Kwa nini polisi wa Ufaransa wanatumia bunduki wakati wa ukaguzi wa magari barabarani?

ggg

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Picha ya video kutoka katika tukio la polisi la ufyatuaji risasi Paris

Tukio la polisi kumuua kijana mwenye umri wa miaka 17 wakati akiondoa gari katika kituo cha ukaguzi wa polisi huko Paris ni miongoni mwa mfululizo wa matukio mabaya ya hivi karibuni nchini Ufaransa.

Ilikuwa ni kisa cha tatu cha mauaji kama hayo mwaka huu katika kituo cha ukaguzi wa polisi cha magari na ikifuatiwa na rekodi ya vifo 13 mwaka jana.

Wengi wa waathiriwa ni watu wenye asili ya Kiarabu na Waafrika, shirika la habari la Reuters linaripoti.

Je ni sheria gani ya msingi inayoruhusu kufyatua risasi pale polisi anaposimamisha gari barabarani?

Kwa mujibu wa sheria polisi wa Ufaransa wanaruhusiwa kupiga risasi katika matukio matano kufuatia mabadiliko ya sheria ya 2017.

Hiyo inajumuisha wakati dereva au abiria wa gari wakipuuza amri ya kusimama na wakachukuliwa kuwa hatari kwa maisha ya afisa au usalama wa kimwili, au watu wengine.

Mchunguzi wa haki za binadamu wa Ufaransa amewasilisha madai ya uchunguzi kuhusu mauaji ya Jumanne ya Nahel M, ambayo ni uchunguzi wa sita tangu mwaka jana.

Afisa aliyehusika ameshtakiwa kwa mauaji.

Kwa nini Ufaransa iliongeza matumizi ya bunduki kwa polisi?

Ufaransa sio mgeni kwa machafuko katika viunga vyake - vitongoji masikini vya nje vyenye viwango vya juu vya ukosefu wa ajira na uhalifu - na polisi wanasema wanakabiliwa na viwango vinavyoongezeka vya ghasia.

Mwaka wa 2016, katika nyumba moja nje ya jiji la Paris, afisa mmoja aliungua vibaya na alizirai baada ya kundi la vijana kushambulia gari lake la doria kwa mabomu ya petroli.

Vyama vya muungano wa polisi viliandamana na kutaka majibu makali kutoka kwa serikali.

Katika kujibu, waziri wa mambo ya ndani wa wakati huo Bernard Cazeneuve aliapa kubadili sheria ya matumizi ya bunduki na polisi, na kupitishwa kwa Kifungu cha 435-1 cha kanuni ya adhabu iliyofuata Machi 2017.

Nini kilitokea Nahel M?

Siku ya Jumanne polisi walimpiga risasi na kumuua mvulana mwenye umri wa miaka 17 mwenye asili ya Algeria, aliyetajwa kama Nahel M, alipokuwa akiendesha gari kutoka kwenye kituo cha polisi baada ya kusimamishwa.

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa Nanterre, Nahel alipigwa risasi baada ya kukataa kusimamisha gari alilokuwa akiendesha kufuatia amri ya polisi wawili, ambao baadaye walisema gari hilo lilifanya makosa mbalimbali ya barabarani na kuhatarisha watembea kwa miguu.

Siku ya Alhamisi, Laurent-Franck Lienard alisema mteja wake alitumia bunduki yake "kwa kufuata sheria kikamilifu".

"Hakufanya kazi nje ya mfumo wa kisheria," Bw Lienard alisema.

Wakosoaji wa sheria ya silaha wanasemaje?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka jana utafiti ulionyesha kuwa risasi za polisi zilizosababisha vifo vya madereva wa magari yanayotembea ziliongezeka mara tano tangu sheria hiyo kutekelezwa.

Kati ya watu 39 waliouawa na polisi mwaka 2022, 13 walikuwa madereva waliopigwa risasi kwa msingi wa kushindwa kutii amri.

Walimjumuisha Rayana, msichana aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakaiwa akiwa kama abiria ndani ya gari baada ya dereva kupopuuza amri ya polisi ya kusimama.

Wakosoaji wanasema kuongezeka kwa matukio kama haya ni matokeo ya moja kwa moja ya Kifungu cha 435-1, ambacho wanasema hakieleweki sana kwa sababu kinawaacha maafisa kuamua ikiwa kukataa kwa dereva kufuata sheria kunaleta hatari.

Henri Leclerc, rais wa shirika lisilo la kiserikali la Haki za Kibinadamu la Ufaransa, alisema sheria iliruhusu maafisa "kutozuiliwa" na bunduki zao kwani inawapa "ulinzi wa kisheria" kwa risasi.

Baadhi ya wanasiasa pia wametaka sheria hiyo iangaliwe upya.

Mwanasiasa wa mrengo mkali wa kushoto Jean-Luc Mélenchon ameshutumu kuwa ni kama sheria ya "haki ya kuua".

Je, serikali na polisi wanateteaje sera hiyo?

Waziri wa Mambo ya Ndani Gerald Darmanin amekataa ukosoaji wa sheria ya silaha na kusisitiza kuwa watu wachache wameuawa na polisi tangu 2017.

Hata hivyo, utafiti uliofanywa na chombo cha habari cha uchunguzi cha Basta ulipinga hili, ukisema kwamba wakati watu 27 waliuawa na polisi mwaka 2017, idadi hiyo iliongezeka hadi 40 mwaka wa 2020 na kuongezeka zaidi hadi 52 mwaka wa 2021.

Mapema wiki hii Bw Cazeneuve alitetea sheria hiyo, akisema "haiwapi maafisa hata kidogo ruhusa ya kupiga risasi wakati wowote".

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani aliiambia Le Monde kwamba sheria hiyo haipaswi kulaumiwa kwa ukosefu wa taaluma au mafunzo ya polisi.

Akizungumza na BBC, Naibu Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi cha Unsad-Police Thierry Clair amesema uchunguzi utabaini iwapo silaha hiyo ilitumika kihalali.

"Jambo kuu ni kanuni ya uwiano na aina ya tishio," Bw Clair alisema.

"Kwa mfano, moja ya kesi inarejelea kusimamisha gari ambalo abiria wake wanakataa kufuata na kuleta hatari kwa mtu mwingine ikiwa atajaribu kutoroka.

"Na tukio tunalozungumzia - ambalo silaha ilitumiwa - linaweza kuanguka katika kundi hilo."