Ferland Mendy: 'Nilikuwa siwezi hata kusimama, lakini sasa niko klabu ya Real Madrid'

Mchezaji mpya wa Real Madrid Ferland Mendy anasema kuwa aliambiwa kuwa huenda asicheze tena soka baada ya upasuaji aliofanyiwa akiwa na umri wa miaka 15 kumfanya kutembea kwa usaidizi wa kiti cha kutumia magurudumo.

Beki huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 24 alijiunga na Real kwa kandarasi ya miaka sita kutoka Lyon wiki iliopita katika kandarasi ilio na thamani ya £47.1m.

''Nilikuwa katika kiti cha magurudumo kwa muda na nilihudumia kipindi cha kati ya miezi sita hadi saba nikiwa hospitali nikifanyiwa marekebisho ili niweze kutembea'', alisema Mendy.

''Waliniambia kwamba siteweza kucheza tena. lakini sasa niko katika klabu ya Real Madrid''.

Miaka miwili iliopita , Mendy alikuwa bado akiichezea klabu ya daraja la pili ya Le Havre kabla ya kujiunga na Lyon mwezi Juni 2017.

Alicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa dhidi ya Uruguay mnamo mwezi Novemba.

''Mwanzo sikuamini'' , Mendy alisema kuhusu uhamisho wake katika klabu ya Real Madrid.

''Hii ni klabu kubwa na kuweza kutia saini nao kwangu mimi ni kitu kizuri sana'' .

''Nimefurahia sana na natumai kwamba kila kitu kitakwenda sawa''.

Kuwasili kwa Mendy kumefanya gharama ya Real Madrid msimu huu kukaribia £300m.

Klabu hiyo tayari imemsajili mshambuliaji wa Ubelgiji Eden Hazard kutoka Chelsea kwa dau ambalo linaweza kuwa zaidi ya £150m, pamoja na mshambuliaji wa Serbia Luca Jovic kutoka klabu ya Eintracht Frankfurt kwa dau la £53m.

Mnamo mwezi Machi , walimsaini beki wa Porto Eder Militao kwa dau la £42.7m.