Mzozo Ukraine: 'Mtoto wangu anaficha mikate, akihofia chakula kukosekana'

Makumi na maelfu ya raia wamebaki wamekwama katika mji wa Mariupol wa Ukraine uliozingirwa, bila umeme, maji ya bomba au gesi.
Juhudi nyingi za kufungua njia za usambazaji wa misaada na kuwahamisha wakazi zimeshindikana. Kwa wale ambao wamefanikiwa kutoroka, mateso hayajaisha, haswa kwa watoto wao.
Kitu cha kwanza walichokifanya ni kununua mikate, soseji na maji.
Nadia Denysenko na watoto wake walikuwa wametoroka baada ya wiki tatu huko Mariupol, chini ya kuzingirwa na kushambuliwa mara kwa mara, wakiishi katika nyumba yao yenye baridi kali ambapo madirisha yalivunjika baada ya mlipuko kutokea eneo la karibu.
Kwa siku nyingi walikuwa na chakula kidogo sana, na karibu hakuna chochote cha kunywa.
"Tulifurahi sana kuwa na maji ya chupa. Tuliyamaliza kwa sekunde chache," Nadia alisema, akikumbuka wakati alipofikiria usalama wa jamaa na wanawe wawili, wenye umri wa miaka 14 na mitano, na binti wa miaka 12.
"Vita vilipoanza, mwanangu mdogo alisema 'Mama, ningependa kuwa na mkate'."
Simulizi zao nyingine za kustaajabisha huku kukiwa na janga la ajabu.
Ndani ya Mariupol, walikaa nyuma ya kuta.
Usiku ulikuwa kwenye handaki. Kwa kawaida waliamka saa kumi na moja. Milipuko mikubwa, wakati mwingine ikiwa mbali, wakati mwingine ikiwa karibu, ilikuwa si rahisi kulala.
"Ilikuwa kuzimu. Kuzimu tu," Nadia, ambaye ana umri wa miaka 39 na alikuwa akifanya kazi katika duka kubwa mjini, alisema. "Ulikuwa ukiishi bila kujua kama ungeamka ukiwa hai asubuhi."
Mariupol imeona uvamizi mbaya zaidi wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Maelfu wamekufa huku majeshi ya wavamizi yakiuzingira mji huo, na kuushambulia bila huruma kutoka angani, ardhini na pia kutoka baharini.
Mtaa baada ya mtaa, jengo baada ya jengo, majengo mengi yakiwa katika magofu.
"Tulipigwa makombora sana. Hawakujali chochote... Mwanangu aliendelea kuuliza, 'Kwa nini kuna milipuko?'," Nadia alisema. "Ningemwambia, 'Usijali mwanangu. Ni fataki tu."

Wakati walipokuwa katika mji huo, majirani walipika chakula kidogo walichokuwa nacho kwenye jiko la mtaani.
"Mara nyingi tulikaa nje kwa sababu ndani kulikuwa na joto," Nadia alisema.
Katika siku zao mbili za mwisho huko, hawakuwa na chochote cha kula. Hata unga au oatmeal.
"Haijalishi kama mtu ulikuwa na pesa au la, hakukuwa na chakula kilichobaki mjini."
Katika moja ya jitihada zao za kukimbia, walikwenda mahali ambapo magari yalikuwa yamekusanyika, wakiamini kuwa ni mahali pa uhamisho. Walikuja kushambuliwa.
"Lilikuwa jambo ambalo limepangwa," alisema.
Walinusurika tu, Nadia alisema, baada ya mwanaume kumsukuma yeye na watoto wake "kama watoto wa mbwa" ndani ya jengo lililoharibiwa, ambapo walidhani watalindwa.
"Tulipoondoka," alisema, "tulishuhudia jambo baya." Gari lilipuliwa na . Dereva, askari aliyekuwa akijaribu kuitoa familia yake nje ya jiji, alijeruhiwa kichwani.
Yeye na wengine walimleta kwenye chumba cha chini cha ardhi, ambapo msichana, ambaye hakuwa daktari, alimshono kwa kutumia sindano na uzi wa kawaida.
"Baada ya kuona haya yote tulirudi nyumbani na mwanangu mdogo akaniuliza, 'Mama, kwa nini wanataka kutuua?'," Nadia alisema.
"Ninaweza kumwambia nini? Sijui kwanini."

Siku chache baadae, tarehe 17 Machi, tulifanikiwa kuendesha gari mpaka nje ya mji kwa kutumia gari binafsi.
Kwanza, walifika katika kijiji cha Mangush. Na kuelekea Berdyansk, ambako kupo chini ya mamlaka ya Urusi.
Kuanzia hapo, walipanda basi mpaka Zaporizhzhia. Barabarani kulikuwa na vituo vingi vya kukaguliwa na wanajeshi wa Urusi.
"Walitukagua, haswa wanaume ,simu zetu," Nadia alisema. Kwa kufahamu kuwa hayo yatatokea, alikuwa amefuta picha zote tangu alipokuwa Mariupol. "Wakati tuipoondoka mjini , nilikuwa mchafu ,nikiwa na matope meni, nilikuwa sijaoga.
Wakati tulipokosa kitu chochote cha kunywa, huwezi kuwaza juu ya kuoga."
Iliwachukua siku tano kusafiri kutoka Zaporizhzhia mpaka Lviv, magharibi mwa Ukraine ambalo halijapata milipuko mingi ya Urusi.
Miongoni mwa ishara ambazo zilijionesha ni kuwa taifa hili liko kwenye vita, ving'ora vikisikika mara kadhaa kwa siku.
"Tuko salama na tunaweza kununua chakula, lakini bado mwanangu anaficha mikate na pipi.
Anaficha katika maeneo tofautitofauti katika nyumba ambako tunaishi," alisema.
Alimuuliza "Kwanini amefanya hivyo?"
"Alisema, 'Hivyo nitakuwa na kitu cha kula kesho.'"

Nadia anadhani watoto wake wataweza kukabiliana na hali hiyo wanayokutana nayo .
Alisema binti yake , ambaye hakutaka kuhojiwa, alikuwa anaongea sana lakini bado alikuwa hajapata marafiki katika mji mpya.
Anatamani kurudi Mariupol siku moja, vita ikiisha na mji kujengwa tena.
"Wameharibu mji wetu . Hakuna chochote kilichobaki ... Kila kitu kilikuwa kinaenda vizuri na maendeleo yanaenda vizuri , yani kila kitu kilikuwa kinaenda sawa," alisema.
Kitu pekee ambacho hatukuwa nacho, Nadia alisema, ni McDonald.
"Yani sielewi kwanini haya yanatokea.Kwanini wanafanya hivi?"














