Maandamano duniani: Kunani mbona kila pembe ya dunia maandamano?

Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Maandamano

Chanzo cha picha, Getty Images

Inaonekana kila pembe ya dunia leo kuna maandamano yanafanyika, yalifanyika au yatafanyika. Ni maandamano maandamano kila kona.

Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita maandamano yamekuwa yakiongezeka kila uchao. Karibu kila bara kuna nchi kadhaa zimekuwa zikiandamana kwa sababu mbalimbali.

Kuanzia Kenya, Afrika Kusini, Tunisia na Nigeria barani Afrika hadi Ufaransa, Ujerumani, Georgia na Israel huko Ulaya. Peru mpaka Brazil huko Amerika nchi zenye watu kwa jumla karibu mili 800.

Kwa mujibu wa watalaam maandamano ni moja ya njia muhimu ya kufikisha ujumbe wa jambo ama masuala ambayo watu hawakubaliani nayo hasa hasa dhidi ya serikali. Ingawa yapo maandamano mengine machache hufanyika dhidi ya jamii au taasisi zenye maslahi kwa watu wengi.

Hufanyika kwa kuhusisha matembezi ya watu wengi ambayo huanzia mahala fulani wanapokutana kuelekea mahala ama kituo cha mwisho cha kutolea ujumbe.

Maandamano mengine huendana na ghasia na vurugu kubwa zinazosababisha vifo, majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali, uchumi na mazingira. Fahamu nchi zilizo kwenye maandamano na kwanini?

Kenya - 'Hali ngumu ya maisha'

kENYA

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa wiki ya pili sasa Kenya kuna maandamano yanayoongozwa na Raila Odinga, mwanasiasa wa upinzani na kinara wa chama Azimio la Umoja Kwanza.

Maelfu ya wafuasi wake wamekuwa wakiingia mtaani kila Jumatatu na Alhamisi ambapo pamoja na masuala mengine kama kuporwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, wanashinikiza kushughulikiwa kwa hali ngumu ya maisha.

Licha ya ahadi ya Rais William Ruto ya kuwasaidia 'wapambanaji' au hustlers kuboresha maisha yao, nchi hiyo katika kipindi cha mwezi Februari imeshuhudia mfumuko wa bei ukipanda hadi 9.2% kwa mwaka kutoka 9.0% ukilinganisha na mwezi Januari. Oktoba mwaka jana mfumuko ulifika mpaka 9.6% na kuongeza ugumu kwa wananchi wa kawaida.

Maelfu ya Polisi wako mtaani kukabiliana na maelfu ya wafuasi wa Odinga. Mpaka sasa kifo kimoja kimeripotiwa mjini Nairobi, huku majeruhi wakiwa lukuki wakiwemo waandishi wa habari, uharibifu wa mali na ikiwemo ya familia ya rais wa zamani wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta. Inakadiriwa zaidi ya watu 100 wametiwa mbaroni.

Afrika Kusini - 'Rais ajiuzulu na tatizo la ajira

SA

Chanzo cha picha, Getty Images

Machi 20, 2023 mitaa kadhaa ya Afrika Kusini haikuwa na utulivu mkubwa. Wafuasi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) kinachoongozwa na Julius Malema walikuwa wakiandamana na baadhi walikabiliana na Polisi zaidi ya 15,000 waliosambazwa katika miji kadhaa nchini humo.

Maaandamano hayo ni kutaka Rais Cyril Ramaphosa ajiuzulu kwa kuwa ameshindwa kushughulikia masuala muhimu nchini humo ikiwemo tatizo la ajira na rushwa.

Miji ya Sandton, Cape Town na Pretoria kuliendelea kuwa na maandamano makubwa huku karibu watu 50 walikamatwa waliokuwa wanaelekea kwenye makazi ya rais mjini Pretoria baada ya kukabiliana na Polisi waliokuwa wanatumia mabomu ya kutoa machozi.

Tunisia - 'Kupinga utawala wa mtu mmoja'

Tunisia

Chanzo cha picha, Getty Images

Chama cha wafanyakazi chenye nguvu zaidi Tunisia (UGTT) kiliitisha maandamano makubwa nchi nzima, ilikuwa mwanzoni mwa mwezi huu.

Maelfu ya watu walimiminikakatika mji mkuu wa Tunis wakiupinga utawala wa Rais Kais Saied wanaouona ni wa udikteta. Mwaka uliopita alilivunja bunge na kuzua hasira miongoni mwa wananchi.

Utawala wake umeshuhudiwa kukamatwa zaidi kwa wanasiasa wa upinzani, wanachama wa chama cha wafanyakazi cha UGTT, mkuu wa kituo kimoja cha radio na mfanyabiashara maarufu.

Wengi wanamuona ni kama asiyejali wananchi wake na anayetaka kutawala peke yake 'utawala wa mtu mmoja', ingawa mara kadhaa Saied amesikika akisema, kila anachokifanya ni kwa maslahi ya wananchi wake wote na si kundi fulani la watu.

Nigeria - 'Uhaba wa noti'

Nigeria

Chanzo cha picha, Getty Images

Pamoja na mambo mengine Umati watu wenye hasira waliandama na kuchoma matairi moto na kufunga barabara katika miji wa Ibadan, mji mkuu kusini magharibi mwa Nigeria.

Waliandamana kupinga uhaba wa noti za pesa ambao unadhoofisha uchumi wa nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika. Ghasia za maandamano zilisababisha uharibu mkubwa katika miji ya Ibadan, Abuja, Lagos, Kano, Benin City na Nasarawa ambapo Polisi walikabiliana vikali na waandamanaji.

Hili ndilo taifa linaloshuhudia maandamano karibu kila mwaka kwa sababu za kisiasa, kikabilia na kiusalama.

Ufaransa - 'Kupinga kuongezwa umri wa kustaafu'

France

Chanzo cha picha, Getty Images

Tangu Januari kumekuwa na maandamano yenye ghasia katika miji kadhaa ya Ufaransa, hasa Paris yakiongozwa na Vyama vya Wafanyakazi nchini humo. Karibu watu milioni 1 wako mtaani wengi wao wakiwa ni wafanyakazi.

Vyama hivyo vinapinga mageuzi ya mfumo wa pensheni ulioletwa na Rais Emmanuel Macron ambaye pamoja na mambo mengine anataka kuanzia mwishoni mwa mwaka huu umri wa kustaafu kwa wafanyakazi uongezwe kutoka miaka 62 hadi 64.

Macron anasema hilo ni muhimu na kwa maslahi jumla ya nchi hiyo na yuko tayari umaarufu wake kupungua kusimamia hilo huku waandamanaji wakisema mfanyakazi katika umri huo na mazingira ya sasa ya kazi anakuwa amechoka zaidi.

Waziri wa mambo ya nje, Gérald Darmanin, alisema Polisi wapatao 13,000 wamelekwa mtaani kukabiliana na waandamanaji, kati ya hayo 5,500 wako katika mji wa Paris.

Kumekuwa na makabiliano makubwa na ghasia katika miji ya Paris, Lyon, Marseille, Lille, Bordeaux na Rennes..

Israel - 'Kupinga kudhoofishwa kwa Mahakama'

Israel

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Maelfu ya Waisraeli wako barabarani kote nchini humo katika kile kinachojulikana kuwa maandamano makubwa zaidi katika historia ya Israel.

Maandamano hayo yanapinga mipango ya serikali ya kupunguza nguvu za Mahakama ya Juu, ambayo wakosoaji wanasema inadhoofisha uhuru wa mahakama na kutishia demokrasia.

Maandamano hayo yamekuwa yakiendelea kwa wiki miezi mitatu sasa. kuna wakati hadi waandamanaji 500,000 walikuwa waliingia mitaani katika kile gazeti la Haaretz lilichokiita "maandamano makubwa zaidi katika historia ya nchi."

Mjini Tel Aviv pekee, takriban watu 200,000 walisemekana kuandamana ya Jumamosi pili ya mwezi huu na katika mji wa kaskazini wa Haifa, waliripotiwa kulikuwa na waandamanaji karibu 50,000.

Rais wa Israel Isaac Herzog anataka kuwepo kwa muafaka ili kumaliza mzozo, hata hivyo hilo linapingwa kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anayesimamia mageuzi ya mfumo huo mpya wa haki, ikipitishwa sheria kumlinda kutoondolewa madarakani.

Brazil - 'Kupinga matokeo ya Urais'

Brazil

Chanzo cha picha, Getty Images

Wafuasi wa rais wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro, walikabiliana vikali na polisi katika maandamano nje ya Ikulu, mjini mjini Brasilia, Brazil, Ilikuwa Januari 8,2023.

Wafuasi hao waliandamana na kuvamia Majengo ya Ikulu, Bunge na Mahakama. Walikuwa wanapinga kushindwa kwa kiongozi huyo dhidi ya mpinzani wake wa mrengo wa kushoto, Rais Luiz Inacio Lula da Silva.

Uharibu mkubwa umeonekana huku waandamanaji zaidi ya 300 waliswekwa ndani kwa kushiriki maandamano. Ingawa kwa sasa hali imetulia lakini bado kuna upinzani mkubwa kutoka kwa wafuasi wa Bolsonaro.

Peru - 'Rais ajiuzulu'

Peru

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika kipindi cha miezi mitatu sasa, Peru imeshuhudia maandamano na vurugu za kihistoria.

Hakuna utulivu kabisa na maandamano yamezuka baada ya Rais Pedro Castillo kuondolewa madarakani na makamu wake Dina Boluarte, kushika hatamu.

Waandamanaji wanataka Boluarte aliyeingia madarakani Disemba 7, 2022 ajiuzulu na uitishwe uchaguzi mpya lakini mwenyewe haonekani kufanya hivyo akizima maandamano kwa nguvu.

Kati ya Disemba 7 na Disemba 25, 2022 maandamano yalifika katika kiwango cha juu kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika miaka ya hivi karibuni. Zaidi ya watu 60 wanaripotiwa kupoteza maisha mpaka sasa.