Manchester City 2-1 Liverpool: Man City wapunguza uongozi wa Liverpool hadi alama nne

Chanzo cha picha, Getty Images
Manchester City wamefufua kinyang'anyiro cha ubingwa Ligi ya Premia baada ya kufikisha kikomo mkimbio wa Liverpool wa kutoshindwa mechi 20 tangu mwanzo wa msimu.
Ushindi wa City umepunguza uongozi wa Liverpool kileleni hadi alama nne.
Vijana wa Pep Guardiola walifahamu kwamba wasiposhinda kwenye mechi hiyo Etihad, wangekuwa hawajajitendea haki.
Leroy Sane alifunga bao la ushindi dakika 18 kala ya mechi kumalizika kutokana na pasi kutoka kwa Raheem Sterling, dakika nane baada ya Roberto Firmino kuwasawazishia Liverpool.
Sergio Aguero alikuwa awali amewapatia City bao la kwanza.

Chanzo cha picha, Reuters
Kulikuwa na kioja wakati mmoja pale mshambuliaji wa Liverpool Sadio Mane alipoupiga mpira na kutikisa mlingoti wa goli la City na kabla haujaingiawavuni, beki wa City John Stones akafanikiwa kuuondoa kabla haujavuka kwenye mstari baada ya mara ya kwanza mpira huo kuonekana kumgonga kipa Ederson. Takwimu zinaonesha mpira huo ulikuwa umesalia na 1.12cm kuvuka mstari wa goli.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pep Guardiola: Kila mechi ni kama fainali
Meneja wa Manchester City Pep Guardiola akizungumza na BBC baada ya mechi, alisema: "Nawaonea fahari (wachezaji wangu) , lakini sio tu kwa leo tu. Tulishindwa mechi mbili katika siku nne, lakini hauwezi kusahau yale ambayo tumeyatenda kwa miezi 16. Tulijua kwamba ingekuwa ni kama fainali leo, tungeshindwa basi ingekuwa ni mambo kwisha.
"Hongera kwa wachezaji hawa wazuri ajabu. Hivi ndivyo tunahitajika kucheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya. Timu zote mbili zilijaribu kushambulia, hatukuwa na wasiwasi, hatukuwa na woga, na tulikuwa na presha sana.
"Wao ni viongozi, ni alama nne lakini tumepunguza mwanya. Tulifahamu kwamba tungeshinda mechi hiyo tungekuwa na nafasi ya kushindania ubingwa Ligi ya Premia, tukishindwa basi ndoto kwisha.
"Sikumbuki ni ligi ligi ilikuwa ngumu hivi, kuna klabu nyingi kubwa zinazoshindania taji. Kila mechi ni kama fainali."

Chanzo cha picha, Reuters
Jurgen Klopp: Bahati haikusimama
Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp aliambia Sky Sports kuwa: "Kulikuwa na presha sana. Ilikuwa mechi kali na ya kasi. Tulikosa bahati nyakati muhimu za kutaka kufunga bao. Tulikosa bahati zaidi ya City, ninaweza kusema hivyo.
"Walikuwa na nyakati ambazo walidhiti mchezo na kila mtu alihisi ukali wao. Kisha, tulirejea na tukawa na nafasi kubwa. Huwa hivi nyakati zote. Ni lazima ufunge ukipata nafasi hizi. Aguero anapofunga, hakuwa katika nafasi nzuri sana. Nafasi sawa na hivyo tulipoipata, hatukufunga.
"Haikuwa mechi bora zaidi kwetu au kwa City kwa sababu tulifanya mambo kuwa magumu kwa timu hiyo nyingine. Nishawaambia vijana wangu kwamba ni sawa. Tulishindwa lakini ilitarajiwa wakati mmoja. Usiku huu haikuwa vyema lakini si kwamba ndilo tatizo kubwa zaidi."
Nini kinafuata
Ni mechi za Kombe la FA sasa Manchester City wakiwa wenyeji wa Rotherham Jumapili nao Liverpool wawe wageni wa Wolves Jumatatu













