la kutaka polisi kupeleka maafisa katika maeneo ya ndoa na kufanya msako ili kukomesha "uovu huu wa kijamii".
Gunjan Tiwari (sio jina lake halisi) anaiambia BBC kuwa ombi lake lilitokana na uzoefu wake wa kukataliwa na wanaume kadhaa kwa ajili ya mahari.
Tukio la hivi karibuni zaidi lilitokea Februari wakati babake alikuwa amemwalika kijana mmoja na familia yake nyumbani kwao kwa matumaini ya kumtafutia mwenza wa maisha.
Baada ya wazazi wake kuamkuana na wageni, Gunjan aliingia sebuleni, akiwa amebeba sinia yenye vikombe vya chai ya moto na vitafunwa kwa ajili ya kuwakaribisha wageni.
Anaelezea wakati huo kama "wa kutisha".
"Kila mtu anakutazama, wote wanakupima," aliniambia kwenye simu kutoka nyumbani kwake.
Mipango mingi ya kimsingi ilikuwa imefikiwa ikiwa ni pamoja na jinsi gani Gunjan atatokea mbele ya wageni. Mama yake alikuwa amemchagulia vazi la kijani kibichi kwa sababu alihisi inampendeza binti yake. Pia alimshauri Gunjan asicheke kwani ingevuta hisia kwenye meno yake yasiyo sawa.
Ni mambo ambayo Gunjan anayafahamu sana - baada ya kuyafanya mara sita kwa miaka mingi. Maswali waliyomuuliza pia yalikuwa ya kawaida - kuhusu elimu na kazi yake, na ikiwa angeweza kupika.
Kabla ya kuingia chumbani, alisikia wazazi wake wakimuuliza babake bwana harusi mtarajiwa ni kiasi gani cha mahari alichotarajia. "Tulisikia kwamba wanataka rupia katiti ya milioni tano hadi milioni sita sawa na (dola 61,000 - dola 73,000). Baba yangu alipomuuliza, alitania kwamba 'kama binti yako ni mrembo, tutakuunguzia'," anasema.
Mazungumzo yalipokuwa yakiendelea, Gunjan anasema alifikiri kwamba hawatapunguziwa mahari - wageni walimuuliza kuhusu meno yake yasiyo sawa na alama kwenye paji la uso wake.
Baada ya chai, Gunjan alipopewa dakika chache za kuzungumza faraghani na bwana harusi mtarajiwa, alimwambia kwamba hataolewa kwa ajili ya mahari.
"Alikubali kuwa huo ulikuwa uovu wa kijamii," aliniambia, akiongeza kwamba ilimfanya afikiri kwamba alikuwa tofauti na wengine ambao alikuwa amekutana nao kufikia sasa.
Lakini akina Tiwari waligundua punde kwamba Gunjan alikuwa amekataliwa.
"Mama yangu alikosoa msimamo wangu wa kupinga mahari. Alinikasirikia na hakuzungumza nami kwa zaidi ya wiki mbili," anasema.
Katika kipindi cha miaka sita iliyopita, Gunjan anasema babake amewasiliana na "familia za watu 100-150 wanaohitimu" na kukutana na zaidi ya 40 kati yao. Gunjan mwenyewe amewasilishwa mbele ya wanaume sita kati yao. Na wote, anasema wameangukia kwenye mahari.
"Kwa sababu ya kukataliwa huku nimepoteza imani yangu yote," anasema Gunjan, ambaye ana Shahada ya Uzamili katika hisabati na anafanya masomo ya mtandaoni.
"Ninapofikiria kwa makini, najua sio mimi ninayepungukiwa na kitu, shida iko kwa watu wanaotaka mahari. Lakini mara nyingi najiona nimekuwa dhima kwa wazazi wangu."
Licha ya mahari - kutoa na kukubali - kupigwa marufuku kwa zaidi ya miaka 60, asilimia 90 ya ndoa za Wahindi zifungwa kwa misingi ya mahari- kulingana na utafiti wa hivi karibuni. Malipo ya mahari kati ya mwaka 1950 na 1999 yalifikia robo ya dola trilioni.
Wazazi wa wasichana wanajulikana kuchukua mikopo mikubwa au hata kuuza ardhi na nyumba zao ili kukidhi mahitaji ya mahari na hata hilo si huenda lisimhakikishie bibi arusi maisha ya furaha.
Kulingana na Ofisi ya Kitaifa ya Kurekodi Uhalifu, maharusi 35,493 waliuawa nchini India kati ya 2017 na 2022 - wastani wa wanawake 20 kwa siku - kwa kutoleta mahari ya kutosha.
Wanaharakati wanasema mahari pia ni moja ya sababu za uwiano wa kijinsia wa India - Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu vijusi 400,000 vya kike huavya kila mwaka kwa kutumia vipimo vya uchunguzi wa jinsia kabla ya kuzaa vinavyofanywa na familia zinazohofia kuwa mabinti wangegharimu mahari.
Katika ombi lake lililoelekezwa kwa Harinarayan Chari Mishra, mkuu wa polisi wa Bhopal, Gunjan anasema kuwa suluhu pekee ni kuvamia maeneo ya harusi na kuwakamata wale wanaopatikana wakitoa au kupokea mahari.
"Hofu ya adhabu" itasaidia "kukomesha tabia hii ya kikatili," anaongeza. Wiki iliyopita, alikutana na Bw Mishra kuomba msaada wake katika mapambano yake dhidi ya mahari.
"Mahari ni uovu wa kijamii na tumejitolea kuumaliza. Nimeagiza vituo vyote vya polisi kutoa usaidizi ufaao kwa mwanamke yeyote anayewaomba msaada wao," Bw Mishra aliniambia.
Lakini, anasema, kwamba "polisi wana mapungufu yao, hawawezi kuwa kila mahali na tunahitaji kuongeza ufahamu zaidi juu ya suala hilo, kubadili mawazo".
Mwanaharakati wa haki za wanawake Kavita Srivastava anasema kwa hakika polisi wanaweza kusaidia, lakini kushughulikia mahari ni suala gumu.
"India si nchi inayotawaliwa kimabavu, lakini kuna sheria ya inayopinga mahari na tunahitaji utekelezaji bora wa sheria hiyo."
Mahari, anasema, mara nyingi si malipo ya mara moja kwa familia zenye uchu wa wachumba ambao wanaendelea kudai zaidi hata baada ya ndoa kwa sababu "ni pesa rahisi, njia ya kupata utajiri wa haraka".
Bi Srivastava anatoa mifano ya wanawake ambao wanakabiliwa na unyanyasaji wa nyumbani maishani na hata kufurushwa kutoka kwa nyumba zao za ndoa kwa kutotimiza matakwa yao ya mara kwa mara.
Janga la mahari, anasema, linaweza kupigwa vita iwapo tu vijana wa kiume na wa kike wataanza kuchukua msimamo na kukataa kutoa au kupokea mahari.
Gunjan anasema angependa kuolewa kwa sababu "maisha ni marefu na siwezi kuishi kupeke yangu", lakini ana uhakika kwamba hatalipa mahari.
Lakini huku muda ukizidi kuyoyoma, tamaa ya familia yake ya kutafuta mchumba inazidi kuongezeka.