Kamoʻoalewa: "sayari" ya ajabu iliyogunduliwa karibu na Dunia, ikoje na nini asili yake?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa miaka michache, wanasayansi wamekuwa wakishangaa ni nini hasa asili ya sayari ndogo iliyopewa jina la Kamo`oalewa. Sayari hii iligunduliwa mnamo 2016. Na wanasayansi walichojua wakati huo ni kwamba iko karibu na Dunia, lakini hawakujua mengi zaidi.
Hata hivyo utafiti mpya, umeongeza jambo jipya kuhusu asili yake ya ajabu: inaweza kuwa kipande cha Mwezi wetu wenyewe.
"Haionekani kama ni ya kawaida kwa kile tulichokitarajia," anasema Benjamin Sharkey, mtaalama wa masuala ya sayari kutoka Chuo Kikuu cha Arizona na mwandishi mkuu wa utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la Nature.
Mfanyakazi mwenzake wa Venezuela, Juan Sánchez, ambaye alishiriki katika uchunguzi huo, anaiambia BBC Mundo: "Labda inaweza kuwa imetokea kwa sababu ya mgongano kati ya Mwezi na kimondo. Inawezekana ilikoa kutoka kwenye uso wa Mwezi."
Ingawa njia pekee ya kujua asili ya Kamo`oalewa ni kwa kupata sampuli, jambo ambalo linaweza kutokea muongo huu, wanasayansi wana mambo kadhaa ya kuzingatia kuwa nadharia yake kama ni sahihi.
Kamo`oalewa ni kitu gani?
Kamo`oalewa (zamani ikijulikana kama 2016 HO3) iligunduliwa mwaka wa 2016 na darubini ya Pan-STARRS 1, ambayo iko Hawaii. Wanasayansi waliipa jina kwa Kihawai ambalo linaweza kutafsiriwa kwa Kihispania kama "kipande cha angani kinachozunguka."

Chanzo cha picha, NASA/JPL-Caltech
Ina urefu wa takribani mita 40 na inachukuliwa kitaalamu kama "quasi satellite" , si "mwezi".
"Iko karibu na sayari yetu inapozunguka Jua," anaelezea BBC Mundo Sánchez, ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Venezuela.
Tofauti na Mwezi, Kamo`oalewa haizunguki Dunia. Ndiyo maana ikiwa sayari yetu ingetoweka, mwamba huu ungefuata mzunguko wake wa sasa. Wanasayansi hadi sasa wamegundua sayari 'quasi-satellites' tano, lakini wameweza tu kusoma sayari hii ndogo ya Kamo`oalewa.
"Ni rahisi kuitazama hii kuliko satelaiti nyingine zinazojulikana. Mara moja kwa mwaka, wakati wa mwezi wa Aprili, kitu hiki kinang'aa vya kutosha kuweza kuangaliwa kwa darubini kubwa kutoka duniani," anasema Sánchez.
Nyingine hazionekani sana na hazikuweza kuchanganuliwa.
Mwamba

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati wa kuchunguza sayari hii ndogo, wanasayansi waligundua kwamba ilikuwa na rangi nyekundu isiyo ya kawaida, ishara ya kuwepo kwa madini ya metali.
"Kwa maneno rahisi, kimsingi tulichofanya ni kusoma jinsi mwanga wa jua unavyoakisiwa juu ya uso wa kitu hiki ili kujaribu kubaini kimeundwa na kitu gani. Tulichogundua ni kwamba kitu hicho kimetengenezwa kwa madini ya silicate," anasema Sánchez.
Wanasayansi hao pia walidokeza kwamba jiwe pekee linalojulikana kama mwamba ni lile la sampuli ya mwezi iliyorejeshwa kwenye misheni ya Apollo katika miaka ya 1970.

Chanzo cha picha, Tony873004
"Hatuna uhakika wa 100%. Njia pekee ni kupata sampuli za kitu hiki ili kuwa na uhakika," anasema Sánchez.
Na kupata sample huenda ikawa sio jambo gumu hivyo.
Ikiwa mipango ya China itaendelea vyema, muongo huu Beijing itazindua misheni ya roboti ambayo itatembelea Kamo'oalewa na kuleta sampuli.
Kisha inaweza kuthibitishwa ikiwa Kamoʻoalewa ni sehemu ya Mwezi wetu tunaoujua ama la.













