Hizi ni dhana 6 potofu kuhusu Dinosaria zinazoendelea kuwachanganya watu

    • Author, Fernando Duarte
    • Nafasi, BBC World Service

Uelewa wetu kuhusu dinosaria umetokea mbali tangu viumbe vya kwanza vya aina hiyo kuelezewa katika fasihi ya kisayansi katika Karne ya 19.

Lakini wanapaleontolojia hadi leo bado wanajaribu kuondoa hadithi kuhusu viumbe hawa wa mapema katika sayari yetu. Jambo hili limefanywa kuwa gumu zaidi kutokana na uwakilishi usio sahihi wa dinosaria katika tamaduni maarufu - ikiwa ni pamoja na filamu yenye mafanikio makubwa ya Jurassic Park.

Hapa kuna baadhi ya maoni potofu ambayo bado yanaendelea

Je! dinosaria wote waliuawa na sayari ndogo maarufu?

Takriban miaka milioni 66 iliyopita, dinosaria walikuwa na siku mbaya sana: sayari kubwa, iliyokadiriwa kuwa na kipenyo cha kilomita 10, ilipiga Duniani. Athari yake, iliacha shimo kubwa lkwenye rasi ya Yucatan huko Mexico, iliosababisha wengi kutoweka.

Walakini, wanasayansi wanasema kwamba ni aslimia 75% tu ya wanyama wa dunia walikufa. Na baadhi ya dinosaria walikuwa miongoni mwa walionusurika.

"Ingawa dinosaria wengi walikufa wakati sayari ilipogonga dunia, kundi muhimu la dinosaria wadogo sana na wenye manyoya waliendelea kuwepo na bado tunawaona leo," Profesa Paul Barrett, mtaalam wa historia ya asili ya London (NHM), aliambia. BBC.

"Ndege ni washiriki wa moja kwa moja wa kundi moja la dinosaria."

"Wao ni dinosaria hai na kwa idadi ya aina/spishi za ndege walio hai, kuna aina nyingi zaidi za dinosaria leo kuliko ilivyokuwa miaka milioni 66 iliyopita."

Je, unaweza kujificha kutoka kwa Tyrannosaurus Rex kwa kusimama tuli?

'Tyrannosaurus Rex' ndiye nyota wa onyesho katika filamu ya kwanza ya fasihi iliyofanikiwa sana ya Jurassic Park, iliyotolewa mwaka wa 1993, ikishiriki katika matukio mengi ya kukumbukwa ambapo iliwatia hofu wahusika wakuu ambao ni binadamu.

Lakini filamu hiyo ilionyesha T-Rex kama mnyama asiyeona vizuri ambaye angeweza tu kugundua mawindo yanayoweza kutokea ikiwa mnyama huyo anasonga ama tembea.

Kwa asili, tabia kama hiyo iko katika wanyama kama vile amfibia, lakini Profesa Barrett anasema kwamba haikuwa hivyo kwa wanyama wanaowinda wanyama wengine.

"Dinosaria walikuwa na uwezekano wa kuwa na uwezo wa kuona zaidi. Utafiti mmoja uliofanyika miaka 15 iliyopita kwa kweli ulipendekeza kwamba T-Rex pengine alikuwa na maono bora zaidi ya mnyama yeyote ambaye amewahi kuishi."

"Kusimama bila kutigishika mbele ya T-Rex pengine itakuwa moja ya mambo ya kipumbavu unayoweza kufanya."

Je, T- Rex anaweza kulishinda gari linalotembea?

Vile vile, filamu inaonyesha tukio ambalo T-Rex analipita gari linalosonga mbele.

Kwa kweli kuna tafiti ambazo hapo awali zilikadiria kuwa mwindaji huyu wa kutisha anaweza kukimbia kwa kasi ya hadi kilometa 50km kwa saa. Uigizaji wa hivi karibuni zaidi na wa hali ya juu zaidi unapendekeza mwendo wa kawaida wa karibu wa kilometa 20 hadi 29 kwa saa.

"Pia ni muhimu kukumbuka kwamba jambo moja ni kasi ya juu unayoweza kufikia na nyingine ni kasi nzuri unaweza kukimbia kwa muda mrefu," Dk Mariana Di Giacomo, mhifadhi katika Jumba la Makumbusho la Historia ya Kitaifa la Chuo Kikuu cha Yale, Peabody, anasema.

"Wakimbiaji wa mbio ndefu 'marathon' hawakimbii haraka kama wakimbiaji wa mbio fupi kwa sababu kuendeleza kasi hiyo ya kasi kwa muda mrefu ni ngumu kwa miili yetu."

"Labda T-Rex angeweza kukimbia haraka kwa mbio fupi, lakini hiyo isingetosha kulishinda gari linalotembea," anaongeza.

Je, tunaweza kuumba dinosaria?

T-Rex aliondoka katika ulimwengu huu miaka mamilioni kabla ya kuanza kwa aina/spishi zetu, na hatuna uwezekano wa kukutana tena wakati wowote hivi karibuni - kinyume na kinachoonyeshwa kwenye filamu ya Jurassic Park, wanasayansi wanasisitiza kwamba dinosaria haziwezi kuundwa ama kuumbwa upya .

Sababu kubwa ni kwamba DNA ya dinosaria haizeeki vizuri.

"Haishi kwa muda mrefu sana, kama tunavyojua," Profesa Barrett anaelezea.

"DNA ya zamani zaidi tunayojua katika rekodi ya vizazi ina umri wa miaka milioni mbili. Na kwamba DNA ni vipande vya bakteria, udongo, kuvu na vitu kama hivi."

Kwa wanyama, data ya zamani zaidi ya maumbile inayopatikana ni ya viumbe waliokufa hadi miaka 50,000 iliyopita, Profesa Barrett anasema.

Dk Di Giacomo anakubali, akisema kwamba hata mafanikio ya kisayansi katika suala la 'genetics' ya dinosaria haimaanishi mafanikio katika uundaji wa wake.

"Aina za uundwaji ambazo ziko mbali sana na sisi katika wakati wa kijiolojia ni ngumu sana kwa sababu kuna vigezo vingi visivyojulikana."

Pia anaibua masuala ya kimaadili yanayoweza kutokea:

"Filamu kama vile Jurassic Park na Jurassic World zinatuonyesha sababu zote za kutofanya hivyo, ambazo zinalenga zaidi kuonyesha wanadamu wanaoguswa na matokeo yake. Lakini kuna mazungumzo kidogo juu ya ukatili wa kuleta wanyama hawa katika ulimwengu ambao hauonekani kama walivyokuwa kwa wakati wao."

Dinosaria walikuwa "viumbe wajinga"?

Dk Di Giacomo anaeleza kwamba kukua kwa teknolojia kumewapa wanasayansi rasilimali zaidi ya kuelewa jinsi dinosaria walivyoishi na na tabia zao.

"Sio dinosaria wote walikuwa na akili sana na sio dinosaria wote walikosa akili."

"Walikuwa na akili ya kuwafanya kuishi ulimwenguni."

Profesa Barrett anaongeza kwamba baadhi ya dinosaria walikuwa "wajanja na wenye akili ", yaani wale wadogo wala nyama.

"Baadhi yao huenda walikuwa wakiishi usiku ili kuepuka ushindani na wanyama wakubwa. Ikiwa ndivyo, ni wazi unahitaji ubongo mkubwa ili kukabiliana na taarifa za ziada unazohitaji, pamoja na hisia bora za kusikia, kuona na kunusa."

Je! Dinosaria walikuwa wazazi wa ajabu?

Kwa zaidi ya karne moja, dinosaria walifikiriwa kuwa ni viumbe wakatili na wapweke ambao hawakuweza kuwa wazazi wazuri. Kisha, katika miaka ya 1970 na 1980, uvumbuzi ulifichua tabia ngumu zaidi ya kijamii.

Dinosaria anayekula mimea anayeaminika kuishi miaka milioni 77 iliyopita hata amepewa jina la Maiasaura - ambalo linamaanisha "mjusi mama mzuri" kutoka kwa maneno ya Kigiriki na Kilatini.

Utafiti wa hivi karibuni, uliochapishwa katika jarida la Scientific Reports Oktoba mwaka jana, ulienda mbali zaidi na kuonyesha kwamba dinosaria walioishi miaka milioni 193 iliyopita tayari walikuwa wamejipanga katika makundi na kulea watoto wao wanaoanguliwa.

"Siku hizi tuna ufahamu bora wa dinosaria na tunajua kwamba angalau baadhi ya dinosaria walikuwa wazazi wazuri," Profesa Barrett anasema.

"Ndio, kulikuwa na wengine ambao hawakuwa."