Tanzania: Wafungwa wazee na wagonjwa wapewa kipaumbele zaidi kuachiwa huru

Waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania, George Simbachawene

Chanzo cha picha, Serikali ya Tanzania

Maelezo ya picha, Waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania, George Simbachawene

Waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania, George Simbachawene ametoa taarifa juu ya wafungwa walioachiwa huru katika sherehe za miaka 60 ya uhuru wa Tanzania bara.

"Kwa mara ya kwanza Rais amewaachia watu wenye umri mkubwa na wanaougua kwa muda mrefu ila ni kwa wao kutorudia kufanya makosa,"Waziri Simbachawene amesema.

Tanzania imekuwa na utaratibu wa kuwaachia huru wafungwa katika siku ya maadhimisho ya Sherehe za Uhuru.

Katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru Disemba 9 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaachia huru wafungwa 5704.

Hata hivyo, msamaha wa mwaka huu ni wa aina yake kwa kuwa watu wengi walioachiwa huru ni wazee na wasio na uwezo wa kufanya kazi.

Wafungwa walioachiwa huru walizingatiwa vigezo vifuatavyo;

  • Wawe wametumikia robo ya kifungo chao
  • Wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu na wasio na uwezo wa kufanya kazi
  • Wafungwa wote wa kike walioingia na mimba gerezani au waliingia na watoto wanaonyonya
  • Wafungwa wazee wenye miaka 70 au zaidi
  • Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili
  • Wafungwa waliokaa gerezani kuanzia miaka 20 na kuendelea na wameonesha uadilifu.

Aidha msamaha huo haujahusisha wafungwa wenye kutumikia adhabu ya kunyongwa, na wenye makosa ya kujaribu kuua au kujiua na kuua watoto wachanga.

Hatahivyo wafungwa wa vifungo vya nje pia hawajaachiwa huru.

Pingu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru DIsemba 9 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaachia huru wafungwa 5704.

Wafungwa waliopatikana na hatia ya makosa ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, rushwa na ufisadi pamoja na kutumia vibaya madaraka yao msamaha huo haujawahusu.

Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya biashara za binadamu, usafirishaji wa madawa za kulevya, kuwapa mimba wanafunzi na kuwatesa watoto.

Wafungwa wanaohusika na nyara zozote za serikali.

Waziri Simbachawane amezungumzia pia juu ya uzoefu wa mwaka jana wa wafungwa walioachiwa huru kurudi kufanya matukio ya uhalifu.

"Mwaka jana kuna kipindi kati ya watatu waliochiwa huru wawili waliofanya matukio ya wahalifu ni wale walioachiwa katika msamaha wa rais".

Aidha amesisitiza kuwa gerezani si mahali pa kudumu kuishi hivyo utaratibu huo ni muhimu kufuatwa.

Wanapokuwa gerezani wafungwa huwa wanapata fursa ya kupata mafunzo ya kurekebishwa tabia.

Lakini sheria pia inaruhusu kuwakamata tena wahalifu hao na kuwaweka gerezani.