Imran Khan: Je, mustakabali wake wa kisiasa umezimwa sasa akiwa jela?

Imran Khan amekamatwa kwa mara ya pili katika kipindi cha miezi kadhaa, lakini wakati huu mapokea yanaonekana tofauti sana. Nini kinaweza kutokea baadaye?

Hakuwezi kuwa na tofauti kubwa kati ya kilichotokea Mei 9 na 5 Agosti mwaka huu.

Wakati wa kukamatwa kwa Imran Khan kwa mara ya kwanza kulisababisha maandamano makubwa mitaani kutoka Peshawar hadi Karachi, majengo yakichomwa moto na jeshi likiwa barabarani, lakini Jumamosi usiku haukuwa tofauti na usiku mwingine wowote wa kawaida nchini Pakistan.

Bw Khan kwa sasa yuko gerezani, amehukumiwa miaka mitatu kwa kutoweka wazi pesa alizopata kwa kuuza zawadi za serikali.

Adhabu hiyo itasababisha kuenguliwa kwake kuwania nafasi ya uongozi kabla ya uchaguzi ujao.

Wito wake wa maandamano ya amani, akiwataka watu wasikae kimya majumbani mwao, haujafanikiwa kwa sasa. Kwa nini?

Waulize mawaziri wa serikali na watasema kwamba ni kwa sababu watu hawataki kumfuata Imran Khan au chama chake, PTI - wasiotaka kuhusishwa na kundi lililohusika na ghasia zilizopita. Huo si ujumbe kutoka kwa wafuasi wa Bw Khan.

Uhusiano wa Imran Khan aliouanzisha nchini Pakistan na mashirika ya kijeshi yenye nguvu ya kisiasa na mashirika ya kijasusi - uliharibika zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Bw Khan alionekana sana na wachambuzi kama mtu aliyeingia madarakani kwa usaidizi wa taasisi hiyo na hatimaye kuipoteza wakati uhusiano huo ulipoyumba.

Harakati za kujinyonga?

Tangu wakati huo, badala ya kusubiri kwa utulivu hadi uchaguzi ujao ufike, ameendelea kuukosoa uongozi wa jeshi hilo. Majengo ya jeshi yaliposhambuliwa kufuatia kukamatwa kwa Bw Khan mwezi wa Mei, wanajeshi walieleza kuwa hawakuwa na namna ya kuwavumilia wale waliohusika.

Baada ya tukio hilo kilichofuata kikaacha chama cha Imran Khan kikiwa kimedhoofika.

Wafuasi wake walikamatwa kwa maelfu, na wengine watahukumiwa katika mahakama za kijeshi, licha ya kilio kutoka kwa Mashirika ya kutetea haki za binadamu kwamba mfumo huo wa mahakama za kijeshi haufai kutumika kwa raia.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Pakistan vimetuambia kwamba kuanzia mwishoni mwa mwezi Mei - baada ya wamiliki wa vituo vya televisheni kukutana na jeshi - waandishi wa habari hawakuruhusiwa tena kutaja jina la Bw Khan, kuonyesha picha zake au hata kuandika jina lake kwenye vyombo vyao.

Kwa bahati mbaya, wafuasi wengi wa hapo awali walituambia kwamba walikuwa wameacha kuchapisha kuhusu chama chake cha PTI au kiongozi wake kwenye mitandao ya kijamii, kufuta machapisho yao na kutotazama tena matangazo yake ya umma, wakihofia kufuatiliwa.

Serikali imeambia BBC kwamba haiwashikilii waandamanaji wa amani. Hata hivyo, wanahabari wa BBC Urdu waliwaona wafuasi wa PTI waliokusanyika nje ya nyumba ya Bw Khan huko Lahore Jumamosi alasiri wakibebwa na polisi. Haijabainika wazi kama wanashikiliwa rasmi kwa utaratibu uliopo.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, afisa mmoja wa Polisi aliambia BBC kwamba wamewakamata takriban wafuasi 100 wa PTI. Alisema kuwa kikosi hicho kimeambiwa kukaa macho na kuhakikisha hakuna wafuasi wa Imran Khan wanaoanza kukusanyika.

"Nadhani muitikio kutoka kwa ukandamizaji wa kikatili umewatia hofu wafuasi wa Khan kuandamana," anasema Michael Kugelman, mkurugenzi wa Taasisi ya Wilson Center think tank huko Washington.

"Kwa kweli nadhani wafuafi wa kumsaidia hawakuwa tayari kujiweka hatarini kama tulivyoona Mei 9.

"Kwa maana moja, wanajeshi wamecheza vyema jambo hili. Walitumia mbinu hizi za kikatili ambazo zilizua hisia kubwa na kali zaidi kutoka kwawafuasi wa Khan."

Timu ya wanasheria wa Imran Khan wameweka wazi kuwa wanakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kumfunga jela.

Mtihani wa mitaani na kupiga kura

Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, mawakili wake wameweza mara kwa mara kupata afueni ya muda kutoka kwenye Mahakama tofauti - afueni ya kuchelewesha kesi badala ya kuziondoa baadhi ya kesi mbaya zaidi mahakamani.

Haijulikani ikiwa hii itaendelea. Bw Khan aliachiwa baada ya kukama kukamatwa mwezi Mei, lakini katika mazingira tofauti kabisa ya kisiasa.

Imran Khan ni mmoja wa viongozi kadhaa wa zamani wa Pakistani ambao wameishia katika mahakama za nchi hiyo - wengine ni Nawaz Sharif, Benazir Bhutto na dikteta wa kijeshi Pervez Musharraf, hao ni wachache katika miongo ya hivi karibuni.

Bw Khan aliwafunga wapinzani wake kadhaa wa kisiasa alipokuwa waziri mkuu.

Wanasiasa wa Pakistani mara nyingi watasema kuwa mfumo wa haki umechochewa kisiasa dhidi yao, huku ukihalalishwa dhidi ya upinzani wao.

Iwapo Imran Khan atasalia kutostahili kushikilia wadhifa wa umma, kuna maswali makubwa kuhusu nini kitatokea kwa chama chake.

Bw Khan ametuambia hapo awali kwamba PTI itaishi na kustawi, iwe anaweza kuchaguliwa au la. Lakini hilo halina uhakika kwa sasa.

"Swali kubwa linalofuata, kutokana na uchaguzi unaokuja, ni jinsi gani uongozi uliosalia wa PTI utajaribu kuhamasisha?" Anasema Bw Kugelman.

"Je, watajaribu kuwatoa wafuasi wao mitaani, hilo litafanikiwa? utakuwa mtihani mzuri."

Chama cha PTI ni kama chama binafsi cha Bw Khan, kinamuhusu zaidi yeye. Hata nembo yake iliyochapishwa kwenye fomu za kupigia kura kuna alama ya mpira wa kriketi, ishara ya kupongeza maisha ya awali ya Bw Khan kama mchezaji wa kimataifa wa kriketi.

Wengi wa viongozi wakuu wa kisiasa waliomzunguka Bw Khan mapema mwaka huu wamekihama chama chake. Wengine wanaohusika na chama chake wamejificha wakikwepa kukamatwa.

Haionekani kama itakuwa rahisi kwa chama chake kuendesha kampeni ya kisiasa yenye ufanisi.