Man Utd: David de Gea ataja kipigo cha 4-1 cha Watford kuwa 'cha aibu'

De gea

Chanzo cha picha, Getty Images

Mlinda mlango wa Manchester United David de Gea anaelezea kushindwa kwa timu yake 4-1 na Watford kama "aibu" na "jinamizi lingine".

Mkufunzi wa United Ole Gunnar Solskjaer anakabiliwa na wakati mgumu baada ya timu yake kushuka hadi nafasi ya saba kwenye Ligi ya Premia,

Nahodha Harry Maguire alitupwa nje ya uwanja wa Vicarage Road na penati ya Hornets pia kuokolewa.

"Ni aibu kubwa vile tulivyocheza leo," De Gea aliambia BBC Spor akiashiria mechi ya Jumamosi.

"Kipindi cha kwanza kilikuwa duni sana - haikubaliki kwa klabu hii na kiwango cha wachezaji tuliyo nao. Ni jinamizi lingine. Hali imekuwa na ugumu lakini sijui la kusema.

"Nimekuwa katika wakati mgumu na klabu hii lakini tuko katika hali ngumu - hatujui la kufanya na mpira, tunaruhusu mabao mengi. Ni wakati wa kutisha.

"Ni rahisi kumlaumu koch ana mambo mengine lakini wale walio uwanjani ni wachezaji na ni wao wanastahili kufunga mabao na kupambana uwanjani. Tunahitaji kujitathmini wenyewe na kupatia klabu na mashabiki wanachostahili. Ni vigumu kusema kwa nini kulikuwa na mchezo kama huu - sijui la kusema.

"Ni vigumu kuwa kwenye chumba cha kubadilishia nguo sasa - tuna huzuni, tuna hasira. Binafsi nimeumia - ni wakati mgumu sana kwa klabu nzima."

'Mabadiliko hayaepukiki

Mkufunzi wa Man United Olegunnar Solskjaer

Chanzo cha picha, PA Media

Maelezo ya picha, Mkufunzi wa Man United Olegunnar Solskjaer

United watasafiri hadi Villarreal katika Ligi ya Mabingwa siku ya Jumanne kabla ya kumenyana na viongozi wa Ligi ya Premia Chelsea uwanjani Stamford Bridge Jumapili, Novemba 28.

Mechi yao dhidi ya Arsenal, Crystal Palace, Young Boys na Norwich itafuata kabla ya katikati ya Desemba.

Beki wa zamani wa Arsenal Martin Keown alisema mustakabali wa Solskjaer sasa unaonekana kuwa "hatarini".

"Yeye ni mmoja wao, sehemu ya familia katika klabu hiyo lakini hawawezi kupuuza kwa kuwa yeye ni sehemu ya tatizo," alisema Keown kwenye makala ya michezo ya BBC Final Score.

"Mabadiliko hayaepukiki. Inaonekana ni hatari kwa meneja.

"Bao hilo la mwisho la Watford lilihusu shauku na hamu. Mabeki walikuwa wapi? Hawakuwa na nguvu za kutosha."