Olena Zelenska: Mke wa Rais wa Ukraine aeleza alichofanya mumewe asubuhi ya kwanza Urusi ilipoivamia Ukraine

zelensky

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Olena Zelenska akiwa na mumewe Volodymyr Zelensky

Mke wa rais wa Ukraine, Olena Zelenska, amefanya mahojiano ya nadra kwa vyombo vya habari vya nchi yake huku akionekana na mumewe, Rais Volodymyr Zelensky, kwa mara ya pili tangu Februari, wakati vita vilipoanza.

Zelenska alifichwa mahali pa siri ili kumweka salama.

"Familia yetu imegawanyika kama familia nyingine yoyote ya Kiukreni," alisema katika mahojiano.

Mwandishi aliuliza swali: "Je, mapigano yalikuweka mbali na mumeo?"

"Hapana, hakuna mtu anayeniondoa kwa mume wangu, mapambano hayawezi hata kufanya hivyo," Zelenska alijibu.

"Lakini ndiyo maisha ya kazi yake yalivyo, na sisi na familia yake hatuoni tatizo, hatujaonana kwa muda wa miezi miwili na nusu, tunazungumza kwa simu tu, sasa tumeshaonana. Sasa tuna nafasi, imekuwa rahisi kwetu kuwa pamoja."

"Je, mmepata nafasi ya kukutana kimapenzi?" Aliulizwa na mwandishi.

"Ndiyo, katika mkutano wa televisheni. Asante, "alijibu mke huyo wa rais, ambaye ana watoto wawili: Oleksandra na Kyrylo.

Zelensky

Chanzo cha picha, Getty Images

'Niliamka nikipiga kelele' Katika siku ya kwanza ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mnamo Februari 24, Zelenska alisikia milio ya sauti isiyojulikana kutoka nje, kama ilivyo kwa watu wengine katika nchi yake.

"Niliamshwa kutokana na kelele hizi na kupiga mayowe," alisema.

"Kulikuwa na giza kidogo. Niliona kwamba Volodymyr (Rais) hakuwa amelala kwenye kitanda changu karibu nami. Kisha alikuwa tayari amevaa na hakuwa amevaa skafu. Nilimuuliza nini kinaendelea akasema 'vita imeanza'.

"Siwezi kufikiria jinsi nilivyohisi ... mshtuko na hofu niliyohisi. Aliniambia hivyo na akaondoka, na kisha hatukuonana kwa muda mrefu."

Rais wa Ukraine, ambaye alikuwa ameketi karibu na mkewe wakati wa mahojiano, alisema vita vya Ukraine vinaweza tu kutatuliwa kwa njia ya diplomasia.

"Nimefurahishwa sana na hili. Kuna mambo ambayo hatuwezi kufanya hadi tuketi kwenye meza ya mazungumzo, kwa sababu tunataka kila kitu kirudi kwetu, na Urusi haitaki kurudisha chochote," Zelensky alisema.

Olena Zelenska

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Olena Zelenska

Vita nchini Ukraine sasa vinakaribia miezi mitatu tangu kuanzishwa, na haijulikani vitaisha namna gani na lini.

Wanajeshi wa Urusi wanaendelea na mashambulizi yao katika eneo la mashariki mwa Ukraine la Donbas, huku wakijaribu kufikia mipaka ya mikoa ya Donetsk na Luhansk.

Jeshi la Ukraine linasema makombora ya mizinga ya Urusi yalipiga majengo 45 siku ya Jumapili pekee.

Mwishoni mwa wiki, mpatanishi mkuu wa Ukraine, Mykhailo Podolyak, aliondoa uwezekano wa kusitisha mapigano.

Podolyak alishutumu jeshi la Urusi kwa kufanya mashambulizi zaidi dhidi ya vituo vyake vya kijeshi.

Rais Volodymyr Zelensky

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Volodymyr Zelensky

Baada ya kuuteka mji wa pwani wa Mariupol, majeshi ya Urusi yaliendelea na mashambulizi yao dhidi ya eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine.

Inaaminika kuwa sasa wanajiandaa kuchukua miji ya Sloyansk na Severodonetsk.

Siku ya Jumapili, Zelensky alirefusha hali ya hatari nchini Ukraine, ambayo itaendelea kwa miezi mingine mitatu, hadi Agosti 23.

Sheria hiyo inaeleza kuwa wanaume wenye umri wa kati ya miaka 18 na 60 lazima wabaki nchini ili kushiriki katika vita.