Pacha wa Canada wavunja rekodi ya kuzaliwa kabla ya wakati wao

Chanzo cha picha, GUINNESS
Pacha, kaka na dada wa Canada waliozaliwa wakiwa na wiki 22 wametajwa na Kitabu ch rekodi za Guinness kama pacha waliozaliwa kabla ya muda wao kufika zaidi duniani.
Adiah na Adrial Nadarajah walizaliwa wakiwa na siku 126, na kupita rekodi ya awali ya siku 125 iliyowekwa mapema mwaka 2018 na mapacha katika jimbo la Iowa la Marekani.
Ikiwa watoto hao wangezaliwa hata saa moja mapema zaidi ya wiki 22, shughuli ya kuokoa maisha yao hata haingejaribiwa na hospitali, Guinness inasema.
Muda ambao mimba inakuwa iko tayari kawaida ni wiki 40, na hilo lilifanya watoto hao kuzaliwa kabla ya wakati kwa wiki 18.
Mama Shakina Rajendram alisema kwamba alipoanza uchungu katika wiki 21 tu na siku tano, madaktari walimwambia kwamba watoto "hawakuwa na uwezo wa kuishi" na walikuwa na "nafasi 0% ya kuishi".
Ilikuwa mimba yake ya pili, baada ya kupoteza mimba yake ya kwanza miezi michache iliyopita katika hospitali hiyo hiyo karibu na nyumbani kwao huko Ontario.

Chanzo cha picha, GUINNESS
Baba Kevin Nadarajah alisema kuwa hospitali iliwaambia hawataweza kusaidia na ujauzito huo ambao watoto walizaliwa mapema zaidi, na kumwacha macho usiku kucha akisali na "uso ukibubujikwa na machozi".
Hospitali nyingi hazijaribu kuokoa maisha ya watoto waliozaliwa kabla ya wiki 24 hadi 26.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini kwa bahati nzuri, wanandoa hao waliweza kuhamia Hospitali ya Mount Sinai huko Toronto, ambayo ina kitengo maalum cha uangalizi wa watoto wachanga.
Katika siku ya pili ya uchungu wa Bibi Rajendram - wiki 21 na siku sita za ujauzito - aliambiwa kwamba ikiwa watoto wangezaliwa hata dakika chache kabla ya wiki 22, wangeachwa wafe.
Licha ya kutokwa na damu nyingi, alisema alijaribu kila awezalo "kuwazuia watoto ndani ya tumbo" kwa saa chache zaidi.
Maji yake hatimaye yalikatika dakika 15 baada ya saa sita usiku. Chini ya saa mbili tu baada ya kuingia wiki 22 tumboni, watoto walizaliwa.
Adiah na Adrial sasa wameishi hadi kufikisha umri wa mwaka mmoja, licha ya matatizo makubwa ya kiafya wakati wa awali.
"Tulitazama watoto karibu kufa mbele ya macho yetu mara nyingi," Bi Rajendram alisema. Wakati bado wanafuatiliwa kwa karibu na madaktari, ndugu hawa "wanaendelea vizuri".
Mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati zaidi alikuwa Curtis Means wa Alabama, ambaye alizaliwa akiwa na wiki 21 na siku moja.

Chanzo cha picha, GUINNESS















