Unajua unaweza kufungwa jela 'kirahisi' bila hatia yoyote?

Mkazi wa North Carolina Marekani ambaye alifungwa kwa mauaji na kukaa jela kwa miaka 26 ameachiwa huru baada ya msamaha wa Gavana. Dontae Sharpe amepambana kwa muda mrefu kuthibitisha kutokuwa na hatia wala kuhusika na mauaji tangu akamatwe mwaka 1994. Aliachiliwa kutoka gerezani mnamo Agosti 2019. "Jina la familia yangu limesafishwa," aliwaambia wanahabari siku ya Ijumaa. "Ni mzigo kutoka kwa mabega yangu na mabega ya familia yangu." Habari hizi zinafuatia makala ya BBC kuhusu kukiukwa kwa haki katika kesi yake.

Simulizi ya Bw Sharpe iliangazia jinsi inavyoweza kuchukua muda mrefu hata miaka na miaka kupata msamaha kamili hata baada ya mtu huyo kuondolewa hatia na kupata uhuru wake. Gavana Roy Cooper alisema katika taarifa yake wakati akitangaza msamaha huo kwamba alipitia kwa makini kesi hiyo, na wale ambao wamehukumiwa kimakosa kama vile Bw Sharpe "wanastahili kupewa haki hiyo kikamilifu na hadharani".

Kwa msamaha huu kamili, Bw. Sharpe ataweza sasa kuwasilisha ombi la kulipwa fidia kutoka kwa serikali kwa kufungwa kimakosa. "Uhuru wangu bado haujakamilika kwa kuwa wapo watu wengine gerezani kimakosa, waliohukumiwa kimakosa, na watu wanaosubiri msamaha," Bw. Sharpe aliongeza. "Nimeingia huko na najua kuna watu ambao hawana hatia na wanajua kuwa mfumo wetu ni mbovu na unahitaji kubadilishwa."

Alipatikana na hatia kwa kesi ya mauaji ya daraja la kwanza akidaiwa kumuua George Radcliffe. Lakini miezi kadhaa baada ya kesi hiyo, kijana mmoja aliyekuwa shahidi upande wa serikali alikanusha ushuhuda wake. Pamoja na kijana huyo kukanusha lakini bado ilichukua zaidi ya miongo miwili kwa Bw. Sharpe kuachiliwa huru na kuachiliwa kutoka gerezani.

Mtandao wa law.umich.edu ulioweka ripoti kuhusu watu waliofungwa kimakosa inayoratibiwa na shule za sheria za Chuo Kikuu cha California na kile cha Michigan, inayoonyesha idadi kubwa ya watu waliokaa ndani kimakosa. Inaonyesha pia licha ya Mahakama kuwaona hawana hatia kupitia rufaa zao, bado walichelewa sana kufutiwa makosa yao. Chapisho hilo linataja jumla ya mashitaka 2,887 yalifutwa tangu mwaka 1989 huku maisha ya watu 25,600 yakipotea.

Kwa mfumo wa haki kwa nchi za Afrika hauwezi kuwekwa kando, kwa kushuhudia maelfu kwa maelfu ya watu wakifungwa bila makosa. Wengine wakiachiwa na wengie wakiendelea kutosa jela.

Kwa mfano wa Sharpe na wafuatao, unaweza kusema yoyote anaweza kuhukumiwa kimakosa kesho na kutumikia kifungo jela bila kuwa na hatia, tena unaweza kufungwa kirahisi kwa ushahidi wa uongo unaoweza kushawishi mahakama. Wanasheria wengi wanaeleza namna nzuri ya kuwa salama ni kuepuka mazingira yoyote yanayoweza kukuingiza kwenye majaribu ya mashitaka, yakiwemo ya kijinai.

Licha ya kuwa wengi, hawa ni wachache ambao walishika vichwa vya habari duniani kwa kufungwa kimakosa, hawakuwa na hatia, ila ushahidi uliotolewa uliwaingiza kwenye hatia lakini baadae, ilionekana na Mahakama za juu kuwa hawakuhusika na makosa yao kabla ya kuachiwa huru na kuondolewa mashitaka.

Antony Maza (Marekani)

Alikaa jela miaka 47 na miezi miwili kuanzia mwaka 1973 mpaka mwaka 2021. Alihukumiwa kwa kosa la kumuua Meneja wa Benki, Peter Armata kabla ya Mahakama ya juu kumuona hata hatia na kufutiwa mashitaka Machi 3, mwaka 2021.

Richard Phillips (Marekani)

Mnamo Desemba 14, 2017, Richard Phillips mwenye umri wa miaka 71, aliyepatikana na hatia ya mauaji mwaka wa 1972 huko Detroit, Michigan, aliachiliwa baada ya hatia yake kuondolewa. Upande wa mashtaka ulitupilia mbali mashtaka hayo Machi 2018. Phillips alitumikia kifungo cha miaka 45 na miezi miwili gerezani.

James Richardson

Usimchanganye na mwandishi na mtangazaji wa Televisheni maarufu ama yule mkai wa mcheza mchezo wa vishale duniani (Darts), wenye majina ya James Richardson, huyu ni wingine. Janga la familia lilisababisha hatia isiyo sahihi kwa James Joseph Richardson ambapo mwaka 1967, alipatikana na hatia kufuatia vifo vya watoto wake saba vilivyotokana na kupewa sumu. Mlezi wa watoto, jirani Betsy Reese, awali aliongoza polisi kwenye ushahidi wa sumu. Baada ya miaka 21 ya kukaa gerezani, ikiwemo mitano ya hukumu ya kifo, nadharia mpya ilibadilisha kesi hiyo. Reese aliyezeeka alikiri jambo kwa kusema "Niliua watoto hao." Wapelelezi walifufua tena kesi hiyo na kugundua kuwa alikuwa wa mwisho kuwalisha watoto na alikuwa na chuki binafsi dhidi ya Richardson. Richard aliachiliwa huru mnamo Aprili 25, 1989

Anthony Porter

Ni kama filamu vile, Anthony Porter alikuwa na masaa 50 kabla ya kifo chake (kunyongwa), baada ya kupatikana na hatia ya kuwapiga risasi na kuwaua wanandoa wa Chicago, mwaka 1982. Alihukumiwa hukumu ya kifo mwaka 1983 na kutumikia miaka 17 kusubiri kunyongwa. Kilichochelewesha kutekelezwa kwa hukumu yake ni kwamba walikuwa wanamchunguza kuona kama ana tatizo la akili. Muda huo wa kumchuguza ikawa nafasi kwa Profesa David Protess wa Shule ya Uandishi wa Habari ya Medill, mpelelezi binafsi na timu yake ya wanafunzi wa kufungua upya kesi hiyo kama sehemu ya mfunzo kwa vitendo. Ndipo akajitokeza mtu mwingine Alstory Simon aliyekiri kuwaua wanandoa hao kupitia mkanda wa video na Porter akaachiliwa huru mwaka wa 1999. Cha kufurahisha ni kwamba, hukumu ya Alstory Simon aliyekiri pia iliondolewa baada ya mahakama kupata mbinu zilizotumiwa na mpelelezi binafsi na profesa si halali.

William Dillon

Hukumu isiyo sahihi iliharibu maisha ya William Dillon ya umaarufu kwenye mchezo wa besiboli. Mnamo 1981, kijana huyo akiwa na miaka 21 alionwa na wasaka vipaji wa Detroit Tigers. Siku chache kabla ya majaribio, alikamatwa na Polisi kwa kumpiga James Dvorak. Ingawa Dillon hakuendana na maelezo yaliyotolewa ya kumtambua mshukiwa na hata hakuwepo eneo moja na mwathiriwa wakati wa tukio, alihukumiwa kifungo cha maisha. Mnamo 2007, rufaa ya ushahidi wa kutumia vinasaba 'DNA' ilifanikiwa na Dillon aliondolewa mashitaka. "Nataka tu kuwatia moyo watu na kuwaonyesha unaweza kutoka mahali pasipo na matumaini".