Nike Vaporfly: IAAF kutoa uamuzi kuhusu viatu 'vinavyowawezesha' wanariadha fulani

Shirikisho la riadha duniani IAAF linapanga kuimarisha sheria zake kuhusu viatu vya kiteknolojia vinavyotumiwa na wanariadha.

Bodi ya shirikisho hilo imekuwa ikiangazia mapendekezo ya kundi moja la wataalam huku ikitarajiwa kutoa tangazo lake siku ya Ijumaa.

Huku kukiwa na hofu ya tishio la kisheria, jopo hilo limeamua kutoweka marufuku ya jumla kwa viatu vya Nike aina ya Vaporfly range, kulingana na BBC Sport.

Lakini baadhi ya sampuli hiyo ya viatu huenda ikapigwa marufuku katika mashindano makubwa chini ya sheria mpya za muda inayolenga kuleta uwazi kabla ya kufanyiko kwa michezo ya Olimpiki itakayoanza mwezi Julai mjini Tokyo.

Sheria hizo zitaweka masharti ya viatu vyenye soli kubwa , ijapokuwa pia kutakuwa na tangazo la muda mrefu la teknolojia iliotumika katika mbio fupi na ndefu.

Watengenezaji viatu watatakiwa kutoa mfano wowote wa viatu kwa bodi hiyo ya riadha ili kuidhinishwa kabla ya kutumika katika mashindano makubwa na baadaye kuzuia teknolojia nyengine yoyote mpya hadi baada ya mashindano ya Olimpiki.

Hatahivyo rekodi zote zilizowekwa kwa kutumia viatu hivyo zitaendelea kuheshimiwa.

Kilichotokea

Sheria zilizopo zinasema kwamba viatu havifai kutengenezwa hali ya kwamba vitamwezesha mwanariadha ama kumpa fursa na kwamba aina yoyote ya kiatu itakayotumika ni sharti itumike na wote ili kutoa fursa ya sawa.

Lakini wakosoaji wanasema kwamba hiyo haitoshi na kwamba sheria hiyo imepitwa na viatu hivyo vinavyogharimu £240) na ambavyo vimebadilisha mbio ndefu tangu vilipozinduliwa 2016.

Wengi sasa wana wasiwasi kwamba tekonoljia hiyo imechafua vitabu vya rekodi , inazuia ushindani wa usawa miongoni mwa wanariadha wasiodhaminiwa na Nike hatua inayofanya kuonekana kama ulaghai wa kiteknolojia.

Wengine hatahivyo wanaamini kwamba uvumbuzi wa vifaa vya michezo ni miongoni mwa maendeleo katika michezo na hatua inayofanya wengine kubuni teknolojia zao na kwamba rekodi mpya zinasaidia kuleta hamu ya kiteknolojia.

Kinyume na mjadala na utata ulioletwa na viatu hivyo, Shirikisho la riadha duniani sasa litalazimika kufanya kile kinachoonekana kuwa uamuzi muhimu katika historia ya michezo.

Kwa mujibu wa Nike kiatu hicho kilichoongezwa urefu kina springi inayosaidia kumwezesha mwanariadha kukimbia zaidi kwa silimia 4 pekee.

Mwaka uliopita viatu kama hivyo vilitumiwa na Eliud Kipchoge wakati alipokuwa mwanariadha wa kwanza duniani kukimbia mbio za marathon chini ya saa mbili akitumia viatu aina ya Alphafly mjini Vienna na baadaye vikatumiwa na mwanariadha mwenza kutoka Kenya Brigid Kosgei mjini Chicago wakati alipovunja rekodi ya muda mrefu ya Paula Radcliffe upande wa wanawake.

Hatahivyo haijulikani iwapo viatu hivyo vipya vitaafikia sheria mpya inayotarajiwa kutangazwa na shirikisho la riadha duniani.

Shirikisho hilo limesema kwamba haipo wazi kwamba kuna teknolojia inayoweza kumpatia mwanariadha fursa iliopo kinyume na maadili ya michezo.

Lilisema: Changamoto ni kutafuta usawa katika sheria za riadha na wakati huohuo kuwatia moyo wavubvuzi kuendelea kutoa teknolojia mpya na kufuata sheria zinazosimamia mchezo huo.

Utafiti uliofanywa na gazeti la New York Times unasema kwamba kati ya mbio nyingi zilizokimbiwa kwa kutumia viatu aina ya Vaporfly, waliovitumia viatu hivyo waliwezeshwa kukimbia asilimia 4-5 zaidi ya vile ambavyo wangekimbia kwa kutumia viatu vya kawaida.